Papa Francisko amempongeza Kardinali Polycarp Pengo kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Papa Francisko amempongeza Kardinali Polycarp Pengo kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. 

Papa Ampongeza Kardinali Pengo Miaka 50 ya Daraja ya Upadre!

Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu anampongeza pia kwa moyo, ari na juhudi za kichungaji alizozitekeleza katika Jimbo Katoliki la Nachingwea, Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi na hatimaye Dar es Salaam.

Na Remigius Mmavele, - Dar Es Salaam.

Baba Mtakatifu Francisko ametuma salamu za pongezi kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam katika Jubilei yake ya Miaka 50 ya Upadri. Katika salamu hizo kusomwa na Balozi wa Vatican nchini Tanzania Askofu Mkuu Marek Solczynski na kisha kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na katibu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam Padri Frank Mtavangu. Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Kardinali Pengo katika tukio hilo la furaha,barua hiyo ya pongezi inaeleza:  “Ndugu yetu mpendwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, pokea pongezi na salamu zetu unapoadhimisha miaka 50 tangu ulipopewa daraja ya Upadri, unapoadhimisha tukio hili la furaha tunakupongeza kutoka moyoni aidha tunakupongeza kwa Moyo na juhudi za kichungaji ulizozionyesha kwa upendo mkubwa kwa waamini wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam na kabla ya hapo waamini wa lililokuwa Jimbo la Nachingwea na baadae Jimbo la Tunduru-Masasi. Tunakutakia furaha na faraja tukikuaminisha kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu. kwa moyo mkunjufu na uliojaa upendo wa kindugu tunaungana nawe katika Sala tukikutakia Baraka kutoka katika mamlaka yetu ya Kitume”

Salamu hizo za Baba Mtakatifu zimetolewa Roma , Kanisa Kuu la Yohane wa Lateran Mei 25, 2021 na kusomwa kwa Kardinali Pengo na waamini wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam katika viwanja vya Msimbazi Juni 20, 2021katika adhimisho la misa takatifu ya Jubilee ya miaka 50 ya upadri wa Kardinali Pengo.  Juni 20, 2021 waamini wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam pamoja na waamini wengine kutoka majimbo ya karibu walikusanyika katika viwanja vya msimbazi kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu Mkuu mstaafu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kufikisha miaka 50 ya Daraja takatifu ya Upadri. Katika adhimisho la misa takatifu lililoongozwa na yeye mwenyewe ambalo lilihudhuriwa na Maaskofu wakuu kutoka majimbo makuu pamoja na maaskofu kutoka majimbo mengine nchini Tanzania. Katika mahubiri yake Askofu Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Katoliki Mpanda ameeeleza namna Kardinali Pengo alivyoacha alama nyingi za kichungaji Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam ambako amefanya utume kwa miaka 37. Askofu Nzigilwa amesema licha ya kuweka historia ya kuwa Padre wa kwanza Mtanzania kupewa Daraja ya Uaskofu na Mtakatifu Yohane Paulo II hapo Januari, 06, 1984. Kardinali Pengo ameacha alama nyingine nyingi jimbo kuu katoliki la Dar es Salaam ambazo majimbo mengine yameanza kuandaa mkakati wa kufuata kile kilichoanzishwa na Kardinali Pengo.

Maeneo mengine alikofanya utume ni Jimbo Katoliki la Nachingwea na baadae Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi alihimiza sana watu kulitegemeza kanisa kwa kuwashirikisha waamini wenyewe na kuachana na dhana ya kuwategemea wafadhili. Ndipo alipoanzisha “Tegemeza Jimbo” mwaka 1994 wakati huo Jimbo likiwa na parokia chache ambazo zilikuwa hazifiki hata thelathini, na katika Tegemeza Jimbo ya kwanza jimbo lilipata kiasi cha shilingi milioni kumi na saba. Licha ya kuanza kwa kiasi hicho kidogo cha Pesa Jimbo liliendelea kukua na kujenga mazoea ya kujitegemea hadi Kardinali Pengo anastaafu mwaka 2019 Jimbo limeweza kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni Tatu katika utaratibu huo wa Tegemeza Jimbo. Kardinali Pengo alianzisha utaratibu huo ili jimbo liweze kujitegemea katika uendeshaji wa shughuli zote za kichungaji jimboni bila kutegemea msaada kutoka kwa wafadhili. Mwaka 1996 Kardinali Pengo alianzisha Shirika la Kimisionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu ambalo linashirikisha watoto kutoka parokia zote zilizopo jimbo kuu katoliki la Dar es Salaam. Shirika la Kimisionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu limekuwa chachu ya umisionari kwa kufanya ziara za kimisionari katika parokia zilizopo pembezoni ambazo nyingi zinachangamoto kadhaa za kiuchungaji. Shirika la Kimisionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu ni shirika lenye Uhai na nguvu kubwa ya Kimisionari na Malezi yaliyobora kwa watoto.

Watoto wa Shirika la Kimisionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu wamefanya makongamano kadhaa katika parokia mbalimbali za Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam, wamefanya  mafungo pamoja na  ziara  za kimisionari katika parokia za pembezoni kama vile parokia ya Utete iliyopo Rufiji, parokia ya Mafia iliyopo kisiwani Mafia, hayo yote ni maeneo ambayo yanachangamoto kubwa mno za kimisionari na mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Kardinali Pengo alianzisha umisionari kupitia watoto wadogo ambao wanafanya ziara katika parokia hizo hususani Mafia ambako wana ratiba ya umisionari kwenda kufanya umisionari kila mwaka ifikapo mwezi Oktoba. Tangu wameanza kufanya umisionari katika kisiwa cha Mafia uinjilishaji umeshamiri maisha ya watu yamebadilika kwa kiasi kikubwa na idadi ya vigango imeongezeka. Maisha ya Umisionari ya Kardinali Pengo yaliendelea kushika kasi pale alipokuja na maono mapya ambayo yalizaa utaratibu wa Wanawake Wakatoliki Tanzania, (WAWATA) kwenda kuwategemeza vijana wa Seminari ya Visiga, WAWATA walipewa jukumu la kwa walezi wa Waseminari wa Seminari ya Visiga iliyopo Kibaha, Mkoani Pwani. Safari ya kwanza ya kuwategemeza waseminari wa Visiga ilifanyika mwaka 1992 Kardinali Pengo akiwa na WAWATA wachache wasiozidi ishirini wakiwa katika gari moja walikwenda kuwategemeza waseminari na kusali nao kwa pamoja.

Utaratibu huo wa WAWATA kuwategemeza waseminari wa seminari ya Visiga uliendelea na sasa hivi idadi ya WAWATA imeongezeka mara dufu ambapo kila mwaka wanakwenda kuwategemeza Waseminari wa Seminari ya Visiga wakiwa zaidi ya WAWATA elfu kumi na nne. WAWATA wanakwenda Seminari ya Visiga kusali na waseminari kisha kuwategemeza kwa mahitaji mbalimbali ikiwemo pesa taslimu ambapo mara kadhaa zaidi ya milioni mia moja zimekuwa zikitolewa. Baada ya utume wa WAWATA kuimarika zaidi Kardinali Pengo aliwageukia akina baba ambao ni Wanaume Wakatoliki (UWAKA) ambao aliwapa jukumu la kuwa walezi wa Masista wa Jimbo wa Shirika la Mtakatifu Fransisko ambao makao yao makuu yako Mbagala. Kuanzia mwaka 2008 UWAKA wakaanza rasmi ziara za kuwategemeza Masista wa Shirika la Dada Wadogo ambao walikuwa wanasali nao pamoja na kisha kuwakabidhi majitoleo yao katika siku za mwanzo idadi ya UWAKA waliokuwa wanashiriki katika ziara ilikuwa ni kati ya mia moja hadi mia tatu. Hadi Kardinali Pengo anastaafu idadi ya UWAKA imeongezeka kwa kiasi kikubwa sana hali ambayo imesababisha kubadilishwa kwa eneo la kufanyia misa pamoja na matoleo kwa dada wadogo. Misa na majitoleo sasa hivi vinafanyika nyumba ya malezi ya dada wadogo iliyopo eneo la visiga mkoani pwani. Ubunifu wa kiuchungaji wa Kardinali Pengo haukuishia hapo alihakikisha kwamba waamini wanapata huduma za Kiuchungaji kwa ukaribu zaidi hivyo alitafuta mapadri kutoka mashirika mengine na hata wakujitolea ili waweze kufanya utume jimbo kuu katoliki la Dar es salaam. Alihakikisha kuwa vigango vyote ambavyo vina uwezo wa kuwa parokia vinakuwa parokia haraka sana ili kuwapa tafasi waamini kuweza kupata huduma za kichungaji kwa ukaribu.

Katika miaka 27 ya Uaskofu wake Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alifungua parokia mpya 98 na hadi anastaafu mwaka 2019 idadi ya parokia alizoziacha ilikuwa imefikia 118 pamoja na parokia teule 12. Kardinali Pengo wakati anapokea Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam lilikuwa na parokia 20 tu. Hadi anastaafu Kardinali Pengo ameliwezesha Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam kuwa ndio lenye parokia nyingi kuliko majimbo mengine yote nchini Tanzania lakini pia katika ukanda wa AMECEA jimbo hilo pia linaongoza likifuatiwa na Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi, Kenya ambalo lina jumla ya parokia 114. Juni 20, 2021wakati Kardinali anasherehekea Jubilei ya Miaka 50 ya Upadri huku akiwa ameliachia kanisa katoliki alama nyingi zisizofutika kumbukumbu nyingine ni kuwa Juni 20, 1979 parokiani Mazye Kardinali alipata daraja takatifu ya Upadri akiwa na wenzake watatu na kufanya Jumla yao kuwa wanne lakini kati yao aliye hai hadi sasa ni Kardinali Pengo peke yake. Jubilei ya Miaka 50 ya Upadri ya Kardinali Pengo ilifanyika, Jumapili Juni 20,2021 ikiwa imefanana siku na siku yenyewe Juni 20,1979 ambayo ilikuwa Jumapili pia. Kardinali Pengo amefanya utume Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam kwa miaka 37. Miaka 6 kama Gambera Muasisi wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea wakati huo akiwa Padri. Miaka 31 akiwa Askofu ambapo alikuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam kwa miaka miwili pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam kwa kipindi cha miaka 27.

25 June 2021, 12:47