Tafuta

Kardinali Pietro Parolin, Dhamana na Utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu. Kardinali Pietro Parolin, Dhamana na Utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu. 

Kardinali Pietro Parolin: Dhamana na Utume wa Kanisa Katika Jamii!

Kanisa linapenda kukuza na kudumisha uhusiano mwema na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa linapenda kuendeleza utume wake wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa halihitaji upendeleo wa pekee na halina mpango na wongofu wa shuruti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia Jumamosi tarehe 17 hadi Jumatatu tarehe 19 Julai 2021 amekuwa akifanya hija ya kitume kwenye Ufalme wa Monaco. Hii ni sehemu ya kumbukizi la miaka 40 tangu Vatican na Ufalme wa Monaco walipotiliana saini itifaki ya makubaliano kuhusu uteuzi wa Askofu mkuu, hapo tarehe 30 Julai 1981. Mtakatifu Yohane Paulo II akalipandisha hadhi Jimbo la Monaco na kuwa ni Jimbo kuu hapo tarehe 25 Julai 1981. Huu ulikuwa ni uamuzi mzito katika kukuza na kudumisha umoja wa Kanisa pamoja na kuendeleza ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Pamoja na mambo mengine, Jumapili asubuhi, tarehe 18 Julai 2021, Kardinali Parolin ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Majira ya jioni amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na Mapadre, Watawa na Vyama vya Kitume kwenye Ufalme wa Monaco. Katika hotuba yake, Kardinali Parolin, amekazia kuhusu umuhimu wa kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Kanisa linapenda kukuza na kudumisha uhusiano mwema na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kanisa linapenda kuendeleza utume wake wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utume wa familia unapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa. Maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa waamini kutangaza na kushuhudia imani yao katika matendo. Kila kukicha ukanimungu unaendelea kuongezeka sehemu mbalimbali za dunia, hali inayochukua sura ya kisiasa na kijamii kwa madai ya uhuru, kiasi kwamba, baadhi yao wanataka kuona dini ikifutika machoni pa watu!

Kadiri ya mwanga angavu wa Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium” kuna haja ya kujenga na kudumisha uhusiano mwema kati ya Kanisa na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Hii pia ni sehemu ya utekelezaji wa haki msingi za binadamu zinazobubujika kutoka katika uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Mababa wa Kanisa wanasema, Kanisa linapotekeleza dhamana na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo haliombi upendeleo wa pekee na wala halitaki kufanya wongofu wa shuruti. Mama Kanisa anafurahi na kushangilia, pale ambapo Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kutolewa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama ilivyokuwa wakati wa Sherehe ya Pentekoste. Uinjilishaji wa kina usaidie familia ya binadamu kupambana na umaskini, ujinga na maradhi yanayoendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uinjilishaji hauna budi kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii inatokana na ukweli kwamba, uchafuzi mkubwa wa mazingira ni chanzo kikuu cha maafa yanayowatumbukiza watu katika umaskini, magonjwa na njaa.

Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kielelezo makini cha zawadi na nguvu ya Mungu kwa mwanadamu. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo kwa jirani zao, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma ya upendo, iwe ni chachu ya umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Lengo kuu ni kupambana na umaskini, ukosefu wa usawa, ubaguzi na nyanyaso dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sera na mikakati mbalimbali ya uchumi na maendeleo haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uchumi fungamani; kwa kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu. Kumbe, ushuhuda wa Injili usimikwe katika upendo, udugu wa kibinadamu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kuhusu utume wa familia zisaidie kunogesha maisha ya ndoa na familia kama kielelezo cha: ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu.

Kanisa liwasaidie vijana kuwajibika barabara katika mchakato wa ujenzi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kiasi hata cha kuthubutu kusema, “wewe utakuwa wangu wa kufa na kuzikana”. Yote haya yanawezekana ikiwa kama vijana watatambua kwamba, kuna jumuiya ya waamini inayowasindikiza na kuwategemeza katika mchakato wa safari yao ya maisha kama wanandoa na familia! Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote dhidi ya athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kusababisha umaskini mkubwa sehemu mbalimbali za dunia, anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukabiliana na changamoto hizi kwa kujikita katika kanuni maadili, utu wema na uwajibikaji wa kisayansi. Katika mchakato huu, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kuzingatia kanuni maadili yanayokita mizizi yake katika mshikamano na sera ya upendo, ili kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kardinali Parolin anakazia uhusiano uliopo kati ya kazi ya uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu na mwanadamu ambaye amekabidhiwa mazingira ili kuyatunza na kuyaendeleza. Haya ni kati ya mambo msingi yanayoendelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake!

Kardinali Parolin
19 July 2021, 15:40