Kardinali Pietro Parolin: Mchango wa Vatican Barani Afrika: Mchakato wa haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Kardinali Pietro Parolin: Mchango wa Vatican Barani Afrika: Mchakato wa haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. 

Mchango wa Vatican Barani Afrika: Haki, Amani na Mafao ya Wengi!

kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema: Kati ya mambo msingi yanayotekelezwa na Vatican Barani Afrika ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa linataka kuwa ni chombo cha matumaini kwa watu wa Mungu Barani Afrika kwa kujikita zaidi katika msingi ya haki; amani, ushirikiano katika ukweli na uwazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa hija yake ya kitume nchini Cameroon, Jumatatu tarehe, 1 Februari 2021, akiwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika ya Kati, “Université Catholique d'Afrique Centrale” (UCAC) amezungumzia kuhusu “Kiti Kitakatifu Barani Afrika: Daraja kati ya Dhana ya Amani na Utekelezaji wa Haki”. Kati ya mambo msingi yanayotekelezwa na Vatican Barani Afrika ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa linataka kuwa ni chombo cha matumaini kwa watu wa Mungu Barani Afrika kwa kujikita zaidi katika msingi ya haki; amani, ushirikiano katika ukweli na uwazi. Kardinali Parolin anasema, Vatican katika masuala ya diplomasia ya Kimataifa inataka kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Dhana hii inatekelezwa kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya, uchumi pamoja na ustawi wa jamii. Lengo ni kutengeneza madaraja yanayowaunganisha watu na Mwenyezi Mungu ili hatimaye, kujenga umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Amani inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Haya ni mambo yanayosimikwa katika kanuni maadili, uhuru wa kujieleza pamoja na mchakato mzima wa maamuzi yanayotolewa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haki na amani ni sawa na chanda na pete, vinakumbatiana na kukamilishana. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza ushirikiano wa Kimataifa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya amani na udugu wa kibinadamu. Kanisa halina budi kuwafunda watoto wake kujenga dhamiri nyofu, ili kukuza majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuwa na uwajibikaji wa pamoja. Rej. GS. 90. Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 6 Januari 1967 alianzisha Tume ya Kipapa ya Haki na Amani na leo hii, kuna Baraza la Maendeleo Fungamani ya Binadamu linalojikita zaidi katika utekelezaji wa haki jamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa ni daraja linalounganisha dhana ya amani na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni kwa ajili ya maboresho ya maisha ya watu wa Mungu.

Kanisa Barani Afrika linataka kuendelea kuwa ni Sakramenti ya Wokovu, kwa kujielekeza zaidi katika misingi ya: haki, maridhiano na ushirikiano wa kweli. Maendeleo fungamani ya binadamu yanagusa mahitaji yake msingi kama ushuhuda wa haki katika maisha ya watu wa Mungu. Falsafa, sera na siasa ya Kanisa Barani Afrika inapania kujenga daraja la dhana ya amani na mshikamano wa dhati, ili kukidhi mahitaji msingi ya binadamu; kwa kukazia: haki, amani ya kudumu na ushirikiano wa kweli. Haki ya kweli inafumbatwa katika mshikamano unaothamini tunu msingi, utu na heshima ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia. Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maagamizi, kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali mawazo ya vitisho na hofu. Baba Mtakatifu katika ujumbe huo wa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 anapembua kwa kina na mapana amani, kama safari ya matumaini inayokabiliana na vizingiti pamoja na majaribu. Amani ni safari ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza unaosimikwa katika kumbu kumbu, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Amani ni safari ya upatanisho katika umoja wa kidugu. Amani ni safari ya wongofu wa kiekolojia na kwamba, watu wataweza kupata yale yote wanayotumainia.

Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza ushirikiano wa Kimataifa katika mambo ya kiuchumi, kwa kuwapatia raia elimu bora zaidi, ili waweze kushika majukumu katika sekta mbalimbali za maisha. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni dhana inayohitaji ushiriki mkubwa wa Jumuiya ya Kimataifa, utu, heshima na haki msingi za binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Lengo ni kupambana na umaskini, ujinga na maradhi yanayoendelea kupekenya utu wa binadamu. Mahitaji msingi ya binadamu yanapaswa kuwa ni kitovu cha maendeleo na ustawi wa binadamu.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Kanisa limekwisha kuchangia sana kuhusu dhana ya amani inayomwilishwa katika haki. Pengine, kwa sasa unakosekana utashi wa kunafsisha dhana hii katika hali halisi ya watu wa Mungu, kwa kukazia utashi wa kimaadili na kiutu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Diplomasia ya Vatican inasimikwa katika misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maana mambo ya kidunia na yale ya kiimani, asili yake ni katika Mungu yule yule. Utu wa binadamu hauna budi kulindwa na kuheshimiwa. Mchakato wa ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu unapania kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi ili kuvunjilia mbali vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini na kisiasa. Ni mwaliko wa kusimama kidete kupambana na ujinga, umaskini na maradhi.

Kwa ufupi kabisa, tarehe 29 Januari 2021 Kardinali Pietro Parolin amekutana na kuzungumza na Rais Paul Biya wa Cameroon na hivyo kumkabidhi ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Mpasuko wa kisiasa nchini Cameroon kati ya wananchi wanaozungumza lugha ya Kiingereza na Kifaransa ni kati ya mambo ambayo yameguswa na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo. Kardinali Parolin amekutana na kuzungumza pia na Baraza la Maaskofu Katoliki Nchini Cameroon. Tarehe 31 Januari 2021, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Mitume na kumvisha Pallio Takatifu, Askofu mkuu Andrew Nkea Fuanya wa Jimbo kuu la Bamenda nchini Cameroon. Kardinali Pietro Parolin akiwa nchini Cameroon, amebahatika pia kutembelea “Home of Hope in Yaoundè” yaani “Nyumba ya Matumaini mjini Yaoundè iliyoanzishwa na Padre Yves Lescanne, SJ., miaka 40 iliyopita. Lengo la Kituo hiki ni kuwasaidia na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi pamoja na wale waliomaliza adhabu yao magerezani.

Diplomasia ya Kanisa
02 February 2021, 17:23