Tafuta

Vatican: Afya bora, maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kumbe yanapaswa kutumiwa vyema! Vatican: Afya bora, maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kumbe yanapaswa kutumiwa vyema! 

Maji Safi na Salama Ni Sehemu ya Haki Msingi Za Binadamu!

Maendeleo fungamani ya binadamu kwa siku za usoni, yatategemea kwa kiasi kikubwa jinsi ambavyo Jumuiya ya Kimataifa itaweza kuyatunza na kuyatumia maji kwa ajili ya mafao ya wengi. Afya bora, maji safi na salama ni mahitaji msingi ya binadamu, lakini pia yana umuhimu wake kwa viumbe wote wanaoishi duniani. Walimwengu wanapaswa kufaidika na haki hii msingi katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uhaba wa maji safi na salama unaweza kuwa ni chanzo cha migogoro na kinzani kwa siku za usoni, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitasimama kidete kulinda vyanzo vya maji pamoja na kutambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi. Dhana ya maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni agenda iliyoibuliwa hivi karibuni, lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na unyeti wake! Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria, kiufundi, kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa  utamaduni wa utunzaji bora wa vyanzo vya maji. Kwa njia hii, amani duniani inaweza kuimarishwa kwa kuzuia vita, kinzani na migogoro inayoweza kufumbatwa katika mafao ya kisiasa na kiuchumi kwa kubeza: haki msingi, utu, heshima na maisha ya binadamu!

Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss, hivi karibuni akichangia katika mkutano wa 45 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya afya, maji safi na salama, amekazia kwamba, maji ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maendeleo fungamani ya binadamu kwa siku za usoni, yatategemea kwa kiasi kikubwa jinsi ambavyo Jumuiya ya Kimataifa itaweza kuyatunza na kuyatumia maji kwa ajili ya mafao ya wengi. Afya bora, maji safi na salama ni mahitaji msingi ya binadamu, lakini pia yana umuhimu wake kwa viumbe wote wanaoishi duniani. Ujumbe wa Vatican umeendelea kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na maboresho makubwa yatakayowawezesha walimwengu kufaidika na haki hii msingi katika maisha yao.

Huduma ya afya bora, maji safi na salama ni wajibu wa Serikali husika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwani huu ni wajibu wa watu wote, ili kusaidia mchakato wa kijamii na maendeleo fungamani ya binadamu. Askofu mkuu Ivan Jurkovič, anakaza kusema, haki msingi ya afya bora, maji safi na salama inapata chimbuko lake katika utu na heshima ya binadamu. Maji safi na salama yana mchango mkubwa katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Kumbe, maji safi na salama hayawezi kugeuzwa kuwa sawa na bidhaa nyingine yoyote kwa sababu ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Ni katika muktadha huu, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, uratibu wa maji unaunganishwa na wajibu wa kijamii kwa kuwa na mwelekeo sahihi wa kiekolojia sanjari na ujenzi wa mshikamano miongoni mwa nchi mbalimbali.

Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kufanikiwa kuwa na matumizi bora zaidi ya maji safi na salama pamoja na kudumisha utunzaji bora zaidi wa vyanzo vya maji. Baba Mtakatifu Francisko anasema, changamoto mbalimbali zinazomwandamana mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, zinahitaji umoja, ushirikiano na mshikamano, kwa kuendelea kutafuta njia bora na rafiki zitakazomsaidia mwanadamu kukabiliana na changamoto hizi katika uso wa dunia.

Maji Safi na Salama
21 September 2020, 15:24