Ratiba elekezi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko inaonesha utashi wake wa kutaka kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu nchini Iraq ili aweze kuwa ni chombo cha amani, matumaini na faraja. Ratiba elekezi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko inaonesha utashi wake wa kutaka kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu nchini Iraq ili aweze kuwa ni chombo cha amani, matumaini na faraja. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Ratiba Elekezi!

Papa Francisko akiwa mjini Baghdad atazungumza na wakleri, watawa na majandokasisi. Kilele cha hija hii ya kitume ni Jumamosi tarehe 6 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko atakapokutana na viongozi wa dini mbalimbali kwenye eneo la Uru ya Wakaldayo eneo maarufu ambalo Mwenyezi Mungu alikutana na kufanya ahadi na Ibrahimu, Baba wa imani. Papa ni hujaji wa matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021, anafanya hija ya kitume nchini Iraq, inayonogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija za kitume ni muhimu sana katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni nyenzo ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na Serikali mbalimbali duniani. Ni fursa ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu akiwa nchini Iraq atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa asasi zisizo za kiserikali. Akiwa mjini Baghdad atazungumza na wakleri, watawa na majandokasisi. Kilele cha hija hii ya kitume ni Jumamosi tarehe 6 Machi 2021, Baba Mtakatifu atakapokutana na viongozi wa dini mbalimbali kwenye eneo la Uru ya Wakaldayo eneo maarufu ambalo Mwenyezi Mungu alikutana na kufanya ahadi na Ibrahimu, Baba wa imani.

Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu mjini Baghdad. Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 7 Machi 2021 akiwa mjini Mosul atasali ili kuwaombea wahanga wa vita iliyoanza tarehe 20 Machi 2003. Marekani chini ya utawala wa Rais George W. Bush na Tony Blair, Waziri mkuu wa Uingereza walikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Iraq. Kulikuwa tuhuma kwamba, Iraq ilikuwa inamili silaha za maangamizi. Sababu ya pili ilikuwa ni kukomesha utawala wa Rais Saddam Husein kwa sababu alituhumiwa pia kujihusisha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi sehemu mbalimbali za dunia. Hatima ya yote haya, ilikuwa ni kuwarejeshea wananchi wa Iraq uhuru wao. Kumbe, hii itakuwa ni fursa ya kusali na kuwaombea wale wote walioathirika na vita ya Iraq tangu mwaka 2003.  Baba Mtakatifu Jumapili tarehe 7 Machi 2021 majira ya mchana atatembelea Jumuiya ya Qaraqosh na kuongoza Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Jioni, Baba Mtakatifu anatarajia kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa “Franso Hariri” huko mjini Erbil na baadaye kurejea tena mjini Baghdad.

Askofu msaidizi Basel Yaldo wa Jimbo kuu la Baghdad anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq itawaimarisha vijana ili kusimama tena kidete kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora kwa nchi yao na kwa vizazi vijavyo. Takwimu zinaonesha kwamba, kabla ya Vita ya Ghuba ya Uajemi vya Mwaka 2003, kulikuwa na Wakristo zaidi ya milioni 1.5, lakini leo hii waamini waliobaki si zaidi ya 400, 000. Wengi wao wameikimbia nchi ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa Dola ya Kiislam “Islamic State, IS”, tangu mwaka 2014 yamesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Iraq ni mahali ambako kuna Makanisa mengi kutoka Mashariki. Iraq pia imekuwa ni jukwaa la majadiliano ya kiekumene. Itakumbukwa kwamba, uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq ni kuendelea kutambua umuhimu wa Wakristo katika ujenzi wa jamii huko nchini Iraq na Mashariki ya Kati katika ujumla wake.

Tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipozindua mchakato wa majadiliano ya kidini katika Tamko lao la “Nostra aetate” yaani “Nyakati Zetu”, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu wa kibinadamu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya waamini wa dini mbali mbali duniani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa Katoliki halikatai yoyote yaliyo kweli na matakatifu katika dini mbali mbali zisizo za kikristo. Lenyewe laheshimu kwa sifa timamu namna zile za kutenda na kuishi, sheria zile na mafundisho yale ambayo, ingawa mara nyingi yanatofautiana na yale ambayo lenyewe laamini na kufundisha, hata hivyo, mara nyingine, yanarudisha nuru ya mshale wa ule Ukweli wenye kumwangazia kila mtu. Kanisa linaendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, njia, ukweli na uzima. Rej. Yn. 14:6. Ndani ya Kristo Yesu kuna utimilifu wa utauwa, na ambamo Mwenyezi Mungu alivipatanisha vitu vyote na nafasi yake.

Askofu msaidizi Basel Yaldo wa Jimbo kuu la Baghdad anasema, Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kutembelea miji ya Baghdad, Erbil, Mosul na Uru ya Wakaldayo maeneo maarufu sana katika mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya: Wayahudi, Waislam na Wakristo. Wote hawa wanaunganishwa pamoja na Mzee Ibrahimu, Baba wa Imani. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2020 alipania kufanya hija ya kitume nchini Iraq lakini kutokana na hali tete ya usalama pamoja na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, hakuweza kutimiza nia hii njema! Ni matumaini ya watu wa Mungu nchini Iraq kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq itasaidia sana kuragibisha mchakato wa amani nchini humo na Mashariki ya Kati katika ujumla wake.

Hija ya Kitume: Amani

 

 

 

 

 

04 March 2021, 16:09