Askofu mkuu Giovanni Gaspari, Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tomè na Principè: Dhamana na utume wa Balozi wa Vatican kwa Makanisa mahalia! Askofu mkuu Giovanni Gaspari, Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tomè na Principè: Dhamana na utume wa Balozi wa Vatican kwa Makanisa mahalia! 

Dhamana na Utume wa Balozi wa Vatican Kwa Kanisa Mahalia!

Askofu mkuu Giovanni Gaspari, alizaliwa tarehe 6 Juni 1963 Jimbo kuu la Pescara, Italia. Tarehe 4 Julai 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Jimbo kuu la Pescara likampatia nafasi ya kujiendeleza zaidi na masomo kiasi cha kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa na Shahada ya Uzamili katika Maadili. Tarehe 1 Julai 2001 akaanza utume wa diplomasia ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 17 Oktoba 2020 amemweka wakfu Askofu mkuu Giovanni Gaspari, Balozi wa Vatican nchini Angola, São Tomé na Príncipe, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin alikazia zaidi kuhusu huduma kwa Mungu na jirani kama chemchemi ya furaha na matumaini; Udhaifu wa binadamu, neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maaskofu wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Wajibu na dhamana ya Balozi wa Vatican kwa Makanisa mahalia pamoja na historia ya maisha na utume wa Askofu mkuu Giovanni Gaspari.

Kardinali Parolin anasema, Kristo Yesu kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, aliwaelezea Mitume wake maana ya uongozi katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Aliwakumbusha Mitume wake kwamba: “Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa. Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa.” Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane. Hivyo, Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkubwa kati yenu, sharti awe mtumishi wenu. Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote. Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.” Rej. Mk. 10:35-52.

Kristo Yesu, Neno wa Mungu alijinyenyekesha, akatwaa mwili na kuzaliwa kati ya binadamu! Akawa mtumishi na mtii, hata mauti ya Msalaba, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma kwa Mungu na jirani, chemchemi ya furaha na matumaini kwa wafuasi wake. Kwa kufuata na kuiga mtindo wa maisha na utume wa Kristo Yesu, hata wafuasi wake nao wanaweza kujivika fadhila ya upendo na kutawala pamoja na Kristo Yesu. Uongozi unapaswa kufahamika kuwa ni chombo cha huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wakipewa kipaumbele cha kwanza! Kristo Yesu amekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika masuala ya uongozi. Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu wanaona kwamba, uongozi ni “kichaka” cha kujineemesha na kujipatia utajiri wa haraka haraka pamoja na kutukuzwa na watu.

Kristo Yesu kwa kutambua udhaifu, changamoto na matatizo wanayoweza wafuasi wake kukumbana nayo katika hija ya maisha yao, akawakirimia neema na baraka, kwa ajili ya huduma kwa Mungu, Kanisa na Maskini. Alijifanya mnyonge, ili kuwakirimia nguvu wafuasi wake, akateswa na kutundikwa Msalabani, ili kwa njia ya ngazi ya Msalaba, hata wafuasi wake waweze kukwaa kwenda mbinguni, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Ignasi wa Antiokia, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu wanawekwa wakfu kwa ajili ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, kumbe, wanapaswa kuyatangaza na kuyashuhudia maneno ya Kristo Yesu kama kielelezo cha imani tendaji, tayari kuwatumikia watu wa Mungu kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Watambue kwamba, wameteuliwa kati ya watu na kuwekwa wakfu kwa ajili ya mambo ya Mungu. Uaskofu ni jina na kielelezo cha huduma kwa wote, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Daraja ya Uaskofu ni huduma ya upendo na umoja kama anavyosema Mtakatifu Paulo VI.

Askofu mkuu Giovanni Gaspari, Balozi wa Vatican nchini Angola, São Tomé na Príncipe, ameitwa na kutumwa kutekeleza dhamana na wajibu huu kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa Makanisa mahalia. Kumbe, anapaswa kutimiza wajibu huu kwa moyo wa furaha, imani na matumaini, daima akiendelea kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Awe ni daraja kati ya Kanisa mahalia na Baba Mtakatifu, kwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wote. Balozi wa Vatican anapaswa kuwa ni chombo cha amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaoheshimu uhuru wa kuabudu pamoja na ujenzi wa jamii inayosimikwa katika sera na mikakati ya uchumi fungamani; usawa na haki kwa wote, kila mtu akipewa nafasi ya kuweza kupata utimilifu katika maisha yake.

Kama mwakilishi wa Kanisa, Balozi wa Vatican anapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha ujenzi wa amani kati ya Mataifa kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi. Hii ni huduma inayoboreshwa kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu, Kufunga na Kusali. Askofu mkuu Giovanni Gaspari, Balozi wa Vatican nchini Angola, São Tomé na Príncipe alizaliwa tarehe 6 Juni 1963 Jimbo kuu la Pescara, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 4 Julai 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Jimbo kuu la Pescara likampatia nafasi ya kujiendeleza zaidi na masomo kiasi cha kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa na Shahada ya Uzamili katika Maadili.

Ilikuwa ni tarehe 1 Julai 2001 Askofu mkuu Giovanni Gaspari alipojiunga na diplomasia ya Kanisa na hatimaye, akatumwa nchini Iran, Albania, Mexico, Lithuania na hatimaye, kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Tarehe 21 Septemba 2020, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu na Balozi wa wa Vatican nchini Angola, São Tomé na Príncipe na kuwekwa wakfu tarehe 17 Oktoba 2020. Barani Afrika anatumwa kukoleza ari na moyo wa majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Daraja: Uaskofu

 

 

21 October 2020, 07:28