Tafuta

Papa Francisko ameonesha mshikamano wa dhati na familia ya Mungu nchini Belarus katika kipindi hiki cha machafuko ya kisiasa baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Papa Francisko ameonesha mshikamano wa dhati na familia ya Mungu nchini Belarus katika kipindi hiki cha machafuko ya kisiasa baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. 

Mshikamano wa Papa Francisko na Wananchi wa Belarus! Amani!

Katika mazungumzo yao, wamegusia kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika medani za kimataifa; mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo. Wamekubaliana kimsingi kwamba, Kanisa Katoliki linaweza kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha ya kiroho kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Belarus.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Agosti 2020, alisikika akisema kwamba, anafuatilia kwa wasi wasi mkubwa hali tete ya kisiasa nchini Belarus, baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo tarehe 9 Agosti 2020 na kumpatia ushindi Rais Alyaksandr Ryhoravich Lukashenka, ambaye amekuwa madarakani tangu tarehe 20 Julai 1995. Amebahatika kuongoza Belarus kwa miaka zaidi ya ishirini na mitano! Baba Mtakatifu alitumia fursa hii, kuwaalika wadau wote wanaohusika na machafuko ya kisiasa nchini humo, kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi sanjari na kukataa katu katu kishawishi cha kutaka kutumia nguvu na badala yake, wasimamie sheria, haki na wajibu. Baba Mtakatifu aliwaweka watu wote wa Mungu nchini Belarus chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican, kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 14 Septemba 2020 ameongoza ujumbe wa Vatican kwenda nchini Belarus na huko akafanikiwa kukutana na Bwana Vladimir Makei, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Belarus. Katika mazungumzo yao, wamegusia kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika medani za kimataifa; mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo. Wamekubaliana kimsingi kwamba, Kanisa Katoliki linaweza kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha ya kiroho kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Belarus.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Belarus. Kwa pamoja wametambua changamoto wanazokabiliana nazo Maaskofu Katoliki nchini Belarus. Askofu mkuu Gallagher amependa kuwahakikishia uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha, utume na changamoto wanazokabiliana nazo. Maaskofu wamejadiliana na kupembua kwa kina na mapana hija ya maisha na utume wa Kanisa nchini Belarus, ambalo linapaswa kuendelea kubaki imara na aminifu, kwa utambulisho, amana, utajiri na utume wake wa Kiinjili, ili kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kitaifa. Ujumbe wa Vatican nchini Belarus, umekazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kusimama kidete, kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili baada ya nchi hii kutawaliwa kwa muda mrefu na sera za Kikomunisti.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher alipata pia fursa ya kukutana na kuzungumza na Bwana Sergei Aleinik, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia ni Balozi wa Belarus mjini Vatican. Viongozi hawa wawili wamejadiliana kuhusu masuala tete ya Kimataifa na hali ilivyo kwa wakati huu. Ujumbe wa Vatican nchini Belarus ulipata nafasi ya kushiriki katika Ibada mbalimbali pamoja na kutembelea Madhabahu ya Watakatifu wa Belarus na hapo wakapa fursa ya kuweza kujifunza zaidi historia, amana na utajiri wa watu wa Mungu nchini Belarus. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher na ujumbe wake, walirejea tena mjini Vatican tarehe 14 septemba 2020.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Belarus, limeitaka Serikali kuacha mara moja kutumia nguvu kupita kiasi, hali inayopelekea watu wengi kupoteza maisha, kupata vilema vya kudumu na wengi wao kuishia magerezani. Mashambulizi yote haya dhidi ya watu wasiokuwa na hatia hayana mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Belarus. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Serikali inaunda mazingira ya majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo, haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Belarus. Baraza la Maaskofu Katoliki Belarus linasikitika kusema kwamba, matumizi ya nguvu kubwa dhidi ya raia yamejenga kinzani kubwa kati ya wananchi na vikosi vya ulinzi na usalama.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Tadeusz Kondrusiewicz, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Belarus, anawataka viongozi wa Serikali na wanasiasa kusimamia ukweli utakaowaweka huru na kamwe watu wa Mungu nchini Belarus hawatakubali kusadaka ukweli kwa ajili ya mafao ya wanasiasa na viongozi wanaotaka kutumia fursa hii ya hali tete ya kisiasa kwa ajili ya mafao binafsi. Vikosi vya ulinzi na usalama kufanya mauaji ya kinyama, kuwakamata na kuwaweka watu kizuizini bila hatia, kwa vile tu wanataka kufahamu ukweli ni dhambi kubwa na ukosefu wa maadili ya uongozi bora. Ni hatari sana kuvuruga misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii, kwani madhara yake ni makubwa hata kwa vizazi vijavyo.

Papa: Elimu

 

 

 

16 September 2020, 15:49