Tafuta

Caritas Internationalis: Ili kukabiliana na changamoto mamboleo kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano na upendo wa dhati kwani binadamu wanahitajiana na kukamilishana. Caritas Internationalis: Ili kukabiliana na changamoto mamboleo kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano na upendo wa dhati kwani binadamu wanahitajiana na kukamilishana. 

Caritas Internationalis: Kipindi cha Kazi ya Uumbaji: Mshikamano na Upendo!

Caritas Internationalis inasema: Maadhimisho ya Kipindi cha Kazi ya Uumbaji ni muda wa kusherehekea utajiri unaobubujika kutoka katika imani ya Kikristo kama changamoto yakulinda na kutunza mazingira. Kama wafuasi wa Kristo Yesu, wakristo wanapaswa kuwa ni walinzi wa kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu kuilinda, kuitunza na kuiendeleza! IMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, hapo tarehe 24 Mei 2015, Siku ya Kuombea Kazi ya Uumbaji, imekuwa ikiadhimishwa na Kanisa Katoliki, kwa kuwa na mwelekeo wa kiekumene kila mwaka ifikapo tarehe 1 Septemba. “Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa huru katika nchi yote kwa watu wote waiketio. Itakuwa Jubilei kwenu”. Rej. Law 25: 10. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya VI ya Kuombea Kazi ya Uumbaji kwa Mwaka 2020 anajielekeza zaidi katika Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Maadhimisho ya Siku ya Mama Dunia. Kadiri ya Maandiko Matakatifu, Jubilei ni Kipindi cha kumbukumbu, toba na wongofu wa ndani, muda muafaka wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Kwa upande wake, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, linabainisha kwamba, Maadhimisho ya Kipindi cha Kazi ya Uumbaji ni muda muafaka wa kusherehekea amana na utajiri unaobubujika kutoka katika imani ya Kikristo kama changamoto na mwaliko wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Kama wafuasi wa Kristo Yesu, wakristo wanapaswa kuwa ni walinzi wa kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu kuilinda, kuitunza na kuiendeleza. Ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano mema na Mama Dunia, ili kurejesha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia. Caritas Internationalis inabainisha kwamba, Janga la Virusi vya Corona, COVID-19, limesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Limeonesha umuhimu wa ushirikiano na mafungamano ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiroho na hata kitamaduni. Katika tafakari ya kina, mwanadamu amegundua mifumo tenge ambayo imepelekea kusambaa kwa magonjwa na kwamba, binadamu ni dhaifu sana mbele ya Virusi vya Corona, COVID-19. Janga hili pia limekuwa ni fursa muhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana katika mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai. Mshikamano mpya umeibuka kutokana na changamoto za janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Caritas Internationalis imekuwa kifanya kazi bega kwa bega na Mashirika ya Caritas mahalia ili kupambana na janga hili.

Hii ni fursa ya kuendelea kusambaza “Virusi vya upendo na mshikamano” kama anavyokazia kusema Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Virusi vya upendo na mshikamano wa dhati vinaendelea kusambaa na kujionesha katika mitindo mbali mbali ya huduma mahali pengi duniani. Katika kipindi cha Maadhimisho ya Kazi ya Uumbaji, Caritas Internationalis inawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa kina na mapana jinsi ya kujenga jamii inayosimikwa katika haki na usawa, kwa kutoa fursa sawa kwa watu wote kuishi kikamilifu utu wao kama binadamu, huku wakiwa na uwiano mwema na Mama Dunia. Kama Wakristo, mahusiano na mafungamano yao yanapaswa kujielekeza zaidi katika kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, jirani pamoja na kazi ya uumbaji. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 liwe ni wito wa kuheshimu na kuthamini utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni wakati wa katekesi yake amewakumbusha walimwengu kwamba, kazi ya uumbaji ni kwa ajili ya binadamu wote na kwamba, wao wamekabidhiwa dhamana ya kulinda, kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji. Matunda ya kazi ya uumbaji yanapaswa kuwanufaisha watu wote bila ubaguzi. Lakini ukweli wa mambo ni kinyume kabisa cha matarajio ya wengi. Maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” ndio waathirika wakuu wa uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Maskini ndio wanaoendelea kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kuwapatia kipaumbele cha kwanza katika kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na usalama wa chakula duniani; wanakuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, mchakato wa utunzaji bora wa ekolojia unakuwa ni endelevu! Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis lina amini kwamba, maendeleo fungamani ya binadamu yanaweza kufikiwa tu, ikiwa kama, Injili ya uhai italindwa na kudumishwa kwa njia ya utunzaji wa ekolojia, sera makini za uchumi shirikishi na fungamani; masuala ya kijamii na kisiasa yakitoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kila mwananchi anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara kama ambavyo inapaswa kuwa kwa jamii nzima ya binadamu. Utashi, uhuru kamili na uwajibikaji ni mambo yanayopaswa kutambuliwa na kudumishwa na wote, ili kila mtu sehemu mbali mbali za dunia aweze kuwajibika kwa kuragibisha uwajibikaji huu kuanzia katika ngazi za chini kabisa. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19, iwe ni fursa ya toba na wongofu wa ndani, tayari kung’amua na kuambata njia mpya za maisha; kwa kujenga na kudumisha mafungamano yanayohemheshimu Mama Dunia, ekolojia, uchumi shirikishi na fungamani; masuala ya kijamii na kisiasa kama sehemu ya maisha ya mwanadamu. Viongozi wa kisiasa, watunga sera na watekelezaji wake, wanapaswa kufanya maamuzi magumu yatakayosaidia kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Waamini wasali zaidi kwa ajili ya kuombea utunzaji bora wa mazingira, lakini sala hii pia inapaswa kumwilishwa katika matendo yatakayosaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika mshikamano wa kidugu na upendo wa dhati!

Caritas Internationalis

 

 

 

02 September 2020, 15:24