Familia ya Mungu nchini Armenia, tarehe 24 Aprili 2021 imeadhimisha kumbukizi la miaka 106 ya Mauaji ya Kimbari nchini humo yaliyopelekea watu milioni 1.5 kupoteza maisha. Familia ya Mungu nchini Armenia, tarehe 24 Aprili 2021 imeadhimisha kumbukizi la miaka 106 ya Mauaji ya Kimbari nchini humo yaliyopelekea watu milioni 1.5 kupoteza maisha. 

Fumbo la Msalaba Katika Maisha ya Wakristo: Ushuhuda wa Upendo

Kardinali K. Koch katika mahubiri yake amejielekeza zaidi kuhusu: safari ya kwenda kwa Baba wa milele; wafiadini kama kielelezo cha upendo kwa Mungu na jirani; Uekumene wa damu sanjari na Fumbo la Msalaba katika maisha ya Wakristo. Lengo la Ibada hii ya Misa Takatifu lilikuwa ni kwa ajili ya kuombea amani duniani., sehemu ya mchakato wa kuganga na kuponya majeraha ya vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Imegota miaka 106 tangu yalipotokea mauaji ya kimbari 'Metz Yeghern' nchini Armenia na kusababisha zaidi ya watu milioni 1.5 kupoteza maisha kutokana na chuki za kidini. Ilikuwa ni tarehe 24 Aprili 1915, kufumba na kufumbua Armenia ikajikuta inageuka kuwa ni bwawa la damu ya watu wasiokuwa na hatia. Ni katika muktadha huu, wakristo wa Makanisa na madhehebu mbalimbali ya Kikristo, Jumapili tarehe 25 Aprili 2025 wameadhimisha Ibada ya Kiekumene, kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 106 tangu mauaji ya kimbari 'Metz Yeghern' kutokea nchini Armenia. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika Kanisa kuu la Mtakatifu Bartolomeo, Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema kwa mwelekeo huu, mashuhuda wa imani, tayari wamekwisha jenga umoja wa Kanisa kwa njia ya kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Wakristo wapya: “Sanguis martyrum semen Christianorum”. Kardinali Kurt Koch katika mahubiri yake amejielekeza zaidi kuhusu: safari ya kwenda kwa Baba wa milele; wafiadini kama kielelezo cha upendo kwa Mungu na jirani; Uekumene wa damu sanjari na Fumbo la Msalaba katika maisha ya Wakristo. Lengo la Ibada hii ya Misa Takatifu lilikuwa ni kwa ajili ya kuombea amani duniani. Huu ni mwaliko kwa waamini kujikita katika uponyaji, upatanisho, msamaha na ujenzi wa umoja na mafungamano ya udugu wa kibinadamu. Waamini wanakumbushwa kwamba, hapa duniani ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu, changamoto na mwaliko ni kujitahidi kujiandalia maisha ya uzima wa milele, watakapounganika na Mwenyezi Mungu.

Kristo Yesu aligeuza mateso na kifo cha Msalaba kuwa ni ufunuo wa chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Kumbe, mateso na kifo cha Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na ufuasi wa Kristo Yesu. Kwani ni kwa njia ya mateso na kifo, wafiadini wanashiriki pia Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu. Jambo la msingi kwa wafiadini ni kujitahidi kusamehe kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Ushuhuda wa imani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni ushindi dhidi ya utamaduni wa kifo, chuki na uhasama. Ni ushuhuda wa upendo kwa Mungu na jirani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa kutoka kwa Kristo mwenyewe. Tangu mwanzo wa Kanisa, kuna Wakristo ambao wameyamimina maisha yao kama ushuhuda wa imani. “Kifodini kinathaminiwa na Kanisa kuwa karama bora na uhakikisho mkuu wa upendo. Ingawa ni wachache wanaojaliwa neema hii ya kifodini, lakini wote wanapaswa wawe tayari kumkiri Kristo mbele ya watu, na kumfuata katika Njia ya Msalaba kati ya madhulumu ambayo hayakosekani kamwe katika Kanisa”. LG. 42.

Madhulumu, nyanyaso na mateso haya ni kwa ajili ya Wakristo wote na hasa katika Karne ya Ishirini na moja, kumetokea mauaji mengi ya kimbari kutokana na chuki za kidini. Kanisa limeendelea kuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa imani. Wakristo ni kati ya waamini wanaoteseka na kunyanyasika kwa wingi sehemu mbalimbali za dunia. Ndiyo maana Makanisa na madhehebu ya Kikristo yanao mashuhuda wao wa imani. Huu ndio uekumene wa damu, ili wote wawe wamoja yaani “Ut Unum Sint” kama alivyowahi kukazia Mtakatifu Yohane Paulo II. Uekumene wa damu ni kielelezo cha umoja na mashikamano wa Kanisa. Damu ya mashuhuda wa imani kwa siku za mbeleni, itakuwa ni alama ya umoja wa Kanisa. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete: kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kifodini ni ushuhuda wa hali ya juu kabisa wa upendo kwa Kristo Yesu, Kanisa na jirani. Huu ndio ushuhuda uliotolewa pia na Wakristo kutoka Armenia. Waamini hao walibaki kuwa waaminifu kwa imani ya Mitume waliyoipokea kwa njia ya Kristo Yesu. Neno la Mashuhuda wa imani. Neno “Martys” kwa lugha ya Kigiriki maana yake ni shuhuda wa imani ambaye amejisadaka bila ya kujibakiza si tu kwa maneno, bali kwa njia ya kifo chake, mfano bora wa kuigwa katika imani. Na wakati huo huo, kwa mara ya kwanza katika historia, Rais Joe Biden wa Marekani, ametambua rasmi maauaji ya kimbari yaliyofanywa na dola ya Ottoman. Nchi nyingine ambazo zimetambua mauaji haya kuwa ni ya kimbari ni pamoja na: Uruguay, Ufaransa, Ujerumani, Canada na Urusi. Uturuki inapinga kuwa mauaji hayo ya Waarmenia kuwa ni ya kimbari, lakini, ukweli wa kihistoria utabaki jinsi ulivyo!

Mauaji ya Kimbari

 

 

27 April 2021, 15:34