Kardinali Parolin anasema, mkataba wa muda kati ya Vatican na China kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahali ni mchakato uliofanyiwa tafakari na sala ya kina na maamuzi yake yakapembuliwa na kutekelezwa. Kardinali Parolin anasema, mkataba wa muda kati ya Vatican na China kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahali ni mchakato uliofanyiwa tafakari na sala ya kina na maamuzi yake yakapembuliwa na kutekelezwa. 

Mkataba Kati ya Vatican Na China: Ni Tafakari, Sala Na Maamuzi Mazito

Kardinali Parolin: Uamuzi wa Vatican kuwekeana saini na Serikali ya China kuhusu uteuzi wa Maaskofu ni mchakato ambao, Papa ameufanyia tafakari ya kina na sala kwa muda mrefu! Matokeo yake yakapimwa na kupembuliwa na hatimaye, Papa kuamua kufanya maamuzi magumu, kielelezo cha uhuru wa ndani, ili kuendeleza majadiliano kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China, ulitiwa saini tarehe 22 Septemba 2018 kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia. Lengo la Vatican ni kuwapata wachungaji bora watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko akashuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi. Mkazo ni kuhusu shughuli za kichungaji na kitume, ili kuwawezesha waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato huu pamoja na mambo mengine unapania kukoleza: imani na matumaini; umoja na mshikamano wa kidugu. Uteuzi wa Maaskofu kwa ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya China ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini China na kwamba, huo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni.

Serikali ya China inatambua kunathamini dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki. Huo ni mwanzo wa amani na utulivu miongoni mwa watu wa Mungu nchini China. Kumbe, Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China hauna uhusiano na masuala ya kisiasa bali unajikita zaidi katika maisha na utume wa Kanisa nchini China, kama kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Itakumbukwa kwamba, Bwana Mike Pompeo, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani katika hotuba yake kwenye Kongamano la Uhuru wa Kidini ambalo lilipambwa na kauli mbiu “Kuendeleza na kulinda uhuru wa kidini kimataifa kwa njia ya diplomasia” katika hotuba yake aliitaka Vatican kutopyaisha tena Mkataba wake na Serikali ya China mintarafu uteuzi wa Maaskofu kwa sababu China ilikuwa inavunja sana haki ya uhuru wa kuabudu. Ikiwa kama Vatican itapyaisha Mkataba huo, kuna hatari ya Vatican kupoteza nguvu na uwezo wake wa kimaadili.

Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican amesema, wote wanajitahidi kutafuta uhuru wa kidini kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa nchini China linatekeleza dhamana na wajibu wake wa kutangaza na kushuhudia Injili katika hali ya amani na utulivu. Tofauti kubwa inayojitokeza hapa ni mbinu mkakati unaotumiwa na Vatican ili kuweza kufikia lengo hili msingi! Kardinali Parolin anakaza kusema, uamuzi wa Vatican kuwekeana saini na Serikali ya China kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia ni mchakato ambao, Baba Mtakatifu Francisko ameufanyia tafakari ya kina na sala kwa muda mrefu! Matokeo yake yakapimwa na kupembuliwa kwa kina na mapana na hatimaye, Baba Mtakatifu kuamua kufanya maamuzi magumu, kielelezo cha uhuru wa ndani, ili kuendeleza majadiliano kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, Mkataba huu utaendelea kufanya kazi bora zaidi, kuliko ulivyowekwa saini,  ili hatimaye, Kanisa liweze kuteuwa Maaskofu mahalia kwa ajili ya majimbo ambayo hadi sasa bado yako wazi! Lengo kuu ni utume na maisha ya Kanisa nchini China!

Vatican na China. Ok

 

09 October 2020, 16:25