Ujumbe wa Siku ya XI ya Sarakasi Duniani: Mshikamano wa udugu na upendo katika kupambana na madhara yanayoendelea kusababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19: Mshikamano wa upendo. Ujumbe wa Siku ya XI ya Sarakasi Duniani: Mshikamano wa udugu na upendo katika kupambana na madhara yanayoendelea kusababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19: Mshikamano wa upendo. 

Ujumbe kwa Siku ya XI ya Sakarasi Duniani: Madhara ya UVIKO-19

Michezo ya Sarakasi ni chanzo cha fursa za ajira kwa binadamu na wanyama wanaotumika kunogesha michezo hii. Michezo hii imedumu kwa zaidi ya miaka 250 kwa sasa inakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha kutokana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wanamichezo hawa wanahitaji kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kuendelea na shughuli zao: Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu linaungana na Shirikisho la Michezo ya Sarakasi Kimataifa (Fédération Mondiale du Cirque, Monaco) chini ya udhamini wa Mfalme Stèphanie wa Monaco kuadhimisha Siku ya Kumi na Moja ya Sarakasi Duniani, Jumamosi tarehe 17 Aprili 2021. Wanamichezo wa Sarakasi ni wasanii wa uzuri. Ni katika muktadha huu, Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya XI ya Sarakasi Duniani, anapenda kuwapongeza viongozi wote waliojitosa kusaidia kugharimia maadhimisho haya. Michezo ya Sarakasi ni chanzo cha fursa za ajira kwa binadamu na wanyama wanaotumika kunogesha michezo hii. Michezo hii imedumu kwa zaidi ya miaka 250 kwa sasa inakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha kutokana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wanamichezo hawa wanahitaji kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kuendelea na shughuli zao.

Vatican kwa upande wake, itaendelea kusikiliza na kujibu mahitaji msingi kutoka kwa Makanisa mahalia hasa kutokana na athari za UVIKO-19: kimwili na kisaikolojia; watu wengi wamekata tamaa; Jumuiya ya Kimataifa imekosa dira na mwelekeo thabiti na kwamba, gonjwa hili limesababisha madonda makubwa katika maisha ya watu na itachukua muda mrefu kuweza kuyaganga, kuyatibu na kuyaponya magonjwa. Dawa madhubuti imeoneshwa na mshikamano wa Injili ya upendo kutoka kwa waamini, mashirika ya kiraia na watu wenye mapenzi mema. UVIKO-19 inawakumbusha watu wa Mungu kwamba, wote wako kwenye mashua moja ya mateso na mahangaiko, kumbe, ni watu wanaotegemeana na kukamilishana. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na matumaini, ili kuwaimarisha wale waliodhohofu na kujikatia tamaa. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anasema, watu wajenge utamaduni wa kusaidia jirani zao na kamwe wasiwageuzie kisogo. UVIKO-19 unaendelea kusababisha changamoto kwa kila mtu duniani. Kumbe, huu ni mwaliko kwa watu wote kuwajibika katika mchakato wa mageuzi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kujenga utamaduni wa mshikamano wa umoja na upendo, ili wote kwa pamoja waweze kugundua maana ya maisha, utu, heshima ya kila binadamu, changamoto inayowafanya kupendana kama ndugu wamoja. Watu washirikiane na kushikamana kwani wanasarakasi wanateseka lakini wanataka kuanza upya kutabasamu na kuwaonjesha wengine furaha katika maisha hasa wagonjwa na maskini. Huu ni mwaliko kwa wanamichezo wa sarakasi, watakapoanza shughuli zao, kuwa ni chemchemi ya furaha kwa watoto na wagonjwa.

Sarakasi
17 April 2021, 15:20