Chanjo ni haki ya kila mtu kuhakikisha kwamba, anapata chanjo kwa sababu huu ni wajibu wa kimaadili na mshikamano wa utu wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Chanjo ni haki ya kila mtu kuhakikisha kwamba, anapata chanjo kwa sababu huu ni wajibu wa kimaadili na mshikamano wa utu wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. 

Chanjo Dhidi ya Virus Vya UVIKO-19: Haki na Wajibu wa Kimaadili

Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ni haki ya wote. na wajibu wa kimaadili. Na haki hii inatekelezwa kwa njia ya mshikamano wa udugu unaotekelezwa kwa kuzingatia kanuni auni, ili kuleta matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na janga hili. Mataifa tajiri zaidi ulimwenguni yamewekeza sana katika tafiti na hatimaye chanjo imeanza kupatikana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, chanjo ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii, watu wanajenga udugu na ujirani mwema kwa njia ya chanjo, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza kutokana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili hatimaye, kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Huu ni utamaduni unaosababisha maafa na utengano! Ujirani mwema ni dhana inayopaswa kufanyiwa kazi, ili kujenga umoja na mafungamano ya kijamii, kitaifa na ndani ya Kanisa katika ujumla wake. Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ni wajibu wa kimaadili kwa kila mtu, ili kuhakikisha usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Hakuna mtu anayeweza kujidai kuwa ni salama dhidi ya UVIKO-19, kwani huu ni ugonjwa hatari ambao haubagui wala kuchagua. Kwa bahati mbaya sana, chanjo hii imepokelewa kwa hisia tofauti sana na malengo yanayokusudiwa kisayansi!

Ufanisi na usalama wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO kwa wakati huu. Chanjo dhidi UVIKO-19 lazima ipatikane kwa kila mtu mahali alipo! Huu ndio mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa mapambano dhidi ya UVIKO-19. Hivi karibuni, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Maisha (Pontificia Academia Pro Vita), wamechapisha Waraka unaoonesha umuhimu wa chanjo; na chanjo Kama Sehemu ya mafao ya wengi. Waraka huu ulitoa angalisho dhidi ya chanjo zinazokumbatia utaifa, kwa baadhi ya Mataifa kutaka kuwa na chanjo zake binafsi, kwa kuhakikisha kwamba, zinapata kiasi kikubwa cha dawa ya chanjo kwa ajili ya wananchi wake. Hii ni hatari sana, kwani uzalishaji na usambazaji wa chanjo hii unaweza kujikuta unawanufaisha watu wachache peke yao na hivyo, kutawala soko la chanjo kwa kupanga bei wanayoitaka wao wenyewe hata kama ni kwa hasara ya watu wengi duniani.

Chanjo lazima ithibitishwe kuwa salama na yenye ufanisi kwa idadi kubwa ya watu kabla ya kuidhinishwa na kuingizwa kwenye programu za kitaifa na kimataifa za chanjo. Kizuizi cha usalama na ufanisi wa chanjo ni kikubwa sana, kwa kutambua kwamba chanjo hupewa watu ambao wana afya njema na haswa ambao hawana maradhi au kwa maneno mengine sio wagonjwa. Ufuatiliaji zaidi unapaswa kufanywa baada ya chanjo kutolewa ili kubainisha usalama na ufanisi wa chanjo. Hii inawawezesha wanasayansi kufuatilia athari na usalama wa chanjo hata kama zinatumiwa kwa idadi kubwa ya watu na kwa muda mfrefu. Takwimu hizi hutumiwa kurekebisha sera za matumizi ya chanjo ili kuongeza tija, ufanisi na usalama wa chanjo zinazotolewa.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, linaendelea kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutambua kwamba, chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ni haki ya wote. Na haki hii inatekelezwa kwa njia ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaotekelezwa kwa kuzingatia kanuni auni, ili kuleta matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na janga hili. Mataifa tajiri zaidi ulimwenguni yamewekeza sana katika tafiti na hatimaye chanjo imeanza kupatikana! Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, Nchi tajiri zaidi zimejiwekea mkakati wa chanjo kwa ajili ya raia wake, kwa kuongozwa na sera za utaifa, Nchi maskini zaidi duniani zinazonekana kuwekwa kando ya sera na mipango ya chanjo duniani.

Katika hali na mazingira ya sasa ambamo kuna maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, inawezekana kabisa kutumia chanjo zote zinazotolewa na wataalam wa sayansi na tiba ya mwanadamu, ikiwa kama zimethibitishwa kuwa ni salama na zenye ufanisi, kwa kuongozwa na dhamiri nyofu kwamba, matumizi ya chanjo hizi hayamaanishi kwamba, watumiaji wanashiriki au kuunga mkono vitendo vya utoaji mimba vinavyokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limetoa Tamko hili wakati ambapo sehemu mbalimbali za dunia wameanza kampeni ya chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linakaza kusema ni wajibu wa kimaadili kwa makampuni ya dawa, mawakala na watengenezaji wa dawa za Serikali kuhakikisha kwamba, wanazalisha, wanaidhinisha, kugawa na kutoa chanjo ambazo zinakubalika kimaadili na kiutu, ambazo kimsingi hazisababishi matatizo kwenye dhamiri za watu.

Ufafanuzi huu unapania kuondoa wasiwasi, hofu na mashaka ambayo yameibuliwa, wakati mwingine kwa kuwajengea watu hofu isiyokuwa na msingi hata kidogo! Chanjo inapaswa kuwafikia watu wote kwa haki na usawa. Hawa ni watu wa Mungu kutoka Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Lengo kuu la chanjo hii ni kuokoa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwani maisha bora ni haki msingi ya binadamu. Maskini, wazee, wakimbizi na wahamiaji ni kati ya makundi ambayo yanakabiliana na hatari kubwa za maambukizi Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Huu ni wakati muafaka kwa wanasiasa kuweka kando masilahi binafsi na utaifa usiokuwa na mashiko. Umuhimu wa chanjo hii unapaswa kuangaliwa kwa masilahi mapana ya usalama, ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Kushindwa kutekelezwa kwa sera hii ni anguko la kimaadili na utu wema! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulivalia junga janga la UVIKO-19. Hii ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuzifutia madeni Nchi maskini zaidi duniani, ili fedha hii itumike katika mchakato wa maboresho ya huduma bora ya afya na usalama.

Kwa kuzingatia haki ya umiliki wa chanjo dhidi ya maambukizi Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kuna haja ya kuanza kufikiria uzalishaji kufanyika Barani Afrika, Amerika ya Kusini na Barani Asia, ili kuharakisha mchakato wa chanjo katika maeneo haya kabla mambo hayajaharibika. Mchakato huu uyashirikishe pia Mashirika ya kidini kwani yana uzoefu na miundo mbinu ya huduma ya afya. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis yanalitaka Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kukutana na kujadiliana kuhusu chanjo ya UVIKO-19 kwa sababu janga hili ni tishio kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Kumbe, maamuzi yake yanapaswa kuzingatia masilahi mapana zaidi ya Jumuiya ya Kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa iangalie uwezekano wa kufuta madeni kwa Nchi maskini zaidi duniani. Ni wakati muafaka kwa chanjo kuzalishwa pia Barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini kwa kuzingatia haki miliki pamoja na ushirikiano wa kiteknolojia na Nchi changa zaidi. Fedha maalum itengwe ili kusaidia juhudi za vyama vya kiraia katika Nchi maskini zaidi, ili kuzijengea uwezo wa kiuchumi katika mchakato wa kuragibisha mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Chanjo: Haki na Wajibu

 

08 February 2021, 15:39