Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu limemteua Padre Joseph Msafiri Mahela, ALCP/OSS kuwa Gambera mpya wa Seminari kuu ya Mama wa Malaika, Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu limemteua Padre Joseph Msafiri Mahela, ALCP/OSS kuwa Gambera mpya wa Seminari kuu ya Mama wa Malaika, Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. 

Padre Joseph Msafiri Mahela, Gambera Kibosho Seminari!

Mheshimiwa Padre Joseph Msafiri Mahela wa ALCP/OSS alizaliwa tarehe 4 Aprili 1973. Ilipofika tarehe 27 Oktoba 2006 alipokelewa rasmi Shirikani. Tarehe 28 Oktoba 2006 akapewa Daraja ya Ushemasi na tarehe 22 Julai 2007 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kati ya 2008 hadi mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Katibu wa Jimbo Katoliki la Kahama. Mwaka 2012 alijipatia PHD, Roma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwa mamlaka aliyopewa na Mama Kanisa, amemteua Mheshimiwa Padre Joseph Msafiri Mahela wa ALCP “APOSTOLIC LIFE COMMUNITY OF PRIESTS” Yaani Jumuiya ya Maisha ya Kipadre. OSS: “OPUS SPIRITUS SANCTI” yaani Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu kuwa Gambera mpya wa Seminari kuu ya Mama wa Malaika, Kibosho Jimbo Katoliki la Moshi nchini Tanzania. Katika barua ya uteuzi, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, amemtaka Gambera mpya kuhakikisha kwamba, anazingatia kanuni, taratibu na sheria kama zilivyobainishwa kwenye Sheria za Kanisa pamoja na Mwongozo wa Malezi ya Kipadre.

“Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” ni Mwongozo unaobainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia! Sura ya Pili ya Mwongozo huu inapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre: Yaani wanapaswa kuunganika na Kristo ili kuwaongoza, kuwachunga na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu.

Itakumbukwa kwamba, Mheshimiwa Padre Joseph Msafiri Mahela wa ALCP/OSS alizaliwa tarehe 4 Aprili 1973, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, tarehe 27 Oktoba 2006 alipokelewa rasmi Shirikani. Tarehe 28 Oktoba 2006 akapewa Daraja ya Ushemasi na hatimaye, tarehe 22 Julai 2007 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Katibu wa Jimbo Katoliki la Kahama. Kuanzia mwaka 2012 alitumwa na Jimbo Katoliki la Kahama kujiendeleza kwa masomo ya juu katika Falsafa, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma na hatimaye kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Falsafa. Na tangu mwezi Desemba 2018 amekuwa ni Jaalimu na Mlezi wa Majandokasisi, Seminari kuu ya Mama wa Malaika, Kibosho Jimbo Katoliki la Moshi nchini Tanzania.

Seminari kuu ya Kibosho
29 March 2021, 15:45