Tafuta

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri Tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Ni chombo madhubuti sana cha diplomasia makini kwa Jumuiya ya Kimataifa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri Tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Ni chombo madhubuti sana cha diplomasia makini kwa Jumuiya ya Kimataifa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele. 

Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti: Chombo Makini cha Diplomasia

Waraka wa "Fratelli tuti" ni chombo madhubuti cha diplomasia hai, inayopania kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, ili kunogesha mahusiano na mafungamano ya kibinadamu katika mchakato wa kuimarisha utawala bora wa Kimataifa. Huu ni utawala unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu; na ni sehemu ya utambulisho wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ulizinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 unakamilishana na Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu anapenda kuunganisha athari za uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kijamii; vita na kinzani; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi pamoja na baa la umaskini linalopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo la Waraka huu, ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaunda mfumo wa uchumi fungamani na masuala ya kijamii yanayokita misingi yake katika haki, heshima na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu anakaza kusema, alama mbalimbali zinaonesha wazi kwamba, kuna uhusiano na mwingiliano mkubwa kati ya udugu wa kibinadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama njia inayowaelekeza watu wa Mungu katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, haki na amani; tunu msingi ambazo ni sehemu ya Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium” tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Waraka unapembua pamoja na mambo mengine kuhusu: magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni, ameshiriki maadhimisho ya Waraka huu, tukio ambalo liliandaliwa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, kilichoko mjini Roma. Ni Waraka unaoweza kuchukuliwa kama chombo madhubuti cha diplomasia hai, inayopania kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, ili kunogesha mahusiano na mafungamano ya kibinadamu katika mchakato wa kuimarisha utawala bora wa Kimataifa. Huu ni utawala unaosimikwa katika utambuzi wa udugu wa kibinadamu. Udugu wa kibinadamu ni sehemu ya utambulisho wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Ni changamoto inayoisukuma Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kukuza na kudumisha: usawa, utu, heshima, uhuru na haki msingi za binadamu; daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yalipewa uzito unaostahili. Uhai, wito wa kila mtu, kazi na karama ya huduma vinapaswa kuimarishwa zaidi.

Udugu wa kibinadamu unapaswa kunafsishwa katika ujasiri na ukarimu, ili kutafuta suluhu ya changamoto mamboleo zinazoendelea kumwandama mwanadamu. Udugu ni chombo madhubuti kinachopaswa kuwatetea maskini na wanyonge. Diplomasia ya Vatican inakazia: Afya bora ili kulinda uhai wa binadamu tangu anapotungwa mimba hadi kifo cha kawaida kinapomsibu. Katika mwelekeo huu, chanjo dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19, lazima ithibitishwe kuwa salama na yenye ufanisi kwa idadi kubwa ya watu kabla ya kuidhinishwa na kuingizwa kwenye programu za chanjo sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni mwaliko wa kujikita katika upendo na mshikamano wa kidugu kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; kazi na ajira, haki ya kibinadamu kimataifa pamoja na udhibiti wa silaha duniani. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakaza kusema, kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu, watu wengi wana kiu ya: haki, amani, ustawi na maendeleo. Lakini kiu hii haiwezi kuzimwa kwa kutumia mtutu wa bunduki na silaha za maangamizi. Mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya: usalama, amani na utulivu kwa kuondokana na wasi wasi pamoja na hofu inayotawala akilini na nyoyoni mwa watu kiasi cha kushindwa kuaminiana, na hivyo, kudhohofisha mafungamano ya watu wa Mataifa pamoja na mchakato wa majadiliano.

Amani na utulivu wa Kimataifa vinaweza kujengeka katika msingi wa mshikamano na ushirikiano wa haki kwa ajili ya huduma kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilisha; na wanapaswa kuwajibika kama wamoja kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu. Mashindano ya utengenezaji wa silaha za maangamizi ni upotevu mkubwa wa rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kuchochea maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Umefika wakati muafaka wa kutumia rasilimali vitu na karama kwa binadamu ili kuondokana na utamaduni wa kifo na badala yake, rasilimali hii, itumike kwa ajili ya huduma inayoenzi Injili ya uhai. Kuna changamoto mamboleo zinazoendelea kuiandama Jumuiya ya Kimataifa, hizi zipewe kipaumbele cha pekee. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni chombo madhubuti katika diplomasia ya Jumuiya ya Kimataifa, na sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa ajili ya mafungamano ya kijamii, ustawi na mafao ya wengi.

Diplomasia

 

 

20 April 2021, 15:45