Baba Mtakatifu amemteuwa Mheshimiwa Padre  Luis Marin de San Martin kuwa Askofu na Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu. Baba Mtakatifu amemteuwa Mheshimiwa Padre Luis Marin de San Martin kuwa Askofu na Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu. 

Askofu mteule Luis M. De S. Martin: Katibu Mkuu Msaidizi Sinodi

Askofu mteule Luis Marín de San Martín, O.S.A. alizaliwa tarehe 21 Agosti 1961. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, tarehe 1 Novemba 1985 akaweka nadhiri zake za daima katika Shirika la Waagostiani. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 4 Juni 1988. Baadaye amejiendeleza zaidi katika tasaufi ya kitaalimungu, Mafundisho Sadikifu ya Kanisa pamoja na Utunzaji wa Nyaraka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Luis Marín de San Martín, O.S.A., kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Luis Marín de San Martín, O.S.A. alizaliwa tarehe 21 Agosti 1961. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, tarehe 1 Novemba 1985 akaweka nadhiri zake za daima katika Shirika la Waagostiani “The Order of St. Augustine”. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 4 Juni 1988. Baadaye amejiendeleza zaidi katika tasaufi ya kitaalimungu, Mafundisho Sadikifu ya Kanisa pamoja na Utunzaji wa Nyaraka. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Paroko, Mlezi wa vijana, Seminari kuu ya Tagaste huko Los Negrales kati ya Mwaka 2002 hadi mwaka 2008, Mshauri mkuu wa Shirika kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2002. Aliwahi kuwa Mkuu wa Monasteri ya “Santa María de La Vid kati ya mwaka 2002-2008; Mkurugenzi wa Taasisi ya Waagostiniani huko Los Negrales. Amekuwa pia ni Jaalimu wa “kutupwa” katika taasisi mbalimbali za Shirika.

Askofu mteule Luis Marín de San Martín hadi kuteuliwa kwake, amekuwa ni Mtunza Nyaraka za Shirika, Makamu mkuu wa Shirika na Rais wa Taasisi ya Tasaufi ya Waagustiani “Institutum Spiritualitatis Augustinianae” tangu mwaka 2013. Ni mwandishi maarufu, mtoa mafungo kwa miaka mingi na amebahatika kufanya kazi na waamini walei kwa muda mrefu! Katika mahojiano maalum na Vatican News, Askofu mteule Luis Marín de San Martín anasema, dhamana na wajibu wake, ni kumsaidia Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika mchakato wa kuragibisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa sasa kuna maandalizi ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2022 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume”. Huu ndio mwelekeo wa maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni changamoto iliyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Wanazungumzia kuhusu: Walei katika Kanisa, Tabia na utume wa waamini walei, hadhi ya walei katika Taifa la Mungu pamoja na Utume wa waamini walei.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha pia majukumu yao ya Kikuhani, Kinabii na Kifalme; mambo yanayofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka, kwa kuulisha Ulimwengu matunda ya kiroho sanjari na kumwilisha Heri za Mlimani, Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Rej. LG. 31-38. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia umuhimu wa Kanisa, Watu wa Mungu, Familia ya Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo. Lengo ni kujenga jumuiya ya waamini inayotangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Yote haya yanawezekana ikiwa kama yatanafsishwa katika dhana ya Sinodi. Hii ni changamoto yenye mashiko katika maisha na utume wa Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemteua pia Mheshimiwa Sr. Nathalie Becquart, kuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Sinodi za Maaskofu. Baba Mtakatifu anajitahidi kutekeleza maazimio mbalimbali yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi. Kumbe, wakleri, watawa na walei, wote kwa pamoja wanaunda Familia Takatifu ya Watu wa Mungu, wanaopaswa kushirikiana na kushikamana. Uteuzi huu ni kielelezo cha ujasiri wa Baba Mtakatifu Francisko anayetambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Askofu mteule Luis Marín de San Martín amehitimisha mahojiano maalum na Vatican News kwa kuwaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza kwa njia ya sala na sadaka zao, wanapojitahidi kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu Luis
11 February 2021, 14:21