2020.11.01: SHEMASI WAPYA 13 WA CHUO KIKUU CHA KIPAPA URUBANIANA  WALIOPEWA DARAJA MIKONONI MWA KARDINALI TAGLE TAREHE  31 OKTOBA 2020 2020.11.01: SHEMASI WAPYA 13 WA CHUO KIKUU CHA KIPAPA URUBANIANA WALIOPEWA DARAJA MIKONONI MWA KARDINALI TAGLE TAREHE 31 OKTOBA 2020 

Kard.Tagle atoa daraja kwa mashemasi 13,kati yao ni shemasi Emil Sibomana wa Tanzania!

Kwa upande mmoja ninaweza kusema kuwa nimeumia kiasi kwa kitendo cha wazazi na ndugu wa karibu ambao wamekuwa wakitulea kutoweza kushiriki misa moja kwa moja.Kwa wengine walikuwa wana tiketi za kuja Roma na Visa lakini haikuwezekana sababu ya Corona.Lakini ninamshukuru Mungu Nimaneno ya shemasi mpya Emil Sibomana akihojiana na Vatican News baada ya daraja la ushemasi na wengine 12 mikononi mwa Kardinale.Tagle.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican & Shemasi Emil Nestory Sibomana -Urbaniana.

Ndugu Msikilizaji wa Vatican News, yafuatayo ni mahojiano na Vatican News na Shemasi mpya akielezea yaliyojiri siku ya tarehe 31 Oktoba 2020 wakati wa kupewa daraja la Ushemasi na wengine 12 mikononi mwa Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Baraza la Kipapa la Unjilishaji wa watu katika Chuo Kikuu cha Kipapa la Urbaniana Roma. Kwanza kabisa napenda kukupongeza na kumshukuru Mungu kwa makuu hayo aliyowatendea Shemasi mpya. Tarehe 31.10 ilikuwa siku kuu ya bikira Maria na mwisho wa mwezi wa kimisionari na Mama maría. Msikilizaji wetu wa Vatican News angependa kujua unaitwa nani na unatokea wapi na ulizaliwa wapi na historia yako kwa ufupi.

Naitwa EMIL NESTORY SIBOMANA. Ni mzaliwa wa Parokia ya Katumba katika Jimbo katoliki la Mpanda, Tanzania. Elimu ya msingi nilipata katika shule ya msingi Ivungwe-Katumba. Elimu ya sekondari: Kidato cha kwanza hadi cha nne nilisoma katika seminari ya Mtakatifu Yusufu Kaengesa iliyopo Jimbo katoliki la Sumbawanga. Kidato cha tano na cha sita nilisoma seminari ya Mtakatifu Yusufu Kilocha iliyopo Jimbo katoliki la Njombe. Mwaka 2012 nikajiunga na seminari kuu ya Mtakatifu Agostino Peramiho iliyopo Jimbo Kuu katoliki la Songea ambapo nilisoma masomo ya filosofia hadi mwaka 2015. Mwaka huo huo 2015 nikatumwa kwenda Roma kuendelea na masomo ya teologia katika Chuo Kikuu cha Urbaniana. Masomo hayo ya teologia nikahitimu mwaka 2018. Baada ya hapo nikaendelea ma masomo ya juu (“Masters”) katika maandiko matakatifu (Biblical theology) na kwa sasa nipo mwaka wa mwisho wa masomo hayo.

Ni hisia zipi ulikuwa nazo kabla ya kuanza maadhimisho na pia swali hilo linajieleza baada ya kupewa daraja la ushemasi. Kwa kweli siku ya kupewa daraja takatifu la ushemasi, nilikuwa naisubiri kwa hamu kubwa ukizingatia kuwa ilitakiwa iwe imeshafanyika tangu tarehe 1 Mei lakini haikuwezekana kwa sababu ya hili janga la ugonjwa wa Corona. Kwa hiyo ikawa imesogezwa mbele mpaka tarehe 31 Oktoba. Nilikuwa namuomba sana Mungu atujalie afya njema, hasa Kardinali Antonio Luis Tagle Rais wa Baraza la Kipapa la Unjilishaji wa Watu ambaye alikuwa anakuja kutupatia hilo daraja. Baada ya Misa kumalizika, furaha ilikuwa kubwa mno. Nikamwambia Mungu: asante kwa zawadi hii. Kwa kweli ninamshukuru sana Mungu kwa mambo makuu aliyonitendea.

Sisi tuliokuwa tunafuatilia kwenye njia za kidigitali tulionja yale maandalizi mazuri na mpangilio ulivyokuwa mzuri sana na wa kusisimua. Unamweleza nini msikilizaji wetu kuhusu maandalizi hayo hadi kufanikisha? Maandalizi yalikuwa makubwa sana. Kwa sababu ya ugonjwa huu wa Corona, tuliambiwa kuwa wazazi, ndugu na marafiki hawawezi kushiriki kwenye tukio hili. Kwa hiyo walezi, wanafunzi wenzetu wamekuwa wakijiandaa kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa sherehe inakuwa nzuri sana. Wanafunzi ndiyo wamehudumia katika misa: kuimba, kutumikia altareni; wanafunzi hao hao ndiyo wamefanikisha kurusha hewani adhimisho la Misa. Kwa kweli kazi wameifanya na tunawashukuru: Mungu awabariki sana.

Tukija katika mahubiri ya Kardinali Tagle rais wa Baraza la kipapa la uinjilishaji wa watu alikazia juu ya maana ya ushemasi kuwa ni kuhudumia na siyo ubwana na akawekea msisitizo wa tafadhali kama vile baba au mama anavyowabembeleza watoto wake wamsikilize kufuata nyayo njema ya Kristo  kuamua sasa  ...Ni kwa jinsi gani haya mafundisho yake yaliweza kukugusa binafsi? Mahubiri ya Kardinali yamenigusa mno. Na itabidi niwe nayasikiliza tena mara kwa mara maana naamini yatakuwa muongozo mzuri kwangu katika utume huu ambao Kanisa limenipatia. Kardinali amekazia kuhusu maana ya Ushemasi, kazi ambazo anatakiwa kufanya. Kiujumla ametusisitiza kuwa wahudumu wa Neno la Mungu na kuhudumia wengine na sio kuwa mabwana. Binafsi ninazidi kumwomba mwenyezi Mungu anijalie neema ya kuweza kutumikia vema katika shamba lake.

Niliona mliopewa ushemasi ni 13 kutoka bara la Afrika na Asia...unalielezeaje suala hili la miito ya Kanisa katika ulimwengu? Kwa hakika tuliopewa daraja la ushemasi tulikuwa 13: 3 kutoka Angola, 1 Kenya, 2 India, 1 Afrika Kusini, 3 Timor Est, 1 Ghana, 1 Pwani ya Pembe (Ivory Cost), 1 Tanzania. Kwa kuongezea, zaidi lakini hapa seminarini tupo wanafunzi kutoka nchi nyingi sana (nataja baadhi tu): China, Vietnam, Cameroon, Zimbabwe, Capo Verde, Burundi, Sudan na Sudan Kusini, Misri, Nigeria, Sir Lanka, Ethiopia, Afrika ya kati, Indonesia, madagascar, Iraq, Pakistan, Bangladesh, Congo na nyingine. Hivyo ni mchanganyiko mkubwa sana, na ambao kwa mtazamo wa haraka unaona kuwa unafunika ulimwengu mzima, ni kama kusema kuwa mikono ya Kristo inakumbatia mataifa yote, kwa kuthibitisha ukweli kwamba aliwatuma wafuasi wake kwenye mataifa yote kutangaza Injili. Ni wazi kabisa kwa mchanganyiko huu kuona utajiri mkubwa sana kwangu mimi kwani nazidi kujifunza tamaduni mbali mbali, ninajifunza pia changamoto na mafanikio kutoka nchi nyingine nje ya nchi yangu Tanzania. Na zaidi inaonyesha kuwa hata kwenye zile nchi ambazo hakuna uhuru mkubwa wa kuabudu, lakini bado wapo watu wanaojitoa, wanathubutu kwa maana ya kwamba wanahatarisha maisha yao na wanaingia seminarini kwenda kinyume na mantiki za ulimwengu huo wa ukandamizwaji. Kwa maana hiyo tuzidi kuombea miito mitakatifu, maana ni wazi kuwa shamba ni kubwa lakini bado watenda kazi ni wachache!

Kutokana na janga hili la covid-19  haikuwezekana ushiriki wa moja kwa moja wa ndugu na marafiki na zaidi sisi sote tulioko Italia na zaidi hapa Roma, je! unaliezeaje hili? Kwa upande mmoja ninaweza kusema kuwa nimeumia kiasi kwa kitendo cha wazazi na ndugu wa karibu ambao wamekuwa wakitulea kutoweza kushiriki misa moja kwa moja. Kwa bahati mbaya wengine walikuwa walishakata tiketi za kuja Roma na walikuwa wamepewa na Visa lakini haikuwezekana kuja kwa sababu ya ugonjwa huu wa Corona. Lakini yote tunamwachia Mungu. Kitu kikubwa kuliko vyote ni kupewa daraja! Tunamshukuru Mungu kwa zawadi hii aliyotupatia.

Ni kweli Mungu ndiyo ajuaye la muhimu ni uzima! Tushukuru Mungu. Hatimaye Shemasi wetu Emil, je unamweleza nini Askofu wako, wazazi, wanajimbo wako, na waamini wote wa Mungu kwa ujumla ambao wanakusikiliza? Kwanza kabisa napenda kutoa shukrani nyingi sana: Nawashukuru sana wazazi wangu: baba Nestory kilotsa na mama Beatrice Ndayisaba. Nawashukuru mababa wahashamu wote ambao nimepita mikononi mwao: Askofu Paschal Kikoti ambaye sasa ameshatangulia mbele ya haki: Apumzike, kwa amani na hasa katika mwezi huu wa Novemba kwa ajili ya marehemu, sala zangu zaidi ninazitoa kwa Mungu. Namshukuru Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga na namshukuru pia Askofu wangu wa sasa Eusebius Nzigilwa. Nawashukuru mapadre wote wa Jimbo katoliki la Mpanda, watawa, walezi na walimu wote walionifundisha, kaka zangu mafrateri, ndugu zangu na waumini wote wanaoendelea kunilea na kunisindikiza katika wito huu. Pili, nawaomba waendelee kuniombea.

Ndugu Msikilizaji wa Vatican News, hayo ndiyo mahojiano na Vatican News na Shemasi mpya EMIL NESTORY SIBOMANA wa Jimbo katoliki la Mpanda Tanzania, kwa sasa masomoni Roma, akielezea yaliyojiri siku ya tarehe 31 Oktoba 2020 wakati wa kupewa daraja la Ushemasi na wengine 12 mikononi mwa Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Baraza la Kipapa la Unjilishaji wa watu katika Chuo Kikuu cha Kipapa la Urbaniana Roma. Shukrani kwa ushuhuda huo na tuwaombee katika safari yao ya kuelekeza ukuhani mtakatifu!

SHEMASI EMILY SIBOMANA
01 November 2020, 16:00