Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 3 Septemba 2020 amemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Lebanon kama kielelezo cha mshikamano na wananchi wa Lebanon. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 3 Septemba 2020 amemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Lebanon kama kielelezo cha mshikamano na wananchi wa Lebanon.  (ANSA)

Siku ya Kufunga Na Kusali kwa Ajili ya Lebanon: Amani na Utulivu

Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu wa Mungu Lebanon katika ujumla wao, wawe ni mashuhuda wa haki, amani na maridhiano, tayari kusimama kidete kulinda ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga utamaduni wa watu kukutana; kwa kuishi katika hali ya amani, utulivu na udugu wa kibinadamu; chachu muhimu sana katika mchakato wa upyaisho wa mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi tarehe 3 Septemba 2020 amewasili Beirut nchini Lebanon na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Harissa kama kielelezo cha uwepo na mshikamano wa upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wananchi wa Lebanon wameguswa na kutikiswa sana na mlipuko wa Beirut ambao umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Huu ni wakati wa kuanza upya kwa ujasiri, ari na moyo mkuu. Katika kipindi hiki kigumu, watu wa Mungu waimarishwe kwa nguvu ya imani na sala, daima wakiendelea kupyaisha ndoto ya nchi yao inayopendeza kwa kujikita katika ustawi na maendeleo fungamani ya wananchi wake.

Watu wa Mungu katika ujumla wao, wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano, tayari kusimama kidete kulinda ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga utamaduni wa watu kukutana; kwa kuishi katika hali ya amani, utulivu na udugu wa kibinadamu; chachu muhimu sana katika mchakato wa upyaisho wa mafao ya wengi. Ni katika hali na mazingira kama haya, wataweza kuwa na uhakika wa mwendelezo wa uwepo wa Ukristo pamoja na mchango wa Lebanon katika Nchi za Kiarabu na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Udugu wa kibinadamu ni utambulisho wa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Lebanon. Ni katika muktadha huu Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 kufunga na kusali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon.

Mlipuko wa Beirut uliojitokeza hapo tarehe 4 Agosti 2020 umesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Tangu wakati huo, Baba Mtakatifu amekuwa akiyaelekeza mawazo na maneno yake nchini Lebanon, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo. Anaendelea kutoa hamasa kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa ukarabati wa Lebanon, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Hata katika hali ya kukata tamaa, bado watu wa Mungu nchini Lebanon wanaweza kushusha nyavu zao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu. Kwa imani, sala na matumaini, yote yanawezekana anasema Kardinali Pietro Parolin. Umoja na mshikamano wa kitaifa ni chachu muhimu sana ya ujenzi wa Lebanon, dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia misingi ya: haki, ukweli na uwazi; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kard. Parolin: Misa
05 September 2020, 08:36