Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona limepekenyua na kufumua magonjwa na madonda ya maisha ya mwanadamu katika sekta mbalimbali za maisha: uchoyo na ubinafsi umeonekana wazi zaidi. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona limepekenyua na kufumua magonjwa na madonda ya maisha ya mwanadamu katika sekta mbalimbali za maisha: uchoyo na ubinafsi umeonekana wazi zaidi. 

UVIKO-19 Imefumua Magonjwa na Udhaifu wa Watu: Ubinafsi Zaidi!

Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limepekenyua na kufumua magonjwa na madonda ya maisha ya mwanadamu katika sekta mbalimbali za maisha: lakini uchoyo na ubinafsi vimeanikwa wazi zaidi. Kuna mamilioni ya watu wanaoteseka kutokana na ujinga na maradhi. Mapambano dhidi ya janga hili yameendelea kuwa magumu kutokana na umaskini na hali ngumu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kipindi cha mapambano dhidi ya maambukizi makubwa yanayosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kimejenga na kuimarisha moyo wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa; hali ambayo pia imegusa familia kubwa ya binadamu. Watu wamegundua kwamba, wanategemeana na kukamilishana na wala hakuna mtu anayeweza kujimwambafai kwamba, anajitegemea kwa kila jambo. Kwa waamini umoja na mshikamano ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga kila wakati. Uchu wa mali, fedha na madaraka pamoja na tabia ya baadhi ya watu kutaka kujimwambafai ni kati ya mambo ambayo yanapelekea: kinzani, mipasuko na mashindano ya kibiashara, kiuchumi na hata kivita. Lakini, ikumbukwe kwamba, mwanadamu anahitaji maendeleo fungamani yanayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; huku amani, ikipewa kipaumbele cha kwanza kwani hili ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Huduma ya upendo na mshikamano; sadaka na majitoleo kwa jirani ni kati ya tunu msingi ambazo watu wa Mungu katika ngazi mbali mbali wanapaswa kuziendeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, katika mwelekeo huu, anakaza kusema janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limepekenyua na kufumua magonjwa na madonda ya maisha ya mwanadamu katika sekta mbalimbali za maisha: Uchoyo na ubinafsi. Kuna watu ambao wamejaliwa kupata elimu na huduma bora za afya, wakati kuna mamilioni ya watu wanaoteseka kutokana na ujinga na maradhi. Kuna baadhi ya watu wanatibiwa kwenye hospitali maarufu wakati ambapo wagonjwa hawana fursa ya kupata dawa muafaka. Mapambano dhidi ya janga hili yameendelea kuwa magumu kiasi cha watu kushindwa kupata vitakasa mikono! Ikiwa kama maji safi na salama ni shida kupatikana, sembuse majitiririka ya kupambana na UVIKO-19? Ni vigumu sana kuepukana na misongamano ya watu kutokana na ukosefu wa usafiri na uhaba wa makazi ya watu. Kumbe, unaweza kukuta nyumba moja ina wapangaji zaidi ya watatu. Watu wanashauriwa kuvaa barakoa, lakini ni watu wangapi wanaozingatia masharti ya uvaaji wa barakoa hizi?

Nchi tajiri zimewekeza sana katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa chanjo na ushauri wa kuvaa barakoa. Mapambano haya yanaonekana zaidi ni ya kiuchumi kwa kuwekeza zaidi katika rasilimali fedha. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anakaza kusema, nchi nyingi zimeathirika kiuchumi, kijamii na kisiasa, kiasi kwamba, hazina uwezo mkubwa wa kuhudumia gharama na changamoto zinazotokana na madhara ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Uchambuzi huu unaozingatia ukweli na uwazi, umetolewa na Kardinali Tagle katika mkutano ulioandaliwa na Wamisionari Wafranciskani kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii pamoja na mitandao ya kijamii. Katika ulimwengu mamboleo, UVIKO-19 imeweka hadharani madonda yanayowaandama wanadamu yanayotokana na maamuzi mabaya yasiyozingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa sekta ya afya. Kumbe, kuna madonda ya watu wenyewe kujitakia kwa kushindwa kutekeleza yale mambo ya msingi ili kuepukana na maambukizi makubwa ya UVIKO-19.

Lakini pia, kuna madonda makubwa yanayotokana na ukosefu wa usawa katika masuala ya uchumi, huduma na miundombinu ya huduma za kijamii. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba Mwenyezi Mungu yuko kati pamoja na waja wake wanaoteseka. Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu, kwa sababu hakuna mtu anayeweza kutembea peke yake, kuteseka pekepeke au kuitupa mkono dunia, akiwa peke yake. Dawa ya magonjwa haya ni Kristo Yesu ambaye kwa upendo na huruma yake, amewawezesha madaktari, wafanyakazi katika sekta ya afya, watu wa kujitolea, wakleri na watawa kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo na mshikamano wa kidugu na wale wote walioguswa na kupapaswa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Mtu anayependa upeo, yuko tayari kusadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, anasema, Baba Mtakatifu Francisko mwezi Machi 2020 aliunda  Kikosi kazi kwa ajili ya kusaidia nchi maskini duniani kupambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kikosi hiki kinajumuisha Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Makanisa mahalia yanayohamasishwa kuchangia kwa hali na mali katika mapambano dhidi ya UVIKO-19. Caritas imepewa dhamana ya kuelimisha na kutoa mafunzo kwa Jumuiya mahalia, ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 badala ya kutegemea Serikali za nchi zao, ambazo pengine hazina uwezo mkubwa wa kupambana na janga hili. Hii pia ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu wenye mwelekeo mpana zaidi na wala si katika masuala ya kiuchumi peke yake. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, washirikishane changamoto na matatizo yanayoibuliwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, akizungumzia kuhusu Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China, ulitiwa saini tarehe 22 Septemba 2018 na kurudiwa tena, amekazia kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia. Lengo la Vatican ni kuwapata waamini nchini China wachungaji bora watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko akashuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi. Mkazo ni kuhusu shughuli za kichungaji na kitume, ili kuwawezesha waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mchakato huu pamoja na mambo mengine unapania kukoleza: imani na matumaini; umoja na mshikamano wa kidugu. Uteuzi wa Maaskofu kwa ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya China ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini China na kwamba, huo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle ana matumaini makubwa katika ushirikiano huu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mkataba una mapungufu yake, lakini hii ni fursa ya kuweza kufanya kazi kwa pamoja.

Kardinali Tagle UVIKO 19
11 April 2021, 15:18