Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC amefariki dunia tarehe 11 Julai 2021 Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC amefariki dunia tarehe 11 Julai 2021 

Kardinali Laurent M. Pasinya wa DRC Amefariki Dunia 11 Julai 2021

Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC alisimama kidete kupambana na ukosefu wa haki, amani na utulivu, kwani alitamani kuona dunia inasimikwa katika misingi ya haki, amani na udugu wa kibinadamu. Kanisa limempoteza kiongozi mashuhuri aliyeshikamana na kufungamana na watu wa Mungu katika hija ya maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC, amefariki dunia Jumapili tarehe 11 Julai 2021 Kwenye Hospitali ya “Clinique de l'Europe, Le Port-Marly”, Versailles nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 81 tangu kuzaliwa kwake! Kwa siku za hivi karibuni, hali ya afya yake ilidhohofu sana, kiasi cha kupelekwa nchini Ufaransa kwa matibabu zaidi. Kardinali Fridolin Ambongo Besungu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC anasikitika kusema kwamba, Kanisa nchini DRC, Afrika na Ulimwengu katika ujumla wake, limempoteza kiongozi mashuhuri. Kwa hakika alikuwa ni mtu wa Mungu mwenye imani thabiti. Aliwaheshimu na kuwathamini binadamu wenzake walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wenye haki, utu, heshima na haki zao msingi. Ni kiongozi aliyejisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kujikita katika uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, alisimama kidete kupambana na ukosefu wa haki, amani na utulivu, kwani alitamani kuona dunia inasimikwa katika misingi ya haki, amani na udugu wa kibinadamu.

Kanisa limempoteza kiongozi mashuhuri aliyeshikamana na kufungamana na watu wa Mungu katika hija ya maisha yao. Alitekeleza dhamana na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu, kama Padre, Askofu na hatimaye kama Kardinali mshauri wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kardinali Fridolin Ambongo Besungu wa Jimbo kuu la Kinshasa, anakaza kusema, Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya ameacha pengo kubwa ambalo haitakuwa rahisi sana kuliziba kwa siku za hivi karibuni. Habari ya kifo chake, imewajaza majonzi na masikitiko makubwa watu wa Mungu ndani na nje ya DRC. Atakumbukwa sana na watu wa Mungu nchini DRC kama kiongozi mwaminifu na mwenye imani thabiti. Alipenda kuona haki, amani, utu na heshima ya binadamu vinapewa kipaumbele cha pekee katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao na mafungamano ya kweli ya watu wa Mungu nchini DRC.

Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa nchini DRC alizaliwa tarehe 7 Oktoba 1939 huko Mongobelè. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi Chuo Kikuu cha Urbanian kilichoko mjini Roma, tarehe 21 Desemba 1963 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Ni kati ya wanafunzi mahiri wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Alibahatika kufundisha Maandiko Matakatifu na Taalimungu, Seminari kuu ya Mtakatifu Yohane XXIII pamoja na Kitivo cha Taalimungu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kinshasa, DRC. Tarehe 13 Februari 1980 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Inongo nchini DRC na kuwekwa wakfu tarehe 4 Mei 1980. Tarehe 7 Aprili 1981 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo wa kuu la Kisangani. Tarehe 1 Septemba 1988 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kisangani.

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1984 alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zaire kama ilivyojulikana wakati ule. Akawa ni kiongozi aliyejipambanua kuongoza mageuzi makubwa yaliyokuwa yanatendeka nchini Zaire, hadi kufikia ukomo wake kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, “Democratic Republic of Congo, DRC.” Katika mchakato huu, akasimamia haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini DRC. Alikosoa pale palipopinda, akapinga kwa nguvu zote kishawishi cha baadhi ya viongozi kutaka kupindisha Katiba ya nchi ili wabaki madarakani. Ni katika muktadha huu, Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, mara kadhaa ameponea chupu chupu kuuwawa kutokana na msimamo wake kuhusu utawala wa sheria, demokrasia, ustawi na maendeleo ya wengi. Tarehe 6 Desemba 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa. Amekuwa ni mshikiri mzuri katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu: Uinjilishaji na urithishaji wa imani ya Mwaka 2012, Changamoto za kichungaji kwa familia katika muktadha wa Uinjilishaji ya mwaka 2014, Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia ya mwaka 2015. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2013 akamteuwa kuwa ni kati ya Makardinali wake washauri katika mchakato wa kufanya mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican.

Amefariki dunia wakati Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” ikiwa katika hatua zake za mwisho mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 20 Novemba 2010 akamteuwa na kumsimika kuwa ni Kardinali. Mwezi Oktoba 2018 akang’atuka kutoka Baraza la Makardinali Washauri. Tarehe 1 Novemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia kung’atuka kwake kutoka madarakani. Na Jumapili tarehe 11 Julai 2021 akaiga dunia, akiwa amewatumikia watu wa Mungu kama Padre kwa muda wa zaidi ya miaka 57. Kama Askofu mwenye dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu ametumikia kwa miaka 41 na kama Kardinali miaka 10. Amefariki dunia akiwa na umti wa miaka 81.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa “Conférence des évêques de France​, CEF, limepokea taarifa ya kifo cha Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa nchini DRC kwa masikitiko makubwa. Huyu ni kati ya viongzo maarufu sana nchini DRC. Kwa hakika alikuwa ni kiongozi jasiri, mpenda haki, amani na upatanisho wa kweli. Ni kiongozi aliyezama katika majadiliano na upatanisho wa kitaifa nchini DRC. Shuhuda wa demokrasia na utawala bora unaozingatia sheria, kanuni na Katiba ya nchi. Familia ya Mungu nchini Ufaransa inapenda kuungana na Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema nchini DRC kuomboleza kifo cha Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya pamoja na kumwombea usingizi wa amani na maisha ya uzima wa milele!

Tanzia DRC

 

 

12 July 2021, 15:15