Salam za rambirambi kwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021. Salam za rambirambi kwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021. 

Salam za Rambirambi kwa Rais Samia Suluhu wa Tanzania

Askofu mkuu Protase Rugambwa, anapenda kuchukua nafasi hii, kuwaambia watanzania kwamba, hawana sababu ya kuwa na hofu wala kukata tamaa, bali wawe jasiri na moyo mkuu katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi: haki, amani, upendo, ustawi na maendeleo ya wengi. Wajenge na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa na kushirikiana na viongozi wapya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kwa niaba ya Jumuiya ya watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma amemtumia salam za rambirambi Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama kufuatia msiba mkubwa ulioikumba Tanzania. Yaani kifo cha Dkt. John Joseph Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa awamu ya tano nchini Tanzania, aliyefariki dunia hapo tarehe 17 Machi 2021. Askofu mkuu anawatakia watanzania wote rambirambi zake katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Kwa namna ya pekee kabisa anapenda kutoa salam zake za rambirambi kwa viongozi wapya na wale watakaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ili wawe na amani, furaha na utayari wa kuyaendeleza yale mema yaliyotendwa na Hayati Dkt. Magufuli enzi ya uhai wake akishirikiana na watanzania wenzake.

Lengo mahususi liwe ni kwa ajili ya kuiendeleza Tanzania katika misingi iliyoachwa na Dkt. John Pombe Magufuli. Askofu mkuu Protase Rugambwa anaungana na watanzania pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili kumwombea Hayati Dkt. Magufuli maisha na uzima wa milele. Anapenda kuchukua nafasi hii, kuwaambia watanzania kwamba, hawana sababu ya kuwa na hofu wala kukata tamaa, bali wawe jasiri na moyo mkuu katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi: haki, amani, upendo, ustawi na maendeleo ya wengi. Wajenge na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Watanzania wanahamasishwa kushirikiana na viongozi wapya katika ujenzi wa Tanzania. Mwishoni anamwomba, Mwenyezi Mungu aibariki Tanzania na watu wake wote!

Dkt Magufuli
25 March 2021, 16:40