Kardinali Pietro Parolin, tarehe 25 Aprili 2021 amemweka wakfu Monsinyo Mark Gerard Miles kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Benin na Togo. Kardinali Pietro Parolin, tarehe 25 Aprili 2021 amemweka wakfu Monsinyo Mark Gerard Miles kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Benin na Togo. 

Askofu Awe Mchungaji Mwema: Mkarimu na Mlinzi Mwaminifu

Askofu mkuu Mark Gerard Miles ametakiwa kumtafakari na kumuiga Mtakatifu Yosefu Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Awe na moyo wazi; kiongozi mwenye moyo wa ukarimu na mwaminifu; awe ni mlinzi wa amana na utajiri wa Kanisa "Fidei Depositum". Awe na huruma na upendo, tayari kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ibada, unyofu wa moyo na mapendo makuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kilele cha Injili kama ilivyoandikwa na Marko ni pale ambapo Akida aliyesimama chini ya Msalaba akimwelekea Kristo Yesu alipoona akikata roho jinsi hii akasema “Hakika mtu huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu” Mk. 15:39. Hii ni sifa kuu ya Kristo Mchungaji mwema aliyeyamimina maisha yake kama sadaka ya wokovu kwa walimwengu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, iliyoadhimishwa Jumapili, tarehe 25 Aprili 2021, umenogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa: Ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudema hapo tarehe 8 Desemba 2021.

Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumapili ya Mchungaji Mwema, amemweka wakfu Monsinyo Mark Gerard Miles kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Benin na Togo. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la “Saint Mary Crowned” huko Gibraltar. Katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, mwaliko kwa waamini kumtafakari na kujitahidi kumwilisha sifa zake katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Kama Askofu mkuu, awe na moyo wazi, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu, huduma inayosimikwa katika umoja na upendo, kama mchungaji mwema, tayari kuwalinda waamini ambao ni dhaifu kwa imani. Awe ni kiongozi mwenye moyo wa ukarimu na uaminifu utakaomwezesha kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu, tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha “Amana ya Imani: “Fidei Depositum” inayohifadhiwa na Mama Kanisa, chachu ya utakatifu wa watu wa Mungu.

Karama ya huruma itamwezesha Askofu mkuu mpya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuadhimisha Sakramenti za Kanisa, daima Kristo Yesu mchungaji mwema, akiwa mbele yake kama mfano bora wa kuigwa, aliyewatafuta kondoo “waliotokomea gizani”, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa wote hawa anapaswa kuwa ni: Mchungaji mwema, Baba na Mwalimu wa kundi lake. Kardinali Pietro Parolin amemsihi, Askofu mkuu mpya Mark Gerard Miles, kuwa mnyenyekevu kwa karama na zawadi za Roho Mtakatifu; mwaminifu katika maisha ya sala, ili kuboresha maisha ya kiroho, tayari kuwatumikia watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu pamoja na kutambua kwamba, kuna wakati ataweza kudaiwa zaidi, kiasi cha kutosa maisha yake. Ni wajibu wake, kuwa karibu na Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Awe karibu na waamini ili aweze kuwaongoza kwenda kwa Baba wa mbinguni kama kauli mbiu yake ya Kiaskofu inavyosema, “Parare viam Domini” kama ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji aliyemwandalia Kristo Yesu njia.

Askofu mkuu Mark G. Miles awasaidie waamini kukimbilia kwenye chemchemi ya furaha ya kweli, matumaini na matunda ya maisha ya kiroho. Yote haya yanawezekana kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Awe ni Askofu mkuu mwenye kutafakari kwa makini Neno la Mungu, daraja ya kuwaunganisha watu na chombo cha upatanisho. Hizi ni silaha madhubuti katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kama Balozi wa Vatican nchini Benin na Togo, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Askofu mkuu Mark Gerard Miles awe ni chombo cha haki na amani, ili kwa njia ya Kristo Yesu, watu wengi waweze kuokolewa.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Mark Gerard Miles alizaliwa tarehe 13 Mei 1967 huko Gibralta, nchini Uingereza. Historia inaonesha kwamba, Askofu mkuu Mark Gerard Miles anakuwa ni Balozi na Askofu mkuu wa kwanza kutoka katika eneo hili la Gibralta. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 14 Septemba 1996 akapewa daraja Takatifu ya Upadre. Hii ilikuwa ni Sikukuu ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba, chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu! Ni ishara ya neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo.Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Baada ya Mwaka 1996 Askofu mkuu Mark Gerard Miles akaanza maandalizi ya kujiunga na Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa. Katika maisha na utume wake wa Kidiplomasia, alipangiwa huko Ucuador, Hungaria na Vatican katika Idara ya masuala ya jumla kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican.

Wakati wa hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippin na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2015, ndiye aliyekuwa anatafsiri hotuba za Baba Mtakatifu mubashara, kutoka katika lugha ya Kihispania kwenda katika lugha ya Kiingereza, kiasi cha kuwaacha wasikilizaji wengi wakiwa wameshika tama kutokana na umahiri wake! Tarehe 31 Agosti 2019 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwa Nchi za Amerika “Organization of American States, OAS”. Tarehe 5 Februari 2021, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Benin na kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Na hatimaye, tarehe 2 Machi 2021 akamwongezea tena eneo la utume, kwa kumteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Togo. Tarehe 25 Aprili 2021 akawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu katika Ibada iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Wakfu Askofu mkuu

 

26 April 2021, 15:05