2020-08-28: Papa ni mwenye ibada ya Mtakatifu Monika alitembelea Kanisa Kuu la Mtakatifu Agostino na kuweka mawaridi katika kaburi la Mtakatifu Monika. 2020-08-28: Papa ni mwenye ibada ya Mtakatifu Monika alitembelea Kanisa Kuu la Mtakatifu Agostino na kuweka mawaridi katika kaburi la Mtakatifu Monika. 

Papa ni mwenye ibada ya Mtakatifu Monika!

Tarehe 27Agosti Papa Francisko alitembelea Kanisa Kuu la Mtakatifu Agostino huko Campo Marzio ili kusali mbele ya kaburi la Mama yake Mtakatifu wa Hippo.Ni uhusiano wa kiroho uliokua kwa kipindi kirefu kama anavyosimulia Padre Pasquale Di Lernia katika mahojiano na Vatican News.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican.

Kwa mara nyingine tena Papa katika siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha kiliturujia ya Mtakatifu Monica alipendelea kwenda katika Kanisa kuu la kiroma la Mtakatifu Agostino ambalo tangu karne ya XV linahifadhi masalia ya Mtatifu huyo  na kuweka mawaridi meupe kama heshima kwa mtakatifu huyo  mama wa Mtakatifu Agostino.

Mara baada ya kufika humo Papa Francisko alibaki kwenye sala kama dakika 10 hivi na baadaye akaweza kukaa na watawa wa kiagostino. Vile vile alibaki kwa kutazama na kushangaa picha ya Bikira Maria wa hija au wa Loreto inayohifadhiwa katika Kikanisa kidogo cha kwanza kulia katika Kanisa kuu na mwisho alisimama mbele ya sanamu ya Mama Maria wa kujifungua iliyochongwa na Jacopo Tatti aitwaye Sansovino.

Watawa wa kiagostini walitumia  fursa hiyo kuweza kumkaribisha Papa Francisko  huko Pavia kunako mwaka 2023 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Pietro wa “Ciel d'Oro”, yaani mbingu ya dhahabu mahali panapohifadhiwa kaburi la Mtakatifu Agostino ili kusherehekea karne  ya 13 tangu  kuwasili kwa masalia hayo. Padre  Pasquale Di Lernia, katibu mkuu wa shirika wa Waagostino ambaye alikuwa mmojawapo wa watawa waliomkaribisha Papa amesimulia kuhusu ibada ya Papa Francisko kwa Mtakatifu Monika na maombi yake kwa watawa mara walipopata fursa mbali mbali ya kukutana naye na kwamba wasali kwa ajili yake katika kaburi la Mama wa Mtakatifu Agostino. Papa Francisko amewaeleza aidha watawa hao kuhusu kurithi uhusiano na Mtakatifu Monika kupitia kwa mama yake ambaye alikuwa ni mmoja wa wanachama ambao somo wao alikuwa ni Monika.

Hata hivyo Papa Francisko alikuwa ameingia katika kikanisa hicho na kusali katika kaburi la Mtakatifu Monika tarehe 27 Agosti, miaka miwili iliyopita wakati anarudi kutoka Ireland katika fursa ya Maadhimisho ya Siku ya Familia ulimwenguni 2018 hasa mara  baada ya kumaliza sala yake kama kawaida katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu Afya ya waroma ili kumshukuru Bikira Maria kwa ajili ya ziara yake aliyokuwa ametimiza, alikwenda  moja kwa hata katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Monika.

Papa akiwa bado ni Kardinali  vile vile alikuwa mara nyingi akienda  kusali mbele ya kaburi hilo la mama wa Askofu wa Hippo. Monika alifariki huko Ostia Tiberina, kunako  mwaka 387 na kwa karne nyingi masalia yake yameweza kutolewa ibada katika Kanisa la Mtakatifu Aurea, huko Ostia Antica. Alikuwa ni Papa Martino wa V aliyependelea kuhamisha masalia hayo  katika jiji kuu. Leo hii katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Agostino huko Campo Marzio, karibu na uwanja wa Navona  ndipo kuna michoro mizuri sana ya mama wa Baba kuu wa Kanisa. Ukiingia upande wa kushoto mwa Altare  utaona michoro mizuri tangu mwaka 1885 ya Pietro Gagliardi inayosimulia matukio tofauti ya maisha ya Mtakatifu Monika.

28 August 2020, 16:00