Kard.Tagle:Wote tunaitwa kujua,kupenda na kutangaza Injili kwa kushuhudia!

Kardinali Antonio Tagle Rais wa Baraza la kipapa la Uinjilishaji wa Watu,na Rais wa Caritas Internationalis,ametoa ujumbe kwa njia ya video katika fursa ya siku ya Kimisionari ulimwenguni tarehe 18 Oktoba 2020.Akigusia ujumbe wa Papa kwa ajili ya Siku ya Kimisionari 2020, amesema,anatoa msaada wake kiroho na zana kwa wamisionari hivyo tunapaswa kuhisi kuwa sehemu ya mwendelezo wa kimisionari na kuunga mkono utume.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Katika Ujumbe wake kwa njia ya video katika fursa ya maadhimisho ya siku ya kimisionari ulimwenguni tarehe 18 Oktoba 2020, Kardinali Luis Antonio G. Tagle, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, na Rais wa Caritas Internationalis, amesema kuwa jitihada za umisionari kwa kila mbatizwa ni sehemu ya kujenga utambulisho wa kuwa  mwamini kamili na kwa maana hiyo "wote tunaitwa kujua, kupenda na kutangaza Injili wakati tunashuhudia  neno na matendo yetu ya dhati ya kutoa sadaka".

Akigusia kuhusu ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya Siku ya Kimisionari 2020, Kardinali Tagle amebainisha kwamba “ Papa kwa njia ya Shirika la Kipapa la shughuli za kimisionari (PMS), anatoa msaada wake kiroho na zana kwa wamisionari hivyo  wote tunapaswa kuhisi kuwa sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kimisionari kwa kushirikiana ili kuunga mkono kiuchumi katika utume wa kimisionari. Hata kama ulimwengu unapitiwa na changamoto za nguvu, lakini  utume unaendelea na mahali pale ambapo kuna mahitaji zaidi, wapo pia wamisionari na ambao wanahitaji msaada wetu”,  amehitimisha ujumbe wake kwa njia ya video Kardinali Tagle.

19 October 2020, 17:05