Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anawaalika wadau katika tasnia ya mawasiliano kufanyia kazi changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 55 ya Mawasiliano Ulimwenguni. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anawaalika wadau katika tasnia ya mawasiliano kufanyia kazi changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 55 ya Mawasiliano Ulimwenguni. 

Siku ya 55 ya Upashanaji Habari: Tafakari ya Dr. Paolo Ruffini

Papa anawataka wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, kujikita katika mambo msingi katika: ukweli, kwa kujionea hali halisi badala ya kubaki katika fikra peke yake. Yote haya ni mambo yanayohitaji rasilimali muda na kwamba, mwandishi wa habari anapaswa kuangalia ukweli na kubaki katika uaminifu; kwa kusikiliza na kuelewa kile kinachoendelea kwa matumaini zaidi! Ukweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa na Mama Kanisa Jumapili, tarehe 16 Mei 2021 sanjari na Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni ulinogeshwa na kauli mbiu “Njoo uone” Yn. 1:46, sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane. Haya ni maneno ya Kristo Yesu alipokutana kwa mara ya kwanza na Mitume wake, kielelezo makini cha mawasiliano ya kibinadamu. Ili kutangaza na kushuhudia ukweli wa maisha unaounda historia kuna haja ya kujitosa kimasomaso na kwenda kutazama, kukaa pamoja na wadau mbalimbali, kuwasikiliza, kupokea maoni yao na hatimaye, kufungua macho ili kujionea hali halisi. Mawasiliano hayana budi kuwa wazi na ya kweli katika kurasa za magazeti, kwenye mitandao ya kijamii, kwenye luninga, wakati wa mahubiri na hata katika mawasiliano katika mambo ya kisiasa na kijamii. Njoo uone ni mchakato ambao imani ya Kikristo imeweza kutangazwa na kushuhudiwa! Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa waandishi wa habari “kuchakarika usiku na mchana ili kutafuta habari”, tukio lile la kwenda na kuona limekua ni mwanzo na chemchemi ya imani, changamoto na mwaliko kwa waandishi wa habari kuwa na ujasiri. Baba Mtakatifu anagusia fursa na mitego iliyoko kwenye wavuti na kwamba hakuna kitu mbadala cha kuona kama mwanadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 16 Mei 2021 limeadhimisha Juma la Mawasiliano ya Jamii Nchini Italia, hii ikiwa ni awamu yake ya kumi na saba. Maadhimisho haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii yamenogeshwa na Masista wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo, lililoanzishwa kunako mwaka 1915 na Mwenyeheri James Alberione, huko Alba nchini Italia na linatekeleza utume wake katika nchi 52 duniani kote! Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika maadhimisho haya amejikita zaidi na changamoto kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewataka wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii na kuanza kujikita katika mambo msingi katika maisha yaani: ukweli, kwa kujionea hali halisi badala ya kubaki katika fikra peke yake. Yote haya ni mambo yanayohitaji rasilimali muda na kwamba, mwandishi wa habari anapaswa kuangalia ukweli na kubaki katika uaminifu wa mambo; kwa kusikiliza na kuelewa kile kinachoendelea kwa matumaini zaidi. Sala iliyotungwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho haya inawahimiza wadau wa tasnia ya habari kutafuta na kuambata: ukweli, kuondokana na maamuzi mbele, kutumia vyema rasilimali muda ili kutafakari na hatimaye, kutoa kipaumbele kwa mambo msingi, kwa kukazia uaminifu.

Baba Mtakatifu anawataka wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kutoka na kuwaendea jirani, ili kuangalia mambo msingi katika maisha; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaelewa, kuwafariji na kuwasaidia, ili kutangaza ukweli wa mambo. Baada ya kutoka katika undani na ubinafsi, waandishi wa habari wanapaswa kuchakarika usiku na mchana ili kutafuta na kuambata ukweli, ili kusimulia na kuandika historia inayoacha chapa ya kweli katika maisha kwa sababu inakita ujumbe wake katika ukweli. Ni hatari kuishi kwenye ulimwengu wa kufikirika na wa sura na balagha. Kumbe hali halisi ni kubwa kuliko fikra peke yake. Kwa waandishi kujionea wenyewe, wataweza kufahamu ukweli wa mambo! Ili kuweza kufikia hatua hii, kuna haja ya kutumia vyema rasilimali muda, ili kuyaangalia mambo katika ukweli wake badala ya kufikia hitimisho la jumla peke yake na matokeo yake, “watu wanalishwa matango pori” kama ilivyo kuhusu chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwamba, ina madhara na baadhi ya watu wakaacha kuchanjwa!

Baba Mtakatifu anawaalika waandishi wa habari kutafuta, kuambata na kusimulia ukweli. Tasnia ya mawasiliano inawahitaji watu makini na wema, wanaoweza kufanya tafsiri sahihi ya matukio katika maisha. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema, Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu. Rej. Mt. 5:8. Waandishi wa habari wavutwe na uzuri wa ukweli na kuendelea kubaki wakiwa waaminifu. Wasikilize, watafute na kujitahidi kuufahamu ukweli wa mambo unaofumbatwa katika upendo, ili kujenga ujirani mwema. Huu ni mwaliko wa kuwa ni Wasamaria wema, ili kuganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali za maisha.

Dr. Ruffini

 

 

18 May 2021, 14:21