Maandamano ya kupinga nchini Belarus Maandamano ya kupinga nchini Belarus 

Vatican:Ask.Mkuu Gallagher yuko Minsk kuonesha ukaribu wa Papa

Ni wiki nyingi sasa huko Belarus wanapitia kipindi kigumu cha mivutano,rais Lukashenko anapingwa vikali na wapinzani wake ambao hawakubaliani na ushindi huo katika uchaguzi uliopita.Katika hali hiyo,unafikia hata ujumbe huko Minsk wa Askofu Mkuu Gallagher,Katibu wa Vatican,wa mahusiano na ushirikiano wa kimataifa kuunga mkono Kanisa Katoliki na Nchi akionesha umakini wa ubaba wa Papa Francisko.

Na Sr. Angela Rwezaula -Vatican

Papa Francisko anatazama kwa umakini hali halisi iliyo chanya na hasi ya ulimwengu huu. Umuhimu wa mtazamo wake katika siku hizi pia unaitazama  nchi ya Belarus, ambayo imekuwa uwanja mkubwa wa machungu kwa siku hizi kati ya Rais Lukashenko na wapinzani wake. Kwa upande wa Umoja wa Ulaya wametoa wito kwa sehemu zote mbili kufungua mazungumzo. Tarehe 11 Septemba 2020, Katibu wa Vatican wa mahusiano na ushirikiano wa kimataifa, Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, amekwenda nchini Jamhuri ya Belarus ili kuunga mkono umakini na ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Kanisa Katoliki na ndani ya Nchi kwa ujumla. Hili ni jambo muhimu la kutia moyo katika kipindi hiki chenye safu za matatizo mengi. Ratiba ya ziara ya Askofu Mkuu Gallagher inatazamia kukutana na viongozi wa mamlaka ya nchi na wahusika wakuu wa Kanisa Katoliki nchini humo.

Papa Francisko anaomba mazungumzo na haki kwa  ajili ya Belarus

Papa Francisko hajaacha kamwe kuomba amani kwa Mungu kwa ajili ya ulimwengu wote. Na kwa maana hiyo hata katika salamu kwa waamini ambao walimsindikiza katika Sala ya Malaika wa Bwana, kunako tarehe 16 Agosti iliyopita mawazo yaliwaendea watu wa nchi ya Belarus. Papa Francisko alisisitiza kwa namna ya pekee hali ya kisiasa na kijamii katika nchi hiyo pendwa na kuwakabidhi watu wa Mungu wa nchi hiyo chini  ya uliniz wake Bikira Maria.

“ Ninafuatilia kwa umakini hali halisi, baada ya uchaguzi na hivyo ninatoa wito kuwa na mazungumzo na kukataa vurugu na kuheshimu haki na sheria. Ninawakabidhi wanachi  wote wa Belarus chini ya ulinzi wa Mama, Regina wa amani”.

Sala ya waamini kuombea nchi ya Belarus ili haki na amani vitawale

Siku zilizofuata tarehe 18 Agosti 2020 mbele ya hali halisi hiyo ngumu, Kamati Tendaji ya haki na amani ya Ulaya iliwaalika wakristo wote kuungana pamoja katika sala ya ‘Baba Yetu’ kwa ajili ya watu wa Belarus  ili ukweli, haki na amani vitawale. Hata hivyo Lukashenko anasema haondoki ng'o madarakani. Maandamano makali yanaendelea hata Dominika  tarehe 13 Septemba huko Minsk, maelfu ya watu watashuka tena katika viwanja. Maandamano hayo kwa mujibu wa viongozi wapinzani itakuwa ni kwa ajili ya Maria Kolesnikova, kiongozi wa upinzaji aliyekatwa siku zilizopitwa. Siku zijazo Kiongozi wa nchi Lukashenko atakuwa huko Sochi, nchini Urusi ili kukutana na Rais wa nchi hiyo Putin.

Vizuizi vya kuingia nchini Belarus Askofu Kondrusiewicz

Kwa mujibu wa taarifa zinasema kwamba  inawezekana Askofu Mkuu Gallagher hasiweze kukutana na Askofu  Mkuu Tadeusz Kondrusiewicz wa Minsk, ambaye tangu tarehe 31 Agosti yupo nchini Poland, mahali alipokwenda kuudhuria Misa ya siku kuu ya Bikira Maria wa Częstochowa na kwa sababu ya vizuizi alivyowekewa  na mamlaka ya Belarus kubaki Poland.

“Katika hali ya mgogoro wa kijamii na kisiasa uliopo katika nchi yetu ninaendelea kuomba pawepo mazungumzo na mapatano. Sitaki kabisa kuwa maamuzi yasiyo ya haki na yasiyo ya kisheria katika huduma ya mipakani iongezee mivutano katika nchi yetu”, ameandika Askofu Kondrusiewicz.

Akizungumzia juu ya kukosa uwezekano wa kutimiza wajibu wake wa kichungaji kwa sababu ya vizuizi vya kuingia nchini mwake, Askofu Kondrusiewicz amewageukia waamini wa jimbo lake Kuu akiomba wasali kwa ajili ya kuweza kurudi haraka iwezekanavyo katika nchi yake Belarus.

12 September 2020, 09:20