Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 Septemba anaanza tena katekesi yake ikiwa na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 Septemba anaanza tena katekesi yake ikiwa na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. 

Katekesi za Papa Francisko na Ushiriki wa Watu wa Mungu

Papa katika kipindi cha miaka saba cha maisha na utume wake amedadavua kuhusu: Sakramenti za Huruma ya Mungu: Ubatizo, Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Ametafakari kuhusu Amri za Mungu, muhtasari wa maisha adili na matakatifu ya watu wa Mungu. Amejielekeza zaidi kwa katekesi kuhusu: familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya sala, haki, amani, upendo na maridhiano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 Septemba 2020 anaanza kuendesha katekesi yake kwa siku ya Jumatano asubuhi kwa ushiriki wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ndani ya Uwanja wa Jengo la Mtakatifu Damas, lililoko mjini Vatican. Katekesi na Ibada za Misa Takatifu zinazoendeshwa na Baba Mtakatifu ni matukio maalum ambayo yanamwezesha kukutana na watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anasema, inapendeza kuonana mubashara na watu wa Mungu na kuwapatia ujumbe wa Neno la Mungu kadiri ya nyuso na mazingira yao. Hii ni fursa inayomwezesha Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Kwa njia hii, Baba Mtakatifu anapata nafasi ya kugusa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, kwa sababu Wakristo wote ni mali ya Kristo na ni watoto wa Mama Kanisa.

Katika katekesi zake na mahubiri anayotoa wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican ni rahisi sana kwani yanayogusa na kuacha chapa katika akili na nyoyo za waamini. Ni nafasi ya kutangaza na kushuhudia mambo msingi ya kanuni maadili sanjari na imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hapa, Baba Mtakatifu anajipambanua kama Katekista mahiri anayewatangaza na kufafanua Neno la Mungu, ili kuwawezesha waamini kukutana na Kristo Yesu, anayewaletea mabadiliko katika maisha yao, ili waweze kupata utimilifu wa maisha, kwa kuendelea kuwatangazia Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha miaka saba cha maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amedadavua kuhusu: Sakramenti za Huruma ya Mungu hasa zaidi Sakramenti ya Ubatizo, Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Ametafakari kuhusu Amri za Mungu, muhtasari wa maisha adili na matakatifu ya watu wa Mungu. Amejielekeza zaidi kwa katekesi kuhusu: familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya sala, haki, amani, upendo na maridhiano.

Baba Mtakatifu amezungumzia amani kama kielelezo cha maendeleo fungamani ya binadamu kwa kukazia mchakato wa sera za uchumi shirikishi na maendeleo fungamani ya binadamu yanayopania kutoa huduma kwa mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anapenda kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiunga pamoja naye, ili kutafakari kuhusu janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kuangalia madhara yake, mintarafu magonjwa ya kijamii. Tafakari hii makini, inaongozwa na Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii ni nafasi muafaka ya kutumia Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuisaidia familia ya binadamu kuweza kuganga na kuponya ulimwengu huu unaoteseka kutokana na magonjwa makubwa na mazito!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa pamoja, wataweza kushiriki tafakari hii kama wafuasi wa Kristo Yesu anayeganga na kuponya, ili kujenga ulimwengu bora zaidi unaosimikwa katika matumaini kwa ajili ya vizazi vya sasa na vile vijavyo! Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa anapenda kuanza kukutana mubashara na watu wa Mungu wakati wa Katekesi, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini; kuganga na kusaidia kuponya madonda ya kijamii sanjari na kupyaisha maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe, kumbe, kuna haja ya kusimama na kutembea kwa pamoja kama ndugu wamoja, ili hatimaye, kwa pamoja watu wote waweze kutoka wakiwa washindi dhidi ya kipeo hiki cha janga la Corona, COVID-19 chenye changamoto pevu!

Papa: Katekesi Septemba 2020
01 September 2020, 14:03