Tafuta

Siku ya Wanawake Duniani 2021: Jumuiya ya Wanawake Tanzania, WAWATA, inaanza mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, kilele ni Septemba 2022. Siku ya Wanawake Duniani 2021: Jumuiya ya Wanawake Tanzania, WAWATA, inaanza mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, kilele ni Septemba 2022. 

Siku ya Wanawake Duniani 2021: WAWATA Miaka 50 Sept. 2022

Kumbukizi la Miaka 110 tangu Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC lilipoanzishwa sanjari na mchakato wa maandalizi ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA. Kilele ni hapo Septemba 2022. Wanawake pia wanapenda kushirikisha mawazo na mang'amuzi yao kuhusu Waraka wa "Fratelli tutti".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2021 inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi limefanya mkutano kwa njia ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Mwaka huu maadhimisho haya yamenogeshwa na kauli mbiu “Wanawake wanasoma Waraka wa Kitume “Fratelli tutti”. Jumatano tarehe 3 Machi 2021 limefanya mkutano wa kiekumene, kidini na kidiplomasia mjini Roma. Mkutano umeratibiwa na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na wawakilishi wa nchi mbali mbali mjini Vatican. Mkutano huu umehudhuriwa na wanawake kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, kwa lengo la kushirikisha maoni na mang’amuzi yao juu ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020.

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti Taifa wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, ameshiriki maadhimisho haya kama sehemu ya kumbukizi la miaka 110 tangu Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC lilipoanzishwa sanjari na mchakato wa maandalizi ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania. Kilele chake ni hapo Septemba 2022. Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC linaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2021 huku kukiwa na changamoto kubwa ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unagusia: Magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu katika Waraka huu anakazia kuhusu: maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo kwamba, haya ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.  Baba Mtakatifu anapembua: kuhusu siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini anasema ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu “Udugu na Urafiki wa Kijamii” unaweza kupokelewa na kunafsishwa na watu wote kwa sababu wote wanashirikishwa katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Bado kuna vikwazo na changamoto nyingi lakini Waraka huu ni hatua kubwa katika kusimama kidete kulinda, kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika safari hii, wanawake wanaweza kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kuendelea kujenga utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Malezi na majiundo ya udugu wa kibinadamu ni muhimu sana, ikiwa kama wanawake watashirikishwa katika hatua zote. Ikumbukwe kwamba, wanawake ni wajenzi wakuu wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika Injili ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Wanawake ni mashuhuda na watetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Injili ya upendo ni kiungo muhimu katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu! Kwa upande wake, Kardinali Gianfranco Ravasi Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni amelishukuru Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, wanadiplomasia wanawake pamoja na wanawake kutoka katika dini mbalimbali duniani ambao wameshiriki katika mkutano huu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unapaswa kuangaliwa pia kwa jicho la wanawake, hasa kwa kujikita katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja, kumbe wanapaswa kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana licha ya tofauti zao msingi. Shuhuda za wanawake mbalimbali iwe ni fursa kwa watu wa Mungu kusoma na hatimaye, kumwilisha ujumbe wa udugu na urafiki wa kijamii katika medani mbalimbali za maisha! Wanawake walioshiriki katika mkutano huu, pamoja na mambo mengine wamekazia umuhimu wa kuelewa sarufi ya majadiliano iliyopelekea Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo tarehe 21 Desemba 2020 kupitisha Azimio Kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu kila mwaka ifikapo tarehe 4 Februari. Umoja wa Mataifa unatambua na kuthamini mchango wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbalimbali duniani, kama sehemu ya mchakato wa kufahamiana sanjari na kutambua tunu msingi za maisha ya kiroho wanazoweza kushirikisha kwa familia nzima ya binadamu. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na waamini, kila kukicha!

Lengo ni kudumisha majadililiano ya kidini na kitamaduni; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Kimataifa, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano wa kidugu na upatanisho wa Kitaifa na Kimataifa. Mambo makuu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Udugu wa kibinadamu, Mshikamano na Amani Duniani! Mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu unapania kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kutokana na uchoyo na ubinafsi. Umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unapaswa kupambwa na picha ya udugu wa kibinadamu. Waraka huu ni dira na mwongozo wa maisha jamii ya binadamu na daraja la kukutana na kujadiliana la Umoja wa Mataifa. Ni Waraka unaohimiza tunu bora za maisha ya kifamilia, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na mwaliko wa kupendana hata katika tofauti zao msingi

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti Taifa wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania anasema, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. WAWATA inaanza mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na kilele chake ni Mwezi Septemba 2022, matendo makuu ya Mungu. Katika kipindi hiki WAWATA imepata mafanikio makubwa, imekumbana na changamoto nyingi na imeonesha pia udhaifu katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ni fursa ya kupyaisha imani, matumaini na mapendo kwa kuwekeza zaidi katika maisha na utume wa WAWATA. Kimsingi, huu ni wakati wa kujikita katika sala, ujenzi wa udugu wa kibinadamu na umisionari katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, mambo msingi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya!

Wanawake Wakatoliki wanapaswa kumwilisha Injili ya upendo, huduma na matumaini katika matendo ya kiroho na kimwili. Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, huku bado kukiwa na maambukizi makubwa ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna watu wengi wamefariki dunia katika hali ya mateso na mahangaiko makubwa. Kuna watu wamepoteza fursa na ajira za kazi. Kumekuwepo na uvunjifu mkubwa wa: amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza watu wa Mungu kupita janga hili wakiwa wameimarika zaidi. Wanawake Wakatoliki licha ya tofauti zao msingi, lakini ni wabebaji wa maji ya uzima kwenye dunia yenye kiu ya haki na amani.

Mama Evaline Malisa Ntenga anasema, waamini watambue kwamba, Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima! Amewafunulia na kuwashirikisha huruma, upendo na msamaha wake usiokuwa na kifani na kwamba, wote ni ndugu na wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanawake wanakumbushwa wajibu na dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa na hata katika jamii katika ujumla wake. Bikira Maria, Mama wa mateso, awe mfano bora wa kuigwa, na waendelee kumjifunza Yesu Kristo kutoka katika shule ya Bikira Maria. WAWATA wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo kwa kuwasaidia wahitaji zaidi hata pale ambapo wao wenyewe hawajajitosheleza kana kwamba, wanayo ziada kama kauli hii inavyonogeshwa na Papa Pio wa XII. Lengo ni kuwathamini wengine na kujiweka karibu nao katika mahitaji yao msingi. Hii ndiyo Injili inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, chombo madhubuti katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Mama Evaline Malisa Ntenga anakaza kusema, waamini watambue kwamba, wameitwa na kubatizwa na hivyo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kuanzia katika familia, jirani na walimwengu katika ujumla wao. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawatambua wanawake kuwa ni vyombo na mashuhuda wa sala inayomwilishwa katika medani mbali mbali za maisha. Wao ni mashuhuda na wajenzi wa udugu wa kibinadamu kama anavyowakumbusha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Ili kuweza kuinjilisha na kutakatifuza malimwengu kuna haja ya kuwa na moyo mmoja na roho moja kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na changamoto mbalimbali za maisha. Umoja na mshikamano wa kimisionari ujikite katika sheria, kanuni na taratibu za Kanisa; kwa kunogeshwa na utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” n. 31.  

Mama Evaline Malisa Ntenga anaendelea kufafanua kwamba, WAWATA inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika”. Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla, pia wanawake wanakuwa na maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Yesu Kristo.

Mama Evaline Malisa Ntenga anahitimisha kwa kupembua Malengo Makuu ya WAWATA ilipokuwa inaanzishwa. WAWATA ilipoanzishwa kunako mwaka 1972, ilijiwekea malengo ili kupata mwelekeo utakaowafikisha mahali ambapo wanaweza kufanya tathmini ya Utume wao katika maisha na utume wa Kanisa na katika mchakato wa ukombozi mzima wa mwanamke mintarafu suala la maisha ya kiroho, mapambano dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi. Malengo haya yalijikita zaidi katika mchakato wa kumjenga mwanamke katika imani thabiti ya Kikristo, ili aweze kuishi maisha matakatifu na hatimaye, ayatakatifuze malimwengu kwa ushuhuda wa maisha yake kama kielelezo cha imani tendaji. WAWATA pamoja na mambo mengine, inapania kumjengea mwanamke uwezo wa kujikomboa yeye na familia yake, ili aweze kuwakomboa watu wengine wenye shida, yatima na wasiojiweza. WAWATA inataka kumwendeleza mwanamke kielimu na kiujuzi ili aondokane na giza la kiroho, ujinga wa akili na aendeleze wengine sanjari na kumwezesha mwanamke katika masuala ya kiuchumi ili kuitegemeza familia, Kanisa na hatimaye, kuwategemeza wengine.

Siku Ya Wanawake 2021

 

 

04 March 2021, 16:31