Askofu mkuu Emmanuel Adamakis katika mahajiono maalum na Vatican News anawahimiza Wakristo kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Askofu mkuu Emmanuel Adamakis katika mahajiono maalum na Vatican News anawahimiza Wakristo kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! 

Tangazeni na Kushuhudia Injili ya Kristo: Mateso, Kifo na Ufufuko

Katika mahojiano maalum kati ya Dr. Andrea Tornielli Mhariri mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia anaelezea umuhimu wa kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wakristo wasimame kidete kutunza mazingira na kukuza udugu wa kibinadamu.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa mwaka 2021 katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume tarehe 29 Juni 2021, unaongozwa na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia. Anafuatana na Askofu mkuu Iosif Bosch wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina pamoja na Shemasi Barnabas Grigoriadis kutoka kwenye Upatriaki huo. Katika mahojiano maalum kati ya Dr. Andrea Tornielli Mhariri mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia anaelezea umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Askofu mkuu Emmanuel Adamakis, anakazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama unavyofafanuliwa kwenye Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Hiki ni chombo madhubuti katika kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano, amani, haki jamii na udugu wa kibinadamu.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Katika mahojiano haya, amegusia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea yatakayoadhimishwa mwaka 2025. Askofu mkuu Emmanuel Adamakis, anasema, katika ulimwengu mamboleo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika imani juu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao wokovu na uzima wa milele. Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu anasema, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt 28:19-20.

Wakristo wanaitwa na kuhimizwa kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani yao kwa watu wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti; watu wenye hofu na mashaka, ili waweze kumtambua Kristo Yesu, Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Nyakati zote ni zake! Ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu, kuna haja kwa Wakristo kujiaminisha kwa Kristo Yesu na kuendelea kujikita katika Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Licha ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia, kuendelea kukumbana na dhuluma pamoja na nyanyaso, lakini hawana budi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa hata kwa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Waamini hao waliweza kuvumilia takribani miaka 300 ya dhuluma na nyanyaso. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kufanya rejea katika historia na maisha ya Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Watambue kwamba, wao wako ulimwenguni lakini si watu wa ulimwengu huu.

Askofu mkuu Emmanuel Adamakis, anasema, utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika maisha na utume wake, ameendelea kujipambanua kuwa ni kiongozi aliye mstari wa mbele katika kulinda, kutetea na kudumisha mazingira pamoja na huduma bora kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Familia ya Watu wa Mungu inapaswa kupokea Kazi ya Uumbaji kwa moyo wa shukrani kwa kutambua kwamba, mazingira ni sawa na “Kisakramenti” kinachofunua uwepo endelevu wa kazi ya Mungu hapa ulimwenguni. Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya amana, utajiri, urithi na imani ya Kanisa. Ukiunganisha Waraka wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” pamoja na"Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unapata msingi wa majadiliano ya kidini na kiekumene na kidini; umoja, upendo na mshikamano wa kidugu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene!

Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake! Kumbe, katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Wakristo wanapaswa kumuungama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chanzo cha imani, furaha na matumaini ya waja wake. Mwenyezi Mungu ni kiini cha majadiliano na watu wake na kamwe hajaacha kuzungumza na wanawadamu katika safari ya maisha yao hapa duniani, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale hata leo hii, Mwenyezi Mungu anazungumza na binadamu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi ni nyenzo msingi ya kupambana na imani na misimamo mikali ya kiimani na kidini. Kanisa linataka kuona misingi ya haki, amani na maridhiano inatawala akili na nyoyo za watu. Amani ya kweli haipatikani kwa njia ya mtutu wa bunduki wala ncha ya upanga! Mtakatifu Paulo Mtume, katika utenzi wake kuhusu upendo, anabainisha mambo msingi yanayofumbata upendo wa udugu wa kibinadamu; upendo hautafuti mambo yake! Rej. 1 Kor 13: 1-13. Upendo ni mafuta yanayopaswa kutumiwa kuganga na kuponya makovu na majeraha ya chuki na uhasama, ili kuondokana na mazalia mapya ya mambo kama haya.

Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2021-2023 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu, ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine, na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa jirani! Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Makanisa ya Kiorthodox ni sehemu ya vinasaba vyake.

Makanisa yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu kama Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Mwaka 2025 Makanisa yataadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso wa Nicea. Umoja wa Kanisa ulikuwa hatarini na hivyo pia kutishia amani na usalama hata katika masuala ya kisiasa.

Tangu mwanzo, Mababa wa Kanisa wameonesha umuhimu wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Kanuni ya Imani ya Nicea-Costantinopoli ndiyo bado inayoyaunganisha Makanisa pamoja na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Hili ni tulio litakaloadhimishwa kiekumene. Askofu mkuu Emmanuel Adamakis, anasema kwamba, hii ni fursa kwa waamini kusherehekea Pasaka ya Bwana, wakiwa wameungana, licha ya tofauti zao msingi. Maadhimisho ya Pasaka katika umoja na mshikamano wa dhati ni kati ya vipaumbele vya majadiliano ya kiekumene yanayoendelea kwa sasa! Kutangaza na kushuhudia ukweli wa Fumbo la Pasaka ni muhimu sana kwa waamini. Jubilei ya Miaka 1, 700 ni mlango kwa waamini kujadili kwa kina na mapana kuhusu Liturujia ya Kanisa na umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano wa Wakristo wote. Kalenda ya maadhimisho mbalimbali ya Kanisa bado ni “mwiba” unaoweza kusababisha mpasuko mkubwa miongoni mwa Wakristo. Maadhimisho haya yanaweza kuwa ni ushuhuda na msingi wa upatanisho miongoni mwa Wakristo!

Uekumene Majadiliano
28 June 2021, 14:19