Dr. Josè Gregorio Hernàndez kutangazwa mwenyeheri tarehe 30 Aprili 2021 huko Venezuela. Dr. Josè Gregorio Hernàndez kutangazwa mwenyeheri tarehe 30 Aprili 2021 huko Venezuela. 

Dr. Josè G. Hernàndez kutangazwa Mwenyeheri 30 Aprili 2021

Dr. José Gregorio Hernández katika maisha na utume wake, kiasi cha kupendwa na watu wa Mungu nchini Venezuela. Huyu alikuwa ni mwanasayansi mahiri, aliyebobea katika taaluma yake, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, lakini zaidi kwa “maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Ni chemchemi ya matumaini na ufufuko nchini humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mtumishi wa Mungu Dr. José Gregorio Hernández anatarajiwa kutangazwa tarehe 30 Aprili 2021 kuwa Mwenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela (CEV) linabainisha kwamba, tarehe 31 Aprili 2021, Kardinali Marcello Semeralo, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Matukio haya muhimu yataadhimishwa kwenye Uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu cha Venezuela, UCV. Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Mwenyeheri mtarajiwa Dr. José Gregorio Hernández atakuwa anaadhimishwa na kukumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Oktoba. Hii ni tarehe ambayo imezoeleka kwa watu wa Mungu nchini Venezuela.

Baba Mtakatifu ameonesha furaha yake kwa Mama Kanisa kutambua na kuthamini mchango na ushuhuda uliotolewa na Mwenyeheri Mtarajiwa Dr. José Gregorio Hernández katika maisha na utume wake, kiasi cha kupendwa na watu wa Mungu nchini Venezuela. Huyu alikuwa ni mwanasayansi mahiri, aliyebobea katika taaluma yake, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, lakini zaidi kwa “maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Mwenyeheri Mtarajiwa Dr. José Gregorio Hernández alisoma, akafaulu masomo yake na kutunukiwa vyeti mbalimbali vya masomo. Hapa ni mahali ambapo alifanyia kazi za tafiti mbalimbali na matokeo yake ni uvumbuzi wa dawa mbalimbali zinazotumiwa na watu wa Mungu nchini Venezuela.

Kardinali Pietro Parolin, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, ataongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Dr. José Gregorio Hernández kuwa Mwenyeheri. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela kwamba, tukio hili la neema ni ufufuko na upyaisho wa matumaini kwa watu wa Mungu nchini Venezuela. Kardinali Baltazar Porras, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mérida na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Caracas anasema undani wa maadhimisho haya utatolewa kadiri ya siku zinavyokaribia kutokana na wimbi kubwa la maambukizi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maadhimisho haya yamekuja kwa wakati muafaka, walimwengu wanapoendelea kushuhudia maafa makubwa yanayotokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Janga hili limeonesha udhaifu wa binadamu na umuhimu wa kushikamana kwa pamoja katika mapambano dhidi ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maadhimisho haya ni fursa ya kumkimbilia Mwenyeheri mtarajiwa Dr. José Gregorio Hernández, kwa sala na maombi, ili aweze kuwafariji ndugu zake katika kipindi hiki cha mahangaiko makubwa. Mwenyeheri huyu ni kiungo muhimu sana kwa watu wa Mungu nchini Venezuela. Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu nchini Venezuela kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utakatifu wa maisha yake, ni tunu ambayo imewavuta watu wengi nchini Venezuela, hususan huduma ya tiba kwa maskini. Ni rejea kwa ajili ya Venezuela kuanza mchakato wa ujenzi wa haki, amani na umoja wa Kitaifa, baada ya kutikiswa sana katika miaka ya hivi karibuni, changamoto na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani kwa watu wote wa Mungu nchini Venezuela.

Mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Dr. José Gregorio Hernández kuwa Mwenyeheri uliridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Juni 2020. Mchakato huu umedumu takribani miaka 70 tangu Askofu Lucas Guillermo Castillo alipotia nia hii kunako mwaka 1949. Tarehe 16 Januari 1986, Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia aitwe Mtumishi wa Mungu. Hapo tarehe 30 Aprili 2021 atatangazwa kuwa ni Mwenyeheri na baadaye Mwenyezi Mungu akipenda, Kanisa hatimaye, litamtangaza kuwa Mtakatifu.

Venezuela

 

 

26 March 2021, 16:31