Tafuta

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko: Tahariri ya Dr. Andrea Tornielli Mhariri mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano: Madhara ya Vita na Hamu ya Kanisa katika mchakato wa ujenzi wa amani nchini Iraq. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko: Tahariri ya Dr. Andrea Tornielli Mhariri mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano: Madhara ya Vita na Hamu ya Kanisa katika mchakato wa ujenzi wa amani nchini Iraq.  Tahariri

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Tahariri: Vita Iraq

Papa Francisko anasema, kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Vita kamwe si suluhu ya shida, changamoto na matatizo yanayoikabili Jumuiya ya Kimataifa. Haya ni maneno ya kinabii, lakini daima duniani kutakuwepo na “viongozi wababe” wanaopenda kutumia mtutu wa bunduki, lakini “dhana ya vita ya haki na halali” kwa sasa imepitwa na wakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1999 alitangaza nia ya kutembelea Iraq kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, ili kutembelea na kujionea maeneo muhimu ya historia ya wokovu! Nia hii njema ikagomba mwamba na kushindikana. Ni hija iliyopania kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene kwa kuchota utajiri wa wito wa Ibrahimu, Baba wa imani. Wachunguzi wa mambo wakasema, kama Mtakatifu Yohane Paulo II angefanya hija ya kitume nchini Iraq, ingeonekana kuwa kama sehemu ya mpango mkakati wa kuimarisha utawala wa Rais Saddam Hussein aliyekuwepo madarakani kwa wakati ule baada ya Vita ya Ghuba ya Uajemi. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa amepania kweli kweli kwenda Iraq, lakini ikashindikana kabisa hata kama hija hii ilikuwa ni ya maisha ya kiroho. Itakumbukwa kwamba, tangu mwaka 1999 Iraq ilikuwa inakabiliwa na hali ngumu sana ya kisiasa baada ya vita na Iran kati ya mwaka 1980 hadi mwaka 1988. Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa imeiwekea Iraq vikwazo vya kiuchumi baada ya kuivamia Kuwait.

Wakati huo, idadi ya Wakristo ilikuwa ni kubwa sana, ikilinganishwa na wakati huu. Kushindikana kwa hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Iraq, likabaki kuwa ni donda ndugu. Mtakatifu Yohane Paulo II akasimama kidete kulaani mashambulizi ya kivita dhidi ya Iraq pamoja na mapinduzi yaliyomng’oa Rais Saddam Hussein kutoka madarakani kunako mwaka 2003. Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu, Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Iraq anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwakumbusha wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, vita si suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Majadiliano katika ukweli na uwazi yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si mtutu wa bunduki. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa anatambua fika majanga ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia! Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo VI hata Mtakatifu Yohane Paulo II alilaani sana vitendo hivi na kusema, “Mai Piu la Guerra” yaani “Kusiwepo tena na vita”.

Kwa bahati mbaya, sauti hii, haikusikilizwa kamwe. Kunako mwaka 2014 Iraq ikatumbukia tena katika mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa Dola ya Kiislam “Islamic State, IS”. Watu wakaathirika sana kutokana na ubaguzi wa kidini na kikabila. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Vita kamwe si suluhu ya shida, changamoto na matatizo yanayoikabili Jumuiya ya Kimataifa. Haya ni maneno ya kinabii, lakini daima duniani kutakuwepo na “viongozi wababe” wanaopenda kutumia mtutu wa bunduki “kuwashikisha wengine adabu.”  Baba Mtakatifu anasema “dhana ya vita ya haki na halali” kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo!

Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa siasa na utu na inabaki kuwa ni aibu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na umati mkubwa wa Wakristo waliokimbia kutoka nchini Iraq ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Iraq ni eneo ambalo limeinjilishwa na Mitume wa Yesu na kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq inapania kuwapatia tena faraja ya maisha ya kiroho. Nia ya Baba Mtakatifu ni kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu wanaoteseka, kusaidia mchakato wa upatanisho, na ujenzi mpya wa Iraq utakaokita mizizi yake katika amani ya kudumu.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatambua fika changamoto zilizoko mbele yake katika hija hii ya kitume yaani: Usalama, janga la maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na hali tete nchini Iraq, lakini ameamua kwenda kuwafariji watu wa Mungu nchini Iraq. Anakwenda kutembelea kwenye nchi ya Mzee Ibrahimu, Baba wa imani. Ni fursa ya kukutana na kusali na waamini wa dini mbalimbali nchini Iraq, lakini zaidi na waamini wa dini ya Kiislam. Lengo ni kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, ujumbe wa matumaini mapya Ukanda wa Mashariki ya Kati na dunia katika ujumla wake.

Tahariri Iraq

 

 

02 March 2021, 14:53