Tafuta

Shirika la Wayesuit kuanzia tarehe 20 Mei 2021 hadi tarehe 31 Julai 2022 wanaadhimisha Mwaka wa Wayesuit Duniani unaoongozwa na kauli mbiu "Angalieni Mambo Yote Mapya katika Kristo". Shirika la Wayesuit kuanzia tarehe 20 Mei 2021 hadi tarehe 31 Julai 2022 wanaadhimisha Mwaka wa Wayesuit Duniani unaoongozwa na kauli mbiu "Angalieni Mambo Yote Mapya katika Kristo".  

Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola: 20 Mei 2021-31 Julai 2022

Padre Arturo Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit ametangaza kwamba, kuanzia tarehe 20 Mei 2021 hadi tarehe 31 Julai 2022, Wayesuit watakuwa wanaadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Kauli mbiu: “Angalieni mambo yote mapya katika Kristo”. Mwaka mzima utaongozwa na Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani: 2019-2029.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Wayesuit lililoanzishwa na Mtakatifu Inyasi wa Loyola katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, linapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo makuu yafuatayo: Kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na mafungo ya maisha ya kiroho; Kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao; Mwishoni, ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Haya ni mambo ambayo yanabainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia hivi karibuni Padre Arturo Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit kama sehemu ya Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani kuanzia mwaka 2019-2029. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi pia ndivyo vipaumbele vya Kanisa la Kiulimwengu kwa wakati huu! Mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sinodi za Maaskofu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Vipaumbele hivi vinachota utajiri wake kutoka katika Wosia wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili.” Vipaumbele vya Wayesuit katika kipindi cha miaka kumi ni msingi wa uhusiano na mafungamano kati ya Wayesuit na Kristo Yesu; mambo yanayomwilishwa katika maisha binafsi na katika Jumuiya inayosali na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Vipaumbele hivi ni sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Wayesuit ambao umefanyiwa kazi katika kipindi cha miaka miwili, ili kuhakikisha kwamba, Wayesuit wanatumia kikamilifu rasilimali watu, vitu na fedha, ili kufikia lengo hili muhimu, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati. Hapa kinachohitajika ni kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu, kwa kuwashirikisha watu kutoka katika makundi na medani mbali mbali za maisha, ili kugundua amana na utajiri unaofumbatwa katika mafungo ya kiroho yanayotolewa na Wayesuit.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, haki jamii inapewa msukumo wa pekee, ili kweli mabadiliko makubwa yanayojitokeza katika masuala ya: kiuchumi, kijamii na kisiasa, yanazingatia haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao ni pamoja na kuyaangalia yale mema, mazuri na matakatifu yanayowazunguka vijana katika “vijiwe vyao”, kwa kusikiliza na kujibu kiu na matamanio yao halali kadiri ya mabadiliko ya jamii; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Hii ni changamoto ya kuwapatia vijana fursa ya kuonesha vipaji na ubunifu wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Umefika wakati kwa viongozi wa Kanisa kujifunza kutoka kwa vijana wa kizazi kipya! Mwishoni, ni utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kushiriki katika sera, mbinu na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira, pamoja na kuangalia sera mbadala, ili kuweza kudhibiti uharibifu wa mazingira unaoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu wengi duniani. Hii ni changamoto ya kushirikiana na wadau mbali mbali kama sehemu ya mbinu mkakati wa utekelezaji wa malengo haya katika maisha na utume wa Wayesuit.

Ni katika muktadha huu, Padre Arturo Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit ametangaza kwamba, kuanzia tarehe 20 Mei 2021 hadi tarehe 31 Julai 2022, Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Wayesuit watakuwa wanaadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Tarehe 20 Mei ni kumbukumbu ya siku ile ambayo Mtakatifu Inyasi alijeruhiwa vitani huko Pamplona na huo ukawa ni mwanzo wa toba na wongofu wake wa ndani. Maadhimisho haya yatadumu kwa kipindi cha miezi kumi na nne, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kupyaisha maisha na utume wao mbele ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Maadhimisho haya yanapambwa na kauli mbiu “Angalieni mambo yote mapya katika Kristo”. Mwaka mzima utaongozwa na Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani: 2019-2029. Wayesuit wamwombe Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema ya toba na wongofu wa ndani katika maisha na utume wao kila kukicha! Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola ni fursa ya kushirikiana na wadau mbali mbali katika maisha na utume wa Wayesuit, ili kuweza kuyapatanisha yote na Kristo Yesu.

Karama ni chemchemi ya maisha na utume wa Shirika, mwaliko na changamoto ya kujenga ukaribu zaidi katika utume ambao Shirika limekabidhiwa na Roho Mtakatifu, ili mwaliko huu uweze kuingia na kugusa undani wa maisha ya watu zaidi. Wayesuit wanataka kujifunza kutoka kwa vijana, ili waweze kuwasindikiza, ili kugundua maana ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Lengo ni kuwajengea vijana uwezo wa kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; mahali ambapo utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wayesuit wanataka kushirikiana na vijana wa kizazi kipya: Muda, ndoto na matumaini waliyo nayo! Kwa Wayesuit waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia, huu ni muda wa kufuata nyayo za Mtakatifu Inyasi wa Loyola, hujaji maarufu, kwa njia ya mapambano ya maisha ya kiroho, toba na wongofu wa ndani, ili kujenga mahusiano ya karibu na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola.

Ukaribu na upendo kwa Mwenyezi Mungu, uwasaidie Wayesuit kujenga na kudumisha umoja katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha Miaka 10. Wao ni warithi wa karama ambayo imeshehenu tunu msingi za maisha ya kimisionari. Ufukara pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu ni kati ya mambo ambayo Mtakatifu Inyasi wa Loyola aliyapokea kama zawadi kutoka juu. Mfano wa maisha ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola na wale wenzake, uwawezeshe Wayesuit kujenga mahusiano ya pekee na Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia amani na utulivu wa ndani. Wawe mstari wa mbele katika kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni sehemu ya urithi na amana inayobubujika kutoka katika Karama ya Wayesuit. Huu ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa kila kukicha! Lengo ni kushikamana na maskini, ili kuleta mageuzi katika miundo mbinu inayokandamiza utu na heshima ya binadamu. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 imesababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu.

Mpasuko mkubwa kati ya maskini na matajiri umeonekana wazi wazi. Kumekuwepo na kinzani katika Jumuiya ya Kimataifa pamoja na uwiano tenge katika masuala ya kiekolojia. Wayesuit waungane na Kristo Yesu pamoja na maskini, kwa kuishi na kuukumbatia ufukara wao, kama ushuhuda wa upendo wao kwa Kristo Yesu. Wayesuit watambue na kukiri dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kujitambulisha na Kristo Yesu, ili aweze kuwasaidia kutubu na kumwongokea. Wawe tayari kuleta mabadiliko katika maisha ya maskini, kwa kusoma alama za nyakati, kwa toba na wongofu wa ndani ili kupyaisha karama ya Shirika. Wayesuit wajenge umoja na mshikamano na Kristo Yesu, ndugu na rafiki yao mpendwa, ili aweze kuwakirimia imani, matumaini na mapendo kwa kuendelea kukaaa pamoja nao, chini maongozi ya Roho Mtakatifu.

Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola 2021-2022

 

08 August 2020, 07:00