Maadhimisho ya Mwaka wa Upendo Ndani ya Familia 19 Machi 2021 hadi 26 Juni 2022. Ni wakati muafaka wa kupyaisha sera na mikakati ya utume wa familia, kwa kusoma alama za nyakati. Maadhimisho ya Mwaka wa Upendo Ndani ya Familia 19 Machi 2021 hadi 26 Juni 2022. Ni wakati muafaka wa kupyaisha sera na mikakati ya utume wa familia, kwa kusoma alama za nyakati. 

Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: Mambo Muhimu!

Kardinali Kevin Joseph Farrell katika hotuba yake elekezi anakazia zaidi: dhamana na utume wa Mtakatifu Yosefu katika ulinzi wa Familia Takatifu; Umuhimu wa kupyaisha sera na mikakati ya utume wa familia sanjari na mchango wa viongozi wa Kanisa wa kutoa kipaumbele cha pekee katika Injili ya familia kwa kukazia: ukuu, utakatifu na udumifu katika maisha ya ndoa na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2021, Mama Kanisa anazindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.  Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, akiwasilisha maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia anasema kwamba, furaha inayopata chimbuko lake ndani ya familia ni furaha ya Kanisa pia na kwamba, tamko la Kikristo kuhusu familia ni Habari Njema kweli! Rej. AL 1. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” unakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Itakumbukwa kwamba, Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa hapo tarehe 8 Desemba 2021.

Baba Mtakatifu Francisko aliutangaza mwaka huu katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu”.Kardinali Kevin Joseph Farrell katika hotuba yake elekezi anakazia zaidi: dhamana na utume wa Mtakatifu Yosefu katika ulinzi wa Familia Takatifu; Umuhimu wa kupyaisha sera na mikakati ya utume wa familia sanjari na mchango wa viongozi wa Kanisa. Mtakatifu Yosefu ni wakili mwaminifu na mwenye hekima aliyepewa dhamana na wajibu wa kuilinda Familia Takatifu ya Yerusalemu. Katika sura ya Mtakatifu Yosefu, wana ndoa wote wanapaswa kujisikia kuwa wanapendwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, wamekabidhiwa dhamana ya kuendeleza kazi ya uumbaji pamoja na kutunza familia zao. Katika kipindi cha janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, familia nyingi duniani zimeathirika sana. Lakini zimedhihirisha kwamba, ni ngome ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu. Hapa ni mahali ambapo watu wanaendelea kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kweli. Familia ni chimbuko la upendo unaokuwa na kukomaa taratibu.

Miaka 5 imegota tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Kumbe, maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni muda muafaka wa kuanza kuvuna matunda yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano katika medani mbalimbali za maisha: kikanisa na kijamii. Ni nafasi ya kutafakari changamoto, fursa na matatizo yaliyopo na kuendelea kuzifanyia kazi. Changamoto ni kuubali na kuupokea Wosia ambao umesheheni maneno ya ujasiri, chachu ya mabadiliko pamoja na mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na watu wa Mungu. Familia zinahitaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, zitakazowawezesha wanandoa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia katika ujumla wake. Familia inapaswa kusimikwa katika upendo wenye huruma, kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, inayotangaza na kushuhudia uwepo mwanana wa Mwana wa Mungu. Katika shida na magumu, familia zisaidiwe kwa hali na mali, ili kuweza kupita vipindi hivi vigumu kwa kusindikizwa na upendo wenye huruma. Familia zinazoogelea kwenye shida na ugumu wa maisha zisikilizwe na zisaidiwe.

Mikakati mbalimbali ya shughuli za kichungaji iwasaidie wanandoa kupyaisha upendo wao kila kukicha. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kushirikishana sera, mikakati na shughuli za kichungaji. Lengo ni kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika maisha ya wanandoa. Umefika wakati wa kubadili fikra, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa familia kama kiini cha shughuli za kichuhngaji katika ngazi mbalimbali za maisha ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia ziwe ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kwa kuendelea kuwa ni Katekesi hai. Maisha yao yawe ni ujumbe wa matumaini hasa miongoni mwa vijana, ili hata wao waweze kutekeleza ndoto katika maisha yao. Huu ni muda muafaka wa kuwaunda na kuwafunda wadau wa sera na mikakati ya utume wa familia. Mkakati huu uanzwe kutekelezwa tangu mwanzo kabisa Mseminari anapoingia seminari kuu. Waoneshe neema inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa, ili waweze kujizatiti, tayari kupambana na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Viongozi wa Kanisa wawe mstari wa mbele kuupokea na kuumwilisha Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” sanjari na kujifunza kutoka na kujisadaka kwa ajili ya familia. Waamini waendelee kumjifunza Mtakatifu Yosefu, kwa kujikita katika ukarimu, utii, nguvu na kuthamini kazi na ajira. Kanisa liendelee kuwa ni Mama na Mwalimu kwa familia; kwa kusikiliza familia kwa makini pamoja na kuendelea kujiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu.

Kwa upande wake Mama Gabriella Gambino, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, anakazia kuhusu umuhimu wa matayarisho kwa wanandoa watarajiwa, ili waweze kutambua kwa dhati kabisa maana, umuhimu na changamoto wanazoweza kukumbana nazo katika hija ya maisha yao katika ndoa na familia. Wafundwe tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa; wapewe miongozo ya kisaikolojia. Wawaoneshe mahali ambapo wanaweza kupata msaada watakapokabiliwa na changamoto za maisha. Wakumbushwe umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, tayari kupokea na kuambata msamaha wa Mungu katika maisha yao. Familia ni kitovu cha elimu ya uraia mwema. Maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Mikakati ya maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji iliyofafanuliwa katika Wosia wa “Amoris laetitia” ipewe msukumo wa pekee kabisa, bila kusahau malezi makini ya watoto ndani ya familia. Yote haya yanahitaji ubunifu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Ikumbukwe kwamba, maisha ya ndoa ni wito! Kumbe, kuna haja pia ya kuwa na katekesi endelevu kwa vijana waliopokea Sakramenti za Kanisa, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni sehemu ya mchakato wa kulipyaisha Kanisa kwa kujielekeza zaidi katika uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushirikishwaji wa watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya unafsishaji ari na wito wa kimisionari, vinginevyo Kanisa litakuwa linajitazama na kujitafuta lenyewe! Utume wa familia upewe kipaumbele cha pekee katika maisha ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Jumapili tarehe 25 Julai 2021 itaadhimishwa Siku ya Wazee Duniani inayokaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Siku ya Wazee Duniani itakuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni hapo Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Mama Gabriella Gambino, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, Ndoa ni wito, waamini wote wanahimizwa kuupalilia wito huu ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Kwa upande wao wanandoa Valentina na Leonardo Nepi, kutoka Italia wanamshukuru Mungu wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” kwa ari, mwamko mpya na matumaini, licha ya matatizo na changamoto zinazoendelea kuibuka katika maisha ya ndoa na familia kwa sasa ni changamoto ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wanandoa wanakumbushwa kwamba, upendo wenye huruma ndani ya familia unasimikwa katika fadhila ya unyenyekevu inayoongozwa na maneno makuu matatu: tafadhali, asante na samahani. Mwaka huu usaidie mchakato wa kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya upendo ndani na nje ya familia. Ni wakati wa kushirikiana na kushikamana na jirani wakati wa raha na shida. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Vyama vya kitume na ushiriki mkamilifu katika maisha ya parokia na jamii katika ujumla wake ni muhimu sana katika kukuza furaha ya upendo ndani ya familia. Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ndoa Takatifu zinawahamasisha waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili, Huruma na Upendo wa Mungu kwa watu wote. Ni katika muktadha huu, familia zinaweza kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, tayari kutangaza na kushuhudia: Ukuu, uzuri na utakatifu wa Injili ya familia!

Mwaka wa Familia

 

 

 

18 March 2021, 15:53