Baraza la Makardinali washauri wa Papa wafanya mkutano Desemba Mosi!
VATICAN NEWS
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msemaji wa vyombo vya habari Vatican amethibitisha juu ya kufanyika mkutano wa Baraza la Makardinali washauri wa Papa tarehe 1 Desemba 2020, jioni saa 10:00. Katika muktadha wa sasa wa janga la kiafya, mkutano huo umefanyika kwa njia ya mtandao. Waliounganishwa kwenye mkutano huo ni Kardinali Óscar A. Rodríguez Maradiaga, S.D.B., Kardinali Reinhard Marx, Sean Patrick O’Malley, O.F.M. Kap., Kardinali Oswald Gracias, na Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, O.F.M. Kap., wakati mjini Vatican walikuwepo Kardinali Pietro Parolin, Kardinali Giuseppe Bertello na Katibu wa Baraza la makardinali washauri, Askofu Marco Mellino.
Hata na Papa Francisko ameshiriki mkutano huo kwa kuunganishwa akiwa katika Makazi yake nyumba ya Mtakatifu Marta. Baada ya salam fupi, Papa Francisko amewakilisha kwa washiriki wa mkutano huo, mjumbe mpya wa Baraza hilo la ushauri ambaye ni Kardinali Ambongo Besungu, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Kinshasa na baadaye wakaendelea kutoa baadhi ya michango ya mawazo kuhusiana na maisha ya Kanisa katika mabara tofauti, kwa namna ya pekee wakitazama hali halisi iliyopo ya kiafya.
Katibu wa Baraza la makardinali washauri wa Papa, ameweza kusoma kwa ufupi yatokanayo, katika hatua za mchakato wa Mswada mpya wa Katiba ya kitume na wakati huo huo uchunguzi, marekebisho na mapendekezo yaliyopokelewa kutoka Mabaraza ya kipapa yalishughulikiwa katika miezi ya hivi karibuni. Mkutano unaofuata umependekezwa kufanyika mwezi wa Februari 2021.