Papa Francisko amemteua Kardinali Jean-Claude Hollerich kuwa Mwezeshaji mkuu wakati wa maadhimisho ya Sinodi XVI ya Maaskofu 2021-2023. Papa Francisko amemteua Kardinali Jean-Claude Hollerich kuwa Mwezeshaji mkuu wakati wa maadhimisho ya Sinodi XVI ya Maaskofu 2021-2023. 

Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2023: Mwezeshaji Mkuu Ateuliwa

Kardinali Jean-Claude Hollerich, S.I. kuwa Mwezeshaji mkuu katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2021-2023. Sinodi hii, inanogeshwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho ya Sinodi kuanzia sasa yataanza kwa kuyashirikisha Makanisa mahalia kama chombo cha uinjilishaji mpya kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Kardinali Jean-Claude Hollerich, S.I. kuwa Mwezeshaji mkuu katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2021-2023. Sinodi hii, inanogeshwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu, kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kila mwamini kadiri ya dhamana, wito na nafasi yake katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu, ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine, na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa watu wa Mungu katika ujumla wao.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Mwezi Oktoba 2021: Mchakato wa Awamu ya Kwanza utayahusu Makanisa Mahalia na Taasisi zote za Kanisa: Oktoba 2021 hadi Aprili 2022. Makanisa mahalia yatatumiwa mada na maswaili dodoso yakufanyiwa kazi. Awamu ya Pili ni kuanzia Septemba 2022 hadi Machi 2023. Lengo kuu ni kuhamasisha majadiliano katika ngazi ya Mabara, ili hatimaye, kutengeneza Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris”. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023 na wajumbe watakaokuwa wameteuliwa watashiriki katika Sinodi itakayoadhimishwa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Lengo kuu ni Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya.

Sinodi 2021-2023
09 July 2021, 16:31