Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 27 Septemba inaadhimisha Siku ya Utalii Duniani na Kauli mbiu ya Mwaka 2020 ni "Utalii na Maendeleo Vijijini" Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 27 Septemba inaadhimisha Siku ya Utalii Duniani na Kauli mbiu ya Mwaka 2020 ni "Utalii na Maendeleo Vijijini" 

Siku ya Utalii Duniani 27 Sept. 2020: Utalii na Maendeleo Vijijini

Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Utalii Duniani kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Utalii na Maendeleo Vijijini”. Maadhimisho haya yanafanyika wakati ambapo janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 linaendelea kuleta majanga makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Utalii ni kati ya sekta ambazo zimeathirika sana na COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (World Tourism Organization, UNWTO) lilianzishwa tarehe 1 Novemba 1974. Ni wakala maalum wa Umoja wa Mataifa wenye majukumu ya kukuza uwajibikaji, maendeleo na upatikanaji wa utalii. Ni shirika linaloongoza duniani kwenye sekta ya utalii na linapania kukuza utalii kama nyenzo ya kukua kwa uchumi, maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na mazingira endelevu. Pia linatoa uongozi na msaada wa kisekta katika kukuza maarifa na sera za utalii duniani. Linahamasisha utekelezaji wa kanuni za kimataifa za maadili ya utalii. Ili kuongeza mchango wa utalii katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii huku likipunguza athari hasi za utalii, pia kuwezesha utalii kama chombo cha kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Sustainable Development Goals), ili kupambana na umaskini na kukuza mchakato wa kukuza na kudumisha amani duniani. Tangu tarehe 27 Septemba 1980, Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 27 Septemba inaadhimisha Siku ya Utalii Duniani, kama kumbukumbu endelevu ya kuridhiwa kwa itifaki ya kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (World Tourism Organization, UNWTO).

Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Utalii Duniani kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Utalii na Maendeleo Vijijini”. Maadhimisho haya yanafanyika wakati ambapo janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 linaendelea kuleta majanga makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Utalii ni kati ya sekta ambazo zimeathirika sana kutoka na gonjwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Usafiri wa anga ulisitishwa, mipaka ikafungwa, watu wakalazika kukaa karantini. Wadau wa sekta ya utalii, wakaathirika sana. Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani zinaonesha kwamba, utalii kwa kipindi cha mwaka 2020 umepungua kwa kiasi cha watalii bilioni moja na hivyo kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kupoteza kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 1, 200, sanjari na upotevu mkubwa wa nafasi za kazi. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuitia shime Jumuiya ya Kimataifa kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kuanza upya, kwani si rahisi sana kurejesha mambo kama yalivyokuwa kabla ya ugonjwa Virusi vya Corona, COVID-19.

Hii ni sehemu ya ujumbe uliotolewa na Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani. Ujumbe wa mwaka huu uliokuwa umechaguliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (World Tourism Organization, UNWTO), ulionesha mchango mkubwa ambao ungeweza kutolewa na sekta ya utalii katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kujielekeza zaidi vijijini. Lengo ni kukuza na kudumisha utalii fungamani na unaowajibisha kwa kuzingatia kanuni ya haki jamii, uchumi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hapa mkazo unawekwa katika kutunza tamaduni za watu mahalia, kutambua na kuthamani Jumuiya mahalia na haki yake ya kuwa mdau katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu na uwajibikaji wa kijamii katika eneo husika. Kumbe, huu ni utalii unaochangia mwingiliano na mafungamano kati ya sekta ya utalii, Jumuiya mahalia pamoja na watalii wenyewe.

Mfumo huu ni muhimu sana katika kukuza pia sekta ya kilimo, kwa kuwawezesha hata wakulima wadogo wadogo kuchangia katika uzalishaji wa chakula. Kilimo na utalii vijijini vinaweza kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuheshimu na kuzingatia ekolojia kwa kuendelea kujikita katika mshikamano na udugu wa kibinadamu, sanjari na kuibua mitindo mipya ya maisha. Sekta ya utalii na kilimo vinaweza kusaidia kuibua utamaduni mpya; kwa kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya binadamu; kwa kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote. Hili ni hitaji msingi la kimaadili na dharura inayohitaji utekelezaji wa pamoja. Utalii Vijijini ni fursa ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na jirani pamoja na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote kwa kuondokana na kishawishi cha mabadiliko makubwa yanayoweza kuwa ni sababu ya hofu na wasi wasi. Utalii ukuze na kujenga ujirani mwema, usaidie watu kutembeleana ili kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu kati ya watu wa Mataifa. Katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19 utalii unaowajibisha na fungamani ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya umaskini ambao umeongezeka maradufu kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19.

Kanisa linapenda kuonesha uwepo wake wa karibu na mshikamano kwa wadau wa sekta ya utalii duniani. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anawahimiza wadau mbalimbali katika sekta ya utalii, kuhamasisha utalii unaowajibisha, kwa kuzingatia kanuni ya hakijamii na uchumi fungamani; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuheshimu tamaduni za watu mahalia. Utalii vijijini upewe msukumo wa pekee, kwa kuwahusisha wanavijiji katika mchakato wa maamuzi mbalimbali bila kusahau maboresho ya ujira kwa wafanyakazi mahalia. Mwaliko unatolewa kwa wanaharakati wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kusaidia kuragibisha wongofu wa kiekolojia; kwa kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kuendeleza uchumi fungamani unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, pamoja na kuwajengea uweazo wa kiuchumi wakulima wadogo wadogo. Makanisa mahalia yasaidie kukuza utalii vijijini; wananchi wasaidie wafanyakazi katika sekta ya utalii ambao kwa wakati huu wanakabiliana na hali ngumu ya maisha, sanjari na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira.

Utalii Duniani
25 September 2020, 16:02