Tafuta

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari: Stella Maris: 1920 hadi 4 Oktoba 2020 kilele chake. Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari: Stella Maris: 1920 hadi 4 Oktoba 2020 kilele chake. 

Jubilei ya Miaka 100 Utume wa Bahari: 1920 Hadi 4 Oktoba 2020

Kardinali Peter Turkson katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari anapembua historia na hali ilivyo kwa sasa; changamoto mamboleo, nembo mpya, umuhimu wa kuyashirikisha Makanisa Mahalia; Mawasiliano, Sala, Wito pamoja na Sala ya Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari. Ilikuwa ni tarehe 17 Aprili 1922 Papa Pio XI alipoidhinisha Utume wa Bahari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris”. Katika kipindi cha miaka 100 kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika Utume wa Bahari kwa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati na kuendelea kujibu kilio cha mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao zinazoteseka na kunyanyasika kutokana na utume wao baharini! Pamoja na mambo mengine, Utume wa Bahari umeendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, mabaharia na wavuvi ambao wanajisadaka usiku na mchana ili kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi wanapata pia fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema Mama Kanisa anapenda kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbali mbali za dunia. Roho Mtakatifu na kwa maombezi ya Bikira Maria aendelee kupyaisha utume na huduma hii mintarafu mahitaji ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo.

Kwa muda wa mwaka mzima, Kanisa limejiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris” sanjari na Kongamano la 25 la Utume wa Bahari ambalo lilitarajiwa kuadhimishwa kuanzia tarehe 29 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba 2020, kama kilele cha Jubilei hii, huko mjini Glasgow, nchini Scotland. Huu ni utume ulioasisiwa na waamini walei ndani ya Kanisa kama sehemu ya mchango wao wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa tunu za Kiinjili. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika Waraka wake kama sehemu ya maadhimisho haya anasema, maadhimisho yote haya kwa sasa yanafanyika kwa njia ya mitandao ya kijamii kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Katika Waraka huu, Kardinali Turkson anapembua historia ya Utume wa Bahari na hali ilivyo kwa sasa; changamoto mamboleo, nembo mpya, umuhimu wa kuyashirikisha Makanisa Mahalia; Mawasiliano, Sala, Wito pamoja na Sala ya Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari. Ilikuwa ni tarehe 17 Aprili 1922 Papa Pio XI alipoidhinisha Utume wa Bahari. Leo hii kuna umati mkubwa wa Mapadre wanaowahudumia mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Kuna jeshi kubwa la watu wanaojitolea zaidi kuwahudumia mabaharia na wavuvi katika bandari 300 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka. Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji, kwa kuwafunulia watu sura pendelevu ya Mama Kanisa kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu wa Mungu na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.

Miaka 100 iliyopita, kimekuwa ni kipindi cha ujenzi wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na mataifa mbalimbali. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa Utume wa Bahari. Lakini vitendo vya kiharamia, uhalifu wa magenge, tatizo la kutua nanga mbali na bandari, kutengwa na kutelekezwa na kwa sasa athari za janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Gonjwa hili limepelekea wavuvi na mabaharia wengi kukumbwa na ugonjwa wa sonona. Kanisa katika kipindi hiki pia limejitahidi kusoma alama za nyakati, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wavuvi, mabaharia na famulia zao. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari, nembo imebadilishwa, ili kutoa utambulisho wa Utume wa Bahari kama nanga ya matumaini, kielelezo cha imani na wokovu na upendo kwa wote. Mwanga wa Kristo unafyekelea mbali ukosefu wa haki, dhuluma na nyanyaso na kwamba, hata wavuvi na mabaharia wanahamasishwa kutunza na kulinda mazingira nyumba ya wote.

Makanisa mahalia yanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika Utume wa Bahari, ili kuwasaidia wavuvi na mabaharia kutekeleza dhamana na wajibu wao, na hatimaye, waweze kuwa watakatifu. Huu ni utume wa uwepo kati pamoja na wavuvi na mabaharia. Wasindikizwe kwa sala na sadaka za majirani zao. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 bado linaendelea kusababisha madhara makubwa kwa wavuvi na mabaharia. Kumbe, kuna haja ya kujizatiti katika utekelezaji wa mkataba kuhusu sheria ya bahari, MLC. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anahitimisha Waraka wake kwa Sala ya Jubilei ya Miaka 100 kwa Bikira Maria, Nyota ya Bahari.

Utume wa Bahari
02 October 2020, 15:15