2020.09.11 Maria Luigia wa Ekaristi Takatifu ametangazwa mwenyeheri tarehe 26 Septemba 2020 huko Napoli,Italia 2020.09.11 Maria Luigia wa Ekaristi Takatifu ametangazwa mwenyeheri tarehe 26 Septemba 2020 huko Napoli,Italia 

Maria Luigia wa Ekaristi Takatifu ni mwenyeheri na mtawa Mtakatifu!

Tarehe 26 Septemba 2020 ametangazwa huko Napoli,Italia mwenye heri Maria Luigia Pascale wa Ekaristi Takatifu,Mnyenyekevu na mwanzilishi wa Shirika la Watawa Waabuduo Msalaba Mtakatifu.Mwakilishi wa Pa pa alikuwa ni Kardinali Crescenzio Sepe Askofu Mkuu wa Napoli.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Kwa unyenyekevu mkubwa na katika usiri wa maisha yafananayo na kifo; ndivyo Maria Lugia Pascale wa Ekaristi Takatifu alivyopambanua fumbo ambalo bado linatambulika katika ukuu wake na uzuri wake lililompelekea kuheshimika kwa Kanisa zima la Napoli. Ni mwanamke ambaye kwa changamoto za wakati wake alizijibu kwa usahihi na kuzigeuza kuwa fursa huku zikimsaidia kuzama katika tafakari na maisha ya sala na ibada ya kuabudu kwa Yesu wa Ekaristi.

Kardinali Crescenzio Sepe Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki Napoli amemwakilisha Papa katika maadhimisho ya tukio kutangazwa mwenyeheri Maria Lugia Pascale wa Ekaristi Takatifu, tarehe 26 Septemba 2020. Katika kuelezea wasifu wake  amekazia kuwa utakatifu una sura nyingi kama umbo lenye pembe nyingi, lakini kitu cha muhimu katika utakatifu ni kujua kupenda na kuwapokea wengine. Aidha, utii ni tunu iliyofunuliwa tangu awali mwa Maisha ya mwenyeheri Maria velotti. Pamoja na kupitia changamoto za mateso katika makuzi yake Maria Velotti alihimili mikiki mikiki hiyo huku akikua na kukomaa katika msamaha na upendo. Magumu mengi aliyoyapitia yalikuwa nyenzo ya kukuza uwezo wa kutii na karama za maisha ya kiroho akielewa thamani na nafasi ya mateso katika kumfuasa Kristo na hivyo ikawa rahisi kujitolea kikamilifu kwa Mungu.

Sr. Maria Luigia wa Ekaristi Takatifu
Sr. Maria Luigia wa Ekaristi Takatifu

Mwenye heri Maria Velotti alikuwa Mtawa wa mtindo wa kifranciskani aliyeweza kujiweka wakfu kikamilifu kwa Bwana. Alikuwa Mtawa wa ndani mashuhuri sana kwa karne ya kumi na tisa kwa tamaduni za kitaliano huku akionesha ujasiri wa kupenda maisha ya kitawa kinyume cha mtazamo wa vijana wengi.  Mnamo mwaka 1853 alivikwa mavazi ya kitawa na baadaye kujifunza kusoma na kuandika.  Walezi wake waliendelea kugundua karama zake zilizokuwa zimefichika ndani ya muunganiko na Msalaba wa Yesu Kristo.

Mwenye heri Maria Velotti hakuishia na maisha ya sala na tafakari bali aliwasikiliza wale waliohitaji ushauri wake hasa vijana, akiwatembelea wagonjwa na kuwasikiliza watu wa aina mbalimbali. Kwa bidii hiyo alianza kuwa kiongozi wa wengine na mnako mwaka 1878 alianzisha Shirika la kitawa la waabuduo Msalaba na mnamo mwaka 1886 aliaga dunia. Baada ya kuelewa maana ya mateso alijitahidi kuwa faraja kwa wengine na kuwahudumia maskini waliokuwa wametengwa na jamii. Alifahamu kuyafungamanisha maisha yake na mateso ya Kristo wa Msalaba.

Chumba cha Sr. Maria Luigia
Chumba cha Sr. Maria Luigia

Fumbo la zawadi ya Utakatifu lilijidhihirisha wazi katika wasifu wa maisha ya Maria Velotti akiwa na zawadi kadhaa ambazo huenda ikawa vigumu kwa watu wa kizazi hiki kuziiga. Huku tukizungumzia juu tafakari za ndani, aliziona hila za mwovu na kumwezesha kufanya uponyaji wa miujiza, aliiona mioyo ya watu kama mtu anayetazama kwenye kioo cha dirisha. Haya ni matukio ya kushangaza ambayo mara nyingi huwavutia watu na kuwageuza katika upendo na utakatifu wa kweli. Aidha Kardinali Crescenzio Sepe, amekazia kusema kuwa; haya yalikuwa maajabu yenye kuvutia katika utakatifu. Mwishoni Kardinali Crescenzio Sepe amehitimisha kwa kuthibitisha kuwa huo ndio utakatifu unaojifunua katika maisha ya mwenyeheri Maria Velotti aliyeishi upendo bila mipaka na bila kujibakiza.

26 September 2020, 16:21