Tafuta

Kamati kuu ya utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa ajili ya Amani na Utulivu inasema, hija ya Papa Francisko nchini Iraq inaandika historia mpya ya imani, matumaini, upendo na mshikamano wa kibinadamu! Kamati kuu ya utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa ajili ya Amani na Utulivu inasema, hija ya Papa Francisko nchini Iraq inaandika historia mpya ya imani, matumaini, upendo na mshikamano wa kibinadamu! 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Haki na Amani!

Hija hii ina umuhimu wa pekee katika Ukanda wa Nchi za Kiarabu kwani inabeba ndanimwe ujumbe wa: upendo na mshikamano kwa waathirika wa vita na vitendo vya kigaidi. Ni hija inayopania kuragibisha udugu wa kibinadamu ndani na nje ya Iraq. Ni tukio la aina yake kwa kiongozi mkuu kama Papa Francisko kuwaongoza watu wa Mungu katika njia ya amani na maridhiano ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jaji Mohamed Abdelsalam, Katibu mkuu mtendaji wa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu katika tamko lake anasema, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kitume nchini Iraq, inayoandika ukurasa mpya wa imani na matumaini. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Ni hija inayofumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, uhamasishaji wa ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Jaji Mohamed Abdelsalam, anasema, watu wa Mungu nchini Iraq wameteseka sana kutokana na vita, mipasuko na migawanyiko ya kijamii pamoja na vitendo vya kigaidi. Baba Mtakatifu Francisko licha ya changamoto kubwa ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, ameamua kujitosa mhanga ili kuwafariji wananchi wa Iraq. Huu ndio udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” na ile Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu. Ratiba elekezi ya hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu inaonesha wazi utashi wake wa kutaka kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu nchini Iraq. Hija hii ina umuhimu wa pekee katika Ukanda wa Falme za Kiarabu kwani inabeba ndanimwe ujumbe wa: upendo na mshikamano kwa waathirika wa vita na vitendo vya kigaidi. Ni hija inayopania kuragibisha udugu wa kibinadamu ndani na nje ya Iraq. Hili ni tukio la aina yake kwa kiongozi mkuu kama Papa Francisko kuwaongoza watu wa Mungu katika njia ya amani na maridhiano ya kweli!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa sahihi kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo.

Kwa kutambua umuhimu na uzito wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu, kumeundwa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati hii na kati ya wajumbe wake ni pamoja na: Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdelsalam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu. Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Amiri Jeshi Msaidizi, watahakikisha kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatekelezwa kwa dhati kabisa na Kamati iliyoundwa, ili kumwilisha malengo yaliyobainishwa kwenye Hati hii.

Katibu mkuu

 

 

04 March 2021, 15:43