Kardinali Pietro Parolin katika kumbukumbu ya Miaka 1300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Odilia, amewataka waamini Barani Ulaya kuwekeza katika Fadhili za Kimungu. Kardinali Pietro Parolin katika kumbukumbu ya Miaka 1300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Odilia, amewataka waamini Barani Ulaya kuwekeza katika Fadhili za Kimungu. 

Bara la Ulaya Wekezeni Katika: Imani, Matumaini na Mapendo!

Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa Bara la Ulaya kuwekeza katika matumaini, imani na upendo, mambo msingi katika utume wa Kanisa kwa wakati huu. Kwa muda wa miaka 90 waamini wa Jimbo kuu la Strasbourg wamekuwa wakifanya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu: Usiku na mchana! Miaka 1300 tangu afariki Mt. Odilia shuhuda wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mtakatifu Ottilia wa Alsace ambaye kwa wengine anajulikana kama Mtakatifu Odilia Alsace, alizaliwa kunako mwaka 662 BK. Ni msimamizi wa mji wa Alsace nchini Ufaransa. Mwaka 2021, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 1300 tangu alipofariki dunia kunako mwaka 720. Odilia maana yake ni “Mwanga wa Mungu”. Kutokana na upofu wake tangu kuzaliwa, ingawa alikuwa anatoka kwenye ukoo wenye uwezo mkubwa, lakini alitengwa na hatimaye kujikuta akiwa analelewa na watawa wa Alsace kwa imani na upendo mkuu. Akabatizwa akiwa na umri wa miaka 15, na hapo akapata muujiza wa kuweza kuona tena, ndiyo maana akaitwa “Odilia, maana yake, Mwanga wa Mungu.” Kwa muujiza huu, akabahatika tena kurejea kwenye familia yake, lakini Mtakatifu Odilia alitamani kuendelea kuishi maisha ya kitawa, ili kuwasaidia wagonjwa, wazee, maskini na wasiojiweza. Baadaye akajiunga na Wamonaki na kubahatika kuanzisha Monasteri mbili huko Hohenburg, ambazo leo hii zimekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii mjini Alsace.

Lakini muujiza mkubwa ni toba na wongofu wa baba yake mzazi ambaye hapo awali, alielemewa sana na malimwengu pamoja na ukatili mkubwa dhidi ya binti yake! Kwa neema ya Mungu akaongoka na kuwa msaada mkubwa uliomwezesha Mtakatifu Odilia kutekeleza ndoto yake ya kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini. Baba huyu aliyekuwa na uchu wa fedha na mali, akatumia utajiri huu kwa ajili ya kujenga Kanisa kubwa, mahali pa kumwabudia Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Odilia akafariki dunia kunako mwaka 720 na kutangazwa na Papa IX kuwa Mtakatifu kwenye Karne XI. Na Papa Pio wa XII kunako mwaka 1946 akamtangaza kuwa ni Msimamizi wa Mji wa Alsace. Jimbo kuu la Strasbourg nchini Ufaransa, tarehe 13 Desemba 2020 lilizindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Odilia, Msimamizi na Mwombezi wa wagonjwa wa macho.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kuwa ni Mwakilishi wake wa Kitume katika Maadhimisho ya Miaka 1300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Odilia anayeadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 13 Desemba. Lakini, Jumapili tarehe 4 Julai 2021, Jimbo kuu la Strasbourg limeadhimisha Jubilei hii.   Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa Bara la Ulaya kuwekeza katika matumaini, imani na upendo, mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa kwa wakati huu. Kwa muda wa miaka 90 waamini wa Jimbo kuu la Strasbourg wamekuwa wakifanya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu: Usiku na mchana! Kardinali Parolin ametumia fursa hii pia kumweka wakfu Askofu msaidizi Gilles Reithinger wa Jimbo kuu la Strasbourg. Katika mahubiri yake, amewataka watu wa Mungu Barani Ulaya kugundua tena maana halisi ya mizizi ya utambulisho wao; kwa kutambua uwepo na uzito wa Msalaba katika maisha na utume wao, daima wakiwa na matumaini ya ufufuko na maisha ya uzima wa milele.

Matumaini ya maisha ya siku za mbeleni kwa mtu mmoja mmoja, familia na jamii katika ujumla wake na hata katika maisha na utume wa Kanisa yanasimikwa katika mchakato wa kuondokana na hofu isiyokuwa na mashiko katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hapa kuna haja kwa familia ya Mungu Barani Ulaya kuwekeza zaidi katika fadhila za kimungu ambazo zinaweka msingi, zinahuisha na kuainisha utendaji adili wa Mkristo. Imani ni fadhila ya kimungu ambayo kwako, waamini wanamsadiki Mungu, kile alichofunua na kukisema na ambacho Kanisa takatifu linawataka kusadiki na kuamini kwa sababu Mungu ndiye ukweli wenyewe! Matumaini ni fadhila ya kimungu inayowawezesha waamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele, kwa kutumaini ahadi za Kristo Yesu sanjari na msaada wa neema ya Roho Mtakatifu. Fadhila ya mapendo, inawawezesha waamini kumpenda Mungu kuliko kitu chochote kile na jirani kama wao wenyewe wanavyojipenda.

Mapendo ni tunda la Roho Mtakatifu na utimilifu wa Sheria. Kardinali Parolin anakaza kusema, watu wa Mungu Barani Ulaya hawana budi kuwekeza katika imani kwa Mwenyezi Mungu ambaye, kamwe hawezi kuwatelekeza watoto wake. Wanapaswa kujiaminisha katika nguvu za Kimungu na hususan nguvu za maisha ya kiroho. Fadhila hizi za kimungu zitawasaidia kujenga utamaduni wa upendo, amani na mshikamano wa kweli; kwa kujikita katika mshikamano na udugu wa kibinadamu. Huu ni udugu unaopaswa kumwilishwa katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ili waamini waweze kunogesha fadhila za kimungu katika uhalisia wa maisha yao, hawana budi kujenga urafiki na mafungamano thabiti na Kristo Yesu kwa njia ya: Neno lake, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mwishoni mwa mahubiri yake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amewataka watu wa Mungu Barani Ulaya, kumwomba Mtakatifu Odilia, ili waweze kuishi kikamilifu upya wa maisha kama alivyojitahidi kuishi, kwa kufungua macho yao kwa Mwenyezi Mungu anayeongoza mapito ya maisha yao!

Mtakatifu Odilia
06 July 2021, 16:10