Vatican inasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana na hatimaye, kung'oa rushwa na ufisadi. Vatican inasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana na hatimaye, kung'oa rushwa na ufisadi. 

Simameni Kidete Kupambana Ili Kung'oa Rushwa na Ufisadi!

Vatican inaunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Umoja wa Mataifa ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi wa mali ya umma. Rushwa na ufisadi ni mambo yanayopekenya kanuni maadili na utu wema; umoja na mafungamano ya kijamii na hivyo kukwamisha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kupambana na ujinga, umaskini na maradhi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema rushwa ni mchakato unaoharibu na kuvunjilia mbali kabisa mafungamano, upendo na mshikamano wa binadamu. Rushwa inatia doa uhusiano kati ya binadamu, Mwenyezi Mungu na kazi ya uumbaji. Lakini kinyume cha rushwa ni: Uaminifu, uadilifu, utu wema, upole na unyofu wa moyo mambo yanayopania kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inaonesha maisha ya mwanadamu asiyekuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha, hali inayoharibu sana mafungamano ya kijamii. Matokeo yake ni kukomaa kwa uchoyo na ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko pamoja tabia ya kutowajali wengine. Rushwa inaonesha ile “roho ya korosho, roho ya kwa nini; roho ya kutu, roho iliyovunda na kuanza kutoa harufu mbaya”. Rushwa ni kikwazo katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inapelekea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Ni chanzo kikuu cha kuibuka na kusambaa kwa magenge ya kihalifu, kitaifa na kimataifa; magenge yanayochochea utamaduni wa kifo. Kimsingi, rushwa ni adui wa haki, utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kuna haja ya kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, kimaadili, kitamaduni na kiutu! Hii inatokana na ukweli kwamba, rushwa inapata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu! Rushwa ina tabia ya kujigeuza geuza kadiri ya mazingira na vionjo vya mtu, kumbe, hakuna anayeweza kujidai kwamba, rushwa ameipatia kisogo! Jambo la msingi ni kuwa macho na makini; kwa kukesha na kusali, ili kutokutumbukia majaribuni! Ni katika muktadha huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuanzia tarehe 3-4 Juni 2021 limekuwa likijadili kuhusu changamoto na mbinu mkakati unaopaswa kutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kuzuia na hatimaye, kupambana na rushwa na ufisadi! Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican anasema, Vatican inaunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Umoja wa Mataifa ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi wa mali ya umma. Rushwa na ufisadi ni mambo yanayopekenya kanuni maadili na utu wema; umoja na mafungamano ya kijamii na hivyo kukwamisha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kupambana na ujinga, umaskini na maradhi.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na maradhi duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, rushwa na ufisadi havina budi kung’olewa na watu kuanza kujielekeza zaidi katika utamaduni fungamani; haki jamii na nidhamu katika matumizi ya rasilimali fedha na vitu. Jamii ijenge na kudumisha utamaduni unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kufyekelea mbali uchoyo na ubinafsi!

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anakaza kusema, utawala wa sheria, nidhamu pamoja na kuzuia uhalifu ni mambo yanayopaswa kwenda sanjari. Haki ya kweli ni ile inayotoa fursa ya kuleta mabadiliko katika maisha ya mtu, kwa kusaidia maboresho: kiroho na kimwili pamoja na kumwelimisha mtu madhara yanayotokana na vitendo vya rushwa na ufisadi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana na kushikama katika mapambano dhidi ya utakatishaji wa fedha na ukwepaji wa kodi. Sheria haina budi kuchukua mkondo wake na wahusika wa vitendo vya rushwa na ufisadi wapewe adhabu inayostahili. Vitendo vya rushwa vinadhalilisha na kupekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu; amani na utulivu. Kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni wa ukweli, uwazi na uwajibikaji katika mali ya umma.

Rushwa na Ufisadi
05 June 2021, 16:11