Uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni sehemu ya vinasaba vya utu, heshima na haki msingi za binadamu kama vinavyofafanuliwa na Baba wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni sehemu ya vinasaba vya utu, heshima na haki msingi za binadamu kama vinavyofafanuliwa na Baba wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.  Tahariri

Uhuru wa Kidini Ni Sehemu ya Utu, Heshima Na Haki za Binadamu

Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. (Rej. DH, namba 2). Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika makala yake kuhusu mchango wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kuhusu uhuru wa dini anasema, Mtakatifu Paulo VI alichangia sana katika maboresho na hatimaye tamko kuhusu Uhuru wa Kidini ambao alitoa ufupisho wake kwa kusema, “Nemo cogatur, nemo impediatur” yaani katika mambo ya dini hakuna mtu anayepaswa kuzuiliwa wala kulazimishwa”.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walionesha wasi wasi kuhusu tamko hili na wakataka lipitishwe bila kupigiwa kura. Lakini, Papa Paulo VI katika busara yake ya kichungaji akawasihi Mababa wa Mtaguso kulipigia kura na likapitishwa kwa kishindo kama msimamo wa Kanisa kuhusu uhuru wa kidini. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. (Rej. DH. n.1). Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Tamko hili lilikuwa na maana sana katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Kunako mwaka 1965, Mtakatifu Paulo VI akafanya hija ya kwanza ya kitume kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, huko New York, Marekani. Akatumia fursa hii kuzungumzia kuhusu uhuru wa dini na umuhimu wa Serikali mbali mbali kuhakikisha kwamba, zinalinda na kudumisha uhuru huu. Dr. Andrea Tornielli, anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 7 Desemba 1995 kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 30 tangu kuchapishwa Tamko la “Dignitatis Humanae”, alitumia fursa hii, kwa mara nyingine tena kukazia uhuru wa dini sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni sehemu ya utume wa Kanisa wa kuendeleza mchakato wa majadiliano kati ya Kanisa na Ulimwengu kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uhuru wa kidini unafumbatwa katika misingi ya ukweli na haki na kwamba, uhuru wa kidini ni kati ya changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga katika ulimwengu mamboleo. Tamko hili ni amana na utajiri wa Mama Kanisa, mintarafu wajibu wake wa kimaadili, ulioisaidia Jumuiya ya Kimataifa kufanya mageuzi makubwa katika masuala ya kisiasa, kijamii sanjari na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa.

Waamini walei wana wajibika kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, upendo na amani. Kwa maana, kama vile ilivyo lazima kukubali ya kwamba mji wa kidunia, hushughulikiao kwa haki mambo ya kidunia, huongozwa na kanuni zake, vivyo hivyo hukataliwa kwa haki mafundisho yale mabaya yatakayo kuijenga jamii bila kuijali dini na kuupinga uhuru wa dini wa raia na kutaka kuuangamiza. (Rej. LG. N- 36). Uhuru wa dini ni dhana inayoweza kusaidia kukuza demokrasia kwa kuzingatia tunu msingi zinazofumbatwa katika imani. Mama Kanisa anawahimiza watoto wake kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kamwe waamini wa dini mbali mbali wasitumbukie katika mchakato wa dhana ya wongofu wa shuruti. Dhamiri nyofu ni mahali patakatifu sana katika maisha ya mwanadamu, mahali ambapo sheria ya Mungu imeandikwa katika moyo wa mwanadamu.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, tarehe 22 Desemba 2005 katika salam na matashi mema kwa ajili ya Sherehe za Noeli, aligusia amana na utajiri mkubwa ulioachwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wa Kanisa, lakini pia kumbukumbu ya miaka 40 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko Kuhusu Uhuru wa Dini, nguzo msingi kwa ajili ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tamko hili lilipyaisha Mafundisho ya Kanisa na linapaswa kuheshimiwa na wote. Waamini wajitaabishe kujisomea yale yaliyoandikwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kuhusu Uhuru wa Dini, ili kuendelea kuwa waaminifu, kwa kusoma alama za nyakati na hatimaye, kusonga mbele, kwa ajili ya kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mama Kanisa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuzama zaidi katika: Mafundisho Jamii ya Kanisa, Maandiko Matakatifu; Uhusiano kati ya Imani na Sayansi; Kanisa na Sayansi; pamoja na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa jamii stahimilivu.  

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, anaendelea kufafanua kwamba wafiadini na waungama imani wa Kanisa la Mwanzo, waliyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Wengi wao wameuwawa kutokana na chuki za kidini, uhuru wa dhamiri nyofu na imani yao kwa Kristo Yesu. Mama Kanisa kwa kutambua dhamana na wajibu wake wa kimisionari, hana budi kujifunga kibwebwe kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa imani; ili hatimaye, kuimarisha: utambulisho na mafungamano ya kitamaduni, umoja na amani kati ya watu wa Mataifa. Dr. Andrea Tornielli, anahitimisha makala yake kwa kusema, Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anakazia uhuru wa dini kwa kusema kwamba huu ni msingi wa: ustawi, maendeleo ya wengi na mafungamano ya kijamii. Kutokana na umuhimu wake, Vatican imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha uhuru wa kidini katika medani za Jumuiya ya Kimataifa, kwa kukemea vikali misimamo mikali ya kidini ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa kwa watu wasiokuwa na hatia sanjari na kuvuruga mchakato wa demokrasia ya kweli. Kanisa lina haki ya kushiriki katika maisha ya hadhara kwani linapania kumhudumia mwanadamu mzima: kiroho na kimwili. Akili ya mwanadamu inatambua uhuru wa dini kama sehemu ya haki msingi za binadamu, inayofumbata, utu na heshima yake. Uhuru wa kidini unapaswa kushuhudiwa katika maisha ya faragha na yale ya hadharani. Hii ni changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Uhuru wa dini ni nguzo ya haki msingi za binadamu; ni kiiini cha Habari Njema ya Wokovu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Uhuru wa kuabudu na kidini unaweza kusaidia kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Hii ni chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na kwamba, ukweli na uwazi ni kanuni msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Kuna baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaotaka kuzima uhuru wa kuabudu au kung’oa kabisa uhuru wa kidini kutoka katika masuala ya kisiasa na matokeo yake ni kuibuka kwa kasi kubwa chuki dhidi ya imani, dhuluma na nyanyaso za kidini. Waamini wa dini mbali mbali duniani wanapaswa kuunganisha sauti zao ili kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu; kwa kujikita katika kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wajenge madaraja ya majadiliano ya kidini kwa kuheshimiana, kwani tofauti zao msingi ni kadiri ya mapenzi ya Mungu na kamwe, zisiwe ni sababu ya chokochoko, uhasama na chuki za kidini, ambazo zimekuwa ni sababu kubwa ya maafa na majanga katika maisha ya watu wengi duniani!  

Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii.

Utu wa Binadamu
21 September 2020, 15:54