Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limetoa Tamko linaloangalisha kuhusu kanuni maadili na utu wema ya chanjo ya dhidi Virusi vya COVID-19. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limetoa Tamko linaloangalisha kuhusu kanuni maadili na utu wema ya chanjo ya dhidi Virusi vya COVID-19. 

Kanuni Maadili Chanjo Dhidi ya COVID-19: Tamko Kutoka Vatican

Kutokana na maambukizi makubwa ya COVID-19, inawezekana kutumia chanzo zote zinazotolewa na wataalam wa sayansi na tiba ya mwanadamu, ikiwa kama zimethibitishwa kuwa ni salama na zenye ufanisi. Matumizi ya chanjo hizi hayamaanishi kwamba, watumiaji wanashiriki au kuunga mkono vitendo vya utoaji mimba vinavyokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chanjo lazima ithibitishwe kuwa salama na yenye ufanisi kwa idadi kubwa ya watu kabla ya kuidhinishwa na kuingizwa kwenye programu za chanjo sehemu mbalimbali za dunia. Matumizi ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, licha ya madhara yake makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu imepokelewa kwa hisia tofauti sana. Kuna baadhi ya watu wanatuhumu chanjo hii kuwa si salama kwa sababu imekiuka kanuni maadili na utu wema kwa kutumia chembechembe kutoka kwenye maiti za watoto waliotolewa mimba. Baadhi ya watu wamekwenda mbali zaidi kwa kusema, Chanjo hii inapania kudhibiti ongezeko la watu duniani kutokana na dalili za watu kukengeuka na kukosa uadilifu na uaminifu katika taaluma zao. Ni katika muktadha huu, Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa akiwa ameambatana na Askofu mkuu Giacomo Morandi, tarehe 17 Desemba 2020 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utata wa kimaadili juu ya matumizi ya chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Baada ya mazungumzo hayo, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limechapisha Tamko linaloonesha kwamba, kimaadili, inaruhusiwa kutumia chanjo dhidi COVID-19 ambayo imetumia chembechembe zinazotokana na mimba zilizoharibiwa katika mchakato wa tafiti na hatimaye, utengenezaji wa chanjo hii. Katika hali na mazingira ya sasa ambamo kuna maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, inawezekana kabisa kutumia chanjo zote zinazotolewa na wataalam wa sayansi na tiba ya mwanadamu, ikiwa kama zimethibitishwa kuwa ni salama na zenye ufanisi, kwa kuongozwa na dhamiri nyofu kwamba, matumizi ya chanjo hizi hayamaanishi kwamba, watumiaji wanashiriki au kuunga mkono vitendo vya utoaji mimba vinavyokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limetoa Tamko hili wakati ambapo sehemu mbalimbali za dunia wameanza kampeni ya chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ufafanuzi huu unapania kuondoa wasiwasi, hofu na mashaka ambayo yameibuliwa, wakati mwingine kwa kuwajenga watu hofu isiyokuwa na msingi.

Tamko hili linafanya rejea pia katika matamko mengine yaliyotolewa na Taasisi ya Kipapa ya Maisha ambayo kunako mwaka 2005 ilifafanua kuhusu matumizi ya chembe chembe zinatokana na mimba zilizoharibiwa. Na hatimaye tarehe 5 Juni 2008 ikachapisha: “Dignitatis persone” yaani “Mwongozo Kuhusu Utu wa Binadamu” uliopitishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Kunako mwaka 2017, Taasisi hii pia ikatoa Angalisho kuhusu Utu wa Binadamu. Nyaraka zote hizi zinatoa mwongozo juu ya mada inayozungumziwa kwa sasa! Si lengo wala nia ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoa hukumu kuhusu usalama na ufanisi wa matumizi ya chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, kwani hii ni dhamana na wajibu wa watafiti wa magonjwa na tiba ya mwanadamu, makampuni pamoja maduka ya dawa. Baraza hili linapenda kujielekeza zaidi katika masuala ya kanuni maadili na utu wema. Chembe chembe zinazotumika ni zile za miaka 1960.

Hapa kuna wajibu unaotofautiana na wala hauna uhusiano wowote ule wa wale na wanaotoa uamuzi wa kutumia chembe chembe hizi kinyume cha sheria, kanuni na taratibu zilizokubaliwa katika uzalishaji wa chanjo hizi na wale ambao hawana uwezo wa kutoa maamuzi yao katika mchakato mzima. Kimaadili na kiutu inakubalika kutumia chanjo iliyotengenezwa kutokana na chembe chembe za mimba zilizoharibiwa. Mtu anaweza kuamua kutokutumia chanjo hii, lakini kutokana na madhara na hatari kubwa ya ugonjwa huu unaoendelea kusababisha vifo vya watu wengi duniani, kumbe, inaruhusiwa kutumia chanjo zote zinazopatikana, ikiwa kama zimeidhinishwa kuwa ni salama na zina ufanisi mkubwa katika kuzuia ugonjwa wa Corona, COVID-19. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linakaza kusema ni wajibu wa kimaadili kwamakampuni ya dawa, mawakala na watengenezaji wa dawa za Serikali kuhakikisha kwamba, wanazalisha, wanaidhinisha, kugawa na kutoa chanjo ambazo zinakubalika kimaadili na kiutu, ambazo kimsingi hazisababishi matatizo kwenye dhamiri za watu.

Ikumbukwe kwamba, kimsingi chanjo si kanuni wala jambo la lazima kimaadili, bali linapaswa kuwa ni hiyari ya mtu mwenyewe na inapaswa kuzingatia mafao na ustawi wa wengi katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Chanjo itoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Kwa wale wanaokataa kutumia chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa sababu mchakato wa chanjo hii umetumia pia chembe chembe za mimba zilizoharibiwa wakumbuke kwamba, wanao wajibu wa kimaadili kuhakikisha kwamba, wanajilinda wao wenyewe na wala wasiwe ni sababu ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa watu wengine. Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, usalama na afya za watu wengine zinalindwa kikamilifu. Mwishoni, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasema ni wajibu wa kimaadili na kiutu kuhakikisha kwamba, chanjo zinazotengenezwa ni salama na zenye ufanisi. Chanjo hizi zitengenezwe kiasi kwamba, zinaweza kukubalika kutumiwa na watu kutoka katika Nchi zinazoendelea bila shaka wala wasi wasi. Bila chanjo hizi kuwafikia wananchi hawa, huu utakuwa ni mwelekeo wa ubaguzi na ukosefu wa haki katika matumizi ya rasilimali za dunia!

Chanjo COVID-19
22 December 2020, 10:57