Tafuta

Rais Joseph Robinette Biden Jr. wa Marekani tarehe 20 Januari 2021 amesimikwa rasmi na hivyo kuwa ni Rais wa 46 nchini Marekani. Anashika madaraka wakati huu Marekani ikiwa inakumbana na changamoto pevu katika historia yake. Rais Joseph Robinette Biden Jr. wa Marekani tarehe 20 Januari 2021 amesimikwa rasmi na hivyo kuwa ni Rais wa 46 nchini Marekani. Anashika madaraka wakati huu Marekani ikiwa inakumbana na changamoto pevu katika historia yake. 

Rais Joe Biden wa Marekani: Changamoto Katika Uongozi Wake!

Rais Joe Biden amefungua ukurasa mpya wa matumaini kwa wananchi wa Marekani ambao wanakabiliwa na changamoto kubwa katika historia ya nchi yao. Mosi ni maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19; Athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi; mifumo ya ubaguzi inayosababisha mipasuko ya kijamii pamoja na mchango wa USA katika Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Donald Trump aliyeongoza kwa muda wa miaka minne tu, kwa kutumia kauli mbiu: "Marekani kwanza" amemaliza muda wake madarakani, kwa mara ya kwanza amewasihi Wamarekani "kuiombea" mafanikio serikali ya Rais Joe Biden ambaye amekula kiapo tarehe 20 Januari 2021 na hivyo kushika madaraka na kuwa ni Rais wa 46 wa Marekani. Pamoja na watu wa Mungu nchini Marekani kuwa na matumaini mapya kutokana na Rais Biden kushika madaraka, lakini anakabiliwa na changamoto kubwa ambayo ni maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Donald Trump alipuuzia na kuiacha Marekani ikitumbukia katika janga hili na hivyo kushika nafasi ya kwanza duniani. Chanjo dhidi ya COVID-19 ni kati ya vipaumbele vya kwanza kwa Serikali mpya ya Marekani. Biden na mkewe Jill, sanjari na Makamu wa Rais Kamala Harris, ambaye ni mwanamke wa kwanza katika historia ya Marekani kushika wadhifa huo, kwanza wamehudhuria hafla ya kumbukumbu katika Bwawa lililopo kwenye Makumbusho ya Lincoln, ili kuwakumbuka na kuwaombea Wamarekani 400,000 waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Corona, COVID-19.

Serikali ya Rais Biden inatarajia kutumia kiasi cha dola trilioni 1.9 za kimarekani kwa ajili ya kupambana na Corona, COVID-19 pamoja na harakati za kufufua uchumi wa Marekani. Rais Biden anatarajia kuirejesha Marekani katika utekelezaji wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015. Katika mkutano huo, Jumuiya ya Kimataifa ilipitisha mkataba mpya wa Paris ambao umeweka historia mpya kwa nchi 195 kukubali kushirikiana katika kushughulikia athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kupitisha mkataba mpya wa kisheria unaozijumuisha nchi zote katika kupunguza gesi joto duniani. Makubaliano haya yanatoa taswira, mwelekeo, na malengo ambayo nchi zote duniani zinashiriki katika kupunguza gesi joto ili kufikia lengo la dunia la kutokuongezeka kwa wastani wa joto la dunia kwa zaidi ya nyuzi 20C au 1.50C. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto ya kimaadili inayoendelea kuvaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Hatua hii ni muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri zaidi nchi changa duniani hasa katika sekta muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi, ustawi na maendeleo ya wengi kama vile: kilimo, mifugo, uvuvi na utalii. Vikosi vya ulinzi na usalama nchini Marekani vimeimarisha ulinzi na usalama kutokana na hofu ya misimamo mikali ya kisiasa na kiitikadi ambayo imewagawa na kuwapekenya sana wananchi wa Marekani katika miaka ya hivi karibuni. Hizi zote ni changamoto zinazomkabili Rais Biden katika uongozi wake, ambao tangu mwanzo unapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya ubaguzi, misimamo mikali ya kiitikadi, magonjwa na umaskini kutokana na kuchechemea kwa uchumi wa Marekani na hivyo athari zake kuwakumba maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Rais Biden anataka kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa “America United”. Ni kwa njia ya umoja, mshikamano na udugu wa kitaifa utakaoiwezesha Marekani kushinda changamoto za ndani na hivyo kuanza tena kushiriki katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umoja wa Kitaifa ni changamoto ambayo pia ilitolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Marekani kunako mwaka 2015. Aliwataka Wamarekani kuondokana na mifumo ya ubaguzi na kuanza kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa umoja, maridhiano na upatanisho wa Kitaifa kwa kufanya kazi kwa pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Marekani. Kuna haja ya kukuza na kudumisha amani, utulivu na maridhiano, kwa kufyekelea mbali ukosefu wa haki jamii. Marekani kwa kuzingatia kwanza: utu, heshima na haki msingi za binadamu tangu nchini mwake, iweze tena kurejea na kutoa mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ubaguzi wa rangi ni dhambi ambayo imeendelea kuwapekenya Wamarekani kwa miaka mingi. Ni matumaini ya wapenda amani duniani kwamba, uwepo na ushiriki mkamilifu wa Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani, atasaidia kuganga na kuponya madonda ya kashfa ya ubaguzi wa rangi ambayo katika ulimwengu mamboleo imepitwa na wakati, kwani wote wanahamasishwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na udugu wa kibinadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” katika sura ya tano, anapembua kwa nina na mapana kuhusu siasa safi zaidi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa amani na utunzaji bora wa mazingira anapenda kuwachangamotisha wanasiasa, kuhakikisha kwamba, wanaondokana na mizizi ya dhambi inayowatumbukiza watu wengi katika majanga na badala yake, wajikite katika ujenzi wa siasa safi na amani kwa kukataa kishawishi cha uchu wa mali na madaraka. Wanasiasa wapambane na unafsia wa haki msingi za binadamu; maamuzi mbele, ubaguzi wa rangi; hofu zisizokuwa na mvuto wala mashiko; sera potofu dhidi ya wakimbizi na wahamiaji; yote haya ni mambo ambayo yanasigana kimsingi na siasa safi kama huduma ya amani. Uwajibikaji na utunzaji wa amani unafumbatwa katika siasa safi kwa kukita mizizi yake katika sakafu ya moyo wa mtu. Heri yao wanaojitaabisha katika ujenzi wa amani; amani jamii, amani katika utunzaji bora wa mazingira na amani katika dhamiri za watu!

Siasa Marekani

 

21 January 2021, 06:54