Kardinali Pietro Parolin ametembea na kuzungumza na wafanyakazi wa Hospitali ya Bambino Gesù kama sehemu ya utamaduni wa salam na matashi mema wakati wa Sherehe za Noeli. Kardinali Pietro Parolin ametembea na kuzungumza na wafanyakazi wa Hospitali ya Bambino Gesù kama sehemu ya utamaduni wa salam na matashi mema wakati wa Sherehe za Noeli. 

Papa Francisko: Salam na Matashi Mema Kwa Wagonjwa Bambino Gesù

Amewashukuru wafanyakazi hawa kwa kutekeleza dhamana na wajibu wao: kitaaluma na kwa weledi; kwa moyo wa ukarimu na mapendo na kwa kuongozwa na dhamiri nyofu. Vatican inaipongeza Hospitali ya Bambino Gesù kwa kuonesha utayari na umahiri wa kuweza kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020 amekwenda na kutembelea Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, ili kutoa heri na baraka za Sherehe za Noeli. Alipowasili, amepokelewa na Professa Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù. Kardinali Parolin ametumia fursa hii, kuungana na wafanyakazi wote wa Hospitali ya Bambino Gesù kwa njia ya mtandao ili kuwasilisha salam na matashi mema ya Noeli kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Kwa namna ya pekee kabisa, Kardinali Parolin amemshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aliyemwezesha tena, licha ya maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19 kuweza kutembelea na kusalimiana na wafanyakazi wa Hospitali ya Bambino Gesù hata kama ni kwa njia ya mitandao. Amewashukuru wafanyakazi hawa kwa kutekeleza dhamana na wajibu wao: kitaaluma na kwa weledi; kwa moyo wa ukarimu na mapendo na kwa kuongozwa na dhamiri nyofu.

Vatican inaipongeza Hospitali ya Bambino Gesù kwa kuonesha utayari na umahiri wa kuweza kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Haya ni majibu makini yanayobubujika kutokana na uzoefu wa kila siku kutoka hospitalini hapo, uzoefu unaofumbata utajiri na amana za kiutu na kiroho, ili kupambana na janga hili ambalo kwa sasa ni hatari sana na tishio kwa usalama na maisha ya binadamu bila kusahau magonjwa yanayowatesa watoto ambao kimsingi ndio walengwa wakuu wa Hospitali ya Bambino Gesù. Watoto wagonjwa katika salam zao na matashi mema, wameandika kwamba, “Sala zao zina nguvu zaidi kuliko hata ugonjwa wa Corona, COVID-19”. Kadi hii ya salam za Noeli, imechukuliwa na Kardinali Pietro Parolin na ameihifadhi kwenye ofisi yake kama kumbukumbu ya Noeli kwa Mwaka 2020.

Kardinali Pietro Parolin, kabla ya kuzungumza na wafanyakazi wote, alipata nafasi ya kukutana kwa faragha na kikundi cha madaktari ambao wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Amewapongeza kwa kufanya kazi kwa umoja na mshikamano na hivyo kupata ufanisi mkubwa katika shughuli zao. Wameweza kutumia rasilimali watu, fedha na vitu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kardinali Parolin amemshukuru na kumpongeza Professa Mariela Enock, kwa kuongoza na kuratibu vyema mapambano haya. Hii ni sehemu ya utamaduni na mapokeo ya Hospitali ya Bambino Gesù inayoendelea kujipambanua kwa huduma makini ya afya hasa miongoni mwa watoto wadogo na katika hatari na magonjwa ya dharura.

Bambino Gesù

 

24 December 2020, 16:01