Tafuta

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 13 Septemba 2020 amevikwa Pallio Takatifu kielelezo cha Kristo mchungaji mwema na alama ya umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 13 Septemba 2020 amevikwa Pallio Takatifu kielelezo cha Kristo mchungaji mwema na alama ya umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. 

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Avikwa Pallia Takatifu

Pallia hii imechukuliwa tangu kukiri kwa Mtakatifu Petro, ili aweze kuitumia ndani ya mipaka ya Jimbo kuu la Dar es Salaam. Iwe ni alama ya umoja, na ishara ya mshikamano na Kiti Kitakatifu cha Kitume. Iwe ni kifungo cha ukarimu na kichocheo cha ujasiri na nguvu, ili hatimaye, siku ya kuja na kujidhihirisha Kristo Yesu aweze kuupata yeye pamoja na kundi lake vazi la umilele na utukufu.

Na Padre Joseph Peter Mosha na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki nchini Tanzania limegawanyika katika Majimbo makuu saba ambayo ni Jimbo kuu la Mbeya, Dodoma, Arusha, Tabora, Songea, Mwanza na Dar es Salaam. Majimbo yote haya yanaongozwa na Maaskofu wakuu. Jimbo kuu la Dar es Salaam linaundwa na majimbo ya: Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Zanzibar, Mahenge na Ifakara. Majimbo yote haya yako chini ya uongozi wa Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi, aliyevikwa “Pallium” kwa lugha ya Kilatin ambayo kwa lugha sanifu ya Kiswahili ni Pallia Takatifu yaani vazi la Kiliturujia atakalokuwa analivaa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu anapokuwa katika maeneo ya Jimbo kuu la Dar es Salaam kadiri ya sheria za Kanisa za Mwaka 1983. Pallia takatifu hutokana na sufu safi iliyokatwa kutoka kwa kondoo waliobarikiwa wakati wa Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari. “Agnes” maana yake kwa lugha ya Kiswahili ni “Mwanakondoo”.

Mtakatifu Agnes, Bikira na shahidi, aliuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima, kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake. Na katika Agano Jipya Yohane Mbatizaji anamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu. Rej. Yn. 1:29, 36. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallia Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Pallia takatifu anayovaa Askofu mkuu shingoni ni alama ya Mchungaji mwema anayewabeba kondoo wake mabegani.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 24 Aprili 2005 wakati alipokuwa anasimikwa rasmi kuliongoza Kanisa Katoliki alisema kwamba, Pallia takatifu wanayovaa Maaskofu wakuu mabegani mwao ni alama pia ya wanakondoo waliopotea, wagonjwa na wadhaifu. Kumbe, ni dhamana na wajibu wa Askofu mkuu kuwabeba wote hawa na kuwapeleka kwenye maji ya uzima. Kumbe, Pallia takatifu ni kielelezo cha nira ya Kristo Yesu anayewaalika waja wake akisema “Jitieni nira yangu… kwa maana nira yangu ni laini…” Mt. 11:20. Pallia takatifu ni alama ya ushiriki mkamilifu wa Maaskofu wakuu katika kuliongoza Kanisa la Kristo. Pallia baada ya kutengenezwa huwekwa chini kabisa ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, karibu na kaburi la Mtakatifu Petro: “Confessio Petri” na kubarikiwa kesho yake tarehe 29 Juni ya kila mwaka, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa Kanisa. Pallia inapambwa kwa alama ya misalaba mitano, kielelezo cha Madonda Matakatifu ya Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Pallia inapambwa pia kwa misumari mitatu iliyotumika kumtundika Kristo Yesu Msalabani, mara mikono na miguu yake ikafungwa kwa misumari.

Itambukwa kwamba, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, ni kati ya Maaskofu wakuu 13 kutoka Barani Afrika ambao wanavishwa Pallio takatifu kwa kipindi cha Mwaka huu wa 2020. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Marek Solczyn’ski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Jumapili tarehe 13 Septemba 2020 katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Dar es Salaam amemvisha Pallia Takatifu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi. Katika sehemu ya kwanza ya Ibada, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi amekiri Kanuni ya Imani na hatimaye, akavishwa Pallia takatifu. Sala iliyofuatia imeeleza kwamba, Pallia hii imechukuliwa tangu kukiri kwa Mtakatifu Petro, ili aweze kuitumia ndani ya mipaka ya Jimbo kuu la Dar es Salaam. Pallia hii iwe ni alama ya umoja, na ishara ya mshikamano na Kiti Kitakatifu cha Kitume. Iwe ni kifungo cha ukarimu na kichocheo cha ujasiri na nguvu, ili hatimaye, siku ya kuja na ya kujidhihirisha Mungu aliye Mfalme wa Wachungaji, Kristo Yesu, aweze kuupata yeye pamoja na kundi lake lile vazi la umilele na utukufu!

Askofu mkuu Marek Solczyn’ski ametumia fursa hii kuwafafanulia watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam, mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 12 Januari 2015 kwa kutamka kwamba, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu watakuwa wanashiriki katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kubariki Pallia takatifu kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa imani, lakini Pallia takatifu watavikwa na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika kadiri ya nafasi zao. Lengo kuu la mabadiliko haya ni kuwawezesha watu wa Mungu kutoka katika Makanisa mahalia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya adhimu katika maisha, historia na utume wa Kanisa mahalia. Pili ni kuendelea kuimarisha mchakato wa unafsishaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.”

Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 30 Juni 2004 alisema kwamba, Watakatifu Petro na Paulo, walitangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa kumwanga damu yao. Pallia takatifu ni kielelezo cha umoja wa Kanisa ambalo limesimikwa katika hiarakia. Kwa sababu Kanisa ni moja linahitaji huduma ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ambye ndiye kiongozi mkuu katika Urika wa Maaskofu. Kanisa la Kiulimwengu linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili sanjari na kuwahudumia watu wa Mungu. Baada ya kuhitimisha sehemu ya kwanza ya Liturujia ya kukabidhiwa Fimbo ya Kichungaji na Kuvikwa Pallia takatifu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi aliendelea kuongoza Ibada ya Misa takatifu. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Ruwa’ichi, amewahimiza waamini kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajumbe wa huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya. Wawe ni watu wa msamaha na matendo mema yenye mvuto na mashiko kwa jirani zao. Waamini wajifunze kusamehe na kusahau, tayari kuwarudishia jirani zao wema na fadhila ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu Baba Mwenyezi. Wakristo wanatumwa kuwa ni mashuhuda wa utashi wa Mungu na wajumbe wa huruma ya Mungu kwa jirani zao.

Ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu huu, Wakristo wanapaswa kuzama katika maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani. Waamini watambue kwamba, hata wao ni wakosefu wanahitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu, kumbe, Mwenyezi Mungu asichoke kuwasamehe, kuwapokea na kuwajalia amani. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi amewataka waamini kuwakumbuka na kuwaombea wale wote ambao wameonja nyanyaso na visasi katika maisha yao, ili waone faraja na nguvu ya Mungu inayoganga na kuokoa, ili wasije hata wao wakakengeuka na kutopea katika hali ya kutaka kulipiza kisasi. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na: wakleri, watawa na viongozi wakuu wa Halmashauri ya Majimbo na Maaskofu Katoliki kutoka: Tanga, Mahenge, Zanzibar, Morogoro na Ifakara. Baadaye alasiri, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi akiwa ameambatana na Askofu mkuu Marek Solczyn’ski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, wameshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Utume wa Wanaume Wakatoliki Tanzania, UWAKA na kufanikiwa kuchangisha kiasi cha shilingi milioni saba ni picha moja iliyonunuliwa kwa njia ya mnada. Lakini kiasi cha fedha zote ni shilingi milioni 11 kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Pallia Takatifu

 

14 September 2020, 14:55