Chama cha Rondine kilianzishwa kunako mwaka 1988 nchini Italia na kinapania kuwafunda vijana kutokana katika  maeneo ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ili kuwa wajenzi wa haki, amani na upatanisho Chama cha Rondine kilianzishwa kunako mwaka 1988 nchini Italia na kinapania kuwafunda vijana kutokana katika maeneo ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ili kuwa wajenzi wa haki, amani na upatanisho 

Chama cha Rondine na Mchakato wa Ujenzi wa Upatanisho na Amani

Lengo ni kuwawezesha vijana kuwa viongozi watakaosimamia: haki, amani, ustawi na mafao ya wengi! Chama cha “Rondine” kinapania kugeuza kinzani na mipasuko ya kijamii kuwa ni fursa kwa vijana kugundua utu na heshima ya binadamu, ambao hapo awali waliwaona kuwa ni adui. Chama cha “World House of Rondine” kilianzishwa na Franco Vaccari kunako mwaka 1988 nchini Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha “World House of Rondine” ni mkusanyiko wa raia kutoka Kaskazini mwa Italia wanaowekeza hasa katika majadiliano ili kupunguza, kama si kuondoa kabisa migogoro na vita sehemu mbali mbali za dunia kwa kuwekeza zaidi katika elimu makini na majiundo endelevu na fungamani miongoni mwa vijana. Lengo ni kuwawezesha vijana wa kizazi kipya kuwa viongozi watakaosimamia amani, ustawi na maendeleo ya wengi kuanzia mahali walipo! Chama cha “Rondine” kinapania kugeuza kinzani na mipasuko ya kijamii kuwa ni fursa kwa vijana kugundua utu na heshima ya binadamu, ambao hapo awali waliwaona kuwa ni adui wanaopaswa kufyekelewa mbali! Chama cha “World House of Rondine” kilianzishwa na Franco Vaccari kunako mwaka 1988 nchini Italia.

Nia ya Vatican kwenye uwanja wa diplomasia kimataifa ni kuhakikisha kwamba: wadau mbali mbali wanahusishwa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, ndiyo maana Vatican katika kipindi cha takribani miaka ishirini imeendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Chama cha “Rondine” kama sehemu ya mchakato wa unaopania kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu; malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, kwa siku za usoni wawe ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa haki, amani na mshikamano wa kidugu duniani; watu wanaoweza kujadiliana na wengine na kutafuta suluhu kwa njia ya amani badala ya kukimbilia mtutu wa bunduki. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 15 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa vijana wa Chama cha “World House of Rondine”.

Hawa ni vijana wanaotoka katika maeneo ambayo yamegubikwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, lakini kwa sasa wanatamani kuwa ni wajenzi na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Amewahakikishia kwamba, atamjulisha Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mkutano huu na nia yao ya kujizatiti katika ujenzi wa misingi ya haki na amani duniani. Katika kundi hili kuna vijana kumi na moja waliochaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kama sehemu ya utekelezaji wa mradi wa elimu kwa ajili ya amani na upatanisho Ukanda wa Mediterrania. Eneo la Mashariki ya Kati na Bahari ya Mediterrania yamegeuka kuwa ni uwanja vya vita vinavyotokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi, chuki na uhasama; mambo ambayo yanapaswa kurekebishwa kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; upatanisho, haki na amani! Kuna haja ya kujenga “Tasaufi ya Amani Ukanda wa Mediterrania", ili kuliwezesha Kanisa kushiriki kikamilifu katika mahangaiko na matumaini ya watu waliokata tamaa ya maisha.

Kardinali Pietro Parolin, ametembelea Jimbo kuu la Arezzo-Cortona-Sansepolcro, na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na vijana waliomo kwenye mradi wa elimu kwa ajili ya amani na upatanisho Ukanda wa Mediterrania. Lengo ni kuendelea kuwasaidia vijana kuwa ni chachu ya mageuzi kijamii na kitamaduni, ili kujenga na kudumisha ari na moyo wa ushirikiano wa udugu wa Kimataifa, tayari kuanza kujikita katika ujenzi wa amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mfumo wa elimu unaokita mizizi yake katika majadiliano, upatanisho na ujenzi wa amani ya kudumu, ili hatimaye, kujenga mtandao wa maendeleo fungamani na shirikishi. Katika mkutano huu, Kardinali Pietro Parolin alikuwa ameambatana na Askofu mkuu Riccardo Fontana wa Jimbo kuu la Arezzo-Cortona-Sansepolcro, Riccardo Fontana pamoja na Bwana Domenico, Rais wa Kampuni ya ENEL.

Vatican inaunga mkono kampeni ya uragibishaji kwa ajili ya kupata viongozi kwa ajili ya amani duniani: “Leaders for peace”. Chama hiki kinawaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kukiunga mkono kwa kuchangia sehemu ya bajeti yake, ili kuwafunda vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani duniani. Kinapania pamoja na mambo mengine kuwaandaa viongozi wa leo na kesho bora zaidi ya mataifa duniani kwa kujikita katika haki msingi za binadamu. Uhuru wa kidini ni msingi wa: haki, utu na heshima ya binadamu! Uhuru wa kidini ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kukuzwa na kudumishwa na wote kwani ni msingi wa haki zote za binadamu, utu na heshima yake.

Kumbe, umoja na mshikamano; amani na utulivu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni muhimu sana!  Jumuiya ya Kimataifa katika kipindi cha mwaka 2018 iliadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, changamoto kwa sasa ni ujenzi wa amani duniani inayofumbatwa katika ukweli, haki, mshikamano tendaji na uhuru wa kweli! Ikumbukwe kwamba, haki msingi za binadamu ni msingi na mhimili mkuu wa: amani, ustawi, maendeleo, mafao, umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Parolin: Rondine

 

17 February 2021, 15:03