Tafuta

Vatican News
Mfuko wa Maendeleo ya Watu wa Amerika ya Kusini na Caribbean kwa Mwaka 2020 unagharimia miradi 168 katika nchi 23, kielelezo cha ushuhuda wa huruma na upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Mfuko wa Maendeleo ya Watu wa Amerika ya Kusini na Caribbean kwa Mwaka 2020 unagharimia miradi 168 katika nchi 23, kielelezo cha ushuhuda wa huruma na upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.  (AFP or licensors)

Mfuko wa Maendeleo Ya Watu wa Amerika ya Kusini na Caribbean

Miradi 168 iliyopitishwa inalenga kuwa ni ushuhuda wa huruma na upendo wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mama Kanisa anawaalika na kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, ili kwa pamoja kuishinda COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wadau mbali mbali wamejitokeza na kujifunga kibwebwe kupambana na janga kubwa la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa weledi, ukarimu na uwajibikaji mkuu. Hizi ni juhudi zilizowaunganisha watu katika ngazi mbali mbali za maisha ya kijamii na kiroho. Madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Wametekeleza dhamana hii kwa moyo mkuu na ushupavu wa hali ya juu kabisa, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao na familia zao. Kuna baadhi yao wameambukizwa na wengine wamefariki dunia kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Janga la Corona, COVID-19 limegusa na kutikisa maisha ya watu na historia ya Jumuiya mbali mbali Baba Mtakatifu anapenda kutoa angalisho kwa watu wote wa familia ya Mungu kutojisahau kwani mara tu baada ya kipeo cha janga la Corona, COVID-19 wakajikuta wakitumbukia katika ombwe na hali ya kufikirika. Ni rahisi sana kuwasahau majirani; au watu wengine wanaowahudumia.

Hivi karibuni, Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu wa Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean unaosimamiwa na kutekelezwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu chini ya Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, imefanya mkutano wake wa mwaka na kupitisha miradi 168 itakayotekelezwa katika nchi 23 za Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean. Mkutano huu umefanyika kwa njia ya mitandao ya kijamii. Imekuwa ni fursa kwa Bodi ya Wakurugenzi kufanya tathmini ya kina kuhusu madhara yaliyosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 huko Amerika ya Kusini na kwenye Visiwa vya Caribbean. Kuna ushirikiano mkubwa kati ya Mfuko wa Maendeleo ya Watu wa Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean na Tume ya Kudhibiti Virusi vya Corona, COVID-19 Vatican ambayo iko chini ya Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu.

Hii ni tume inayopania kuonesha huruma na upendo wa Kanisa kwa familia ya binadamu katika ujumla wake. Mkutano huu ulikuwa chini ya Askofu Javier del Rio Alba wa Jimbo kuu la Arequipa nchini Perù kama Mwenyekiti wa Bodi. Kwa upande wake, Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, amewashukuru na kuwatia shime wajumbe katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha ya mwanadamu. Akawasihi waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika eneo lao. Huduma inayotolewa na Mama Kanisa inapaswa kuwa ni ushuhuda wa imani, mapendo na mshikamano ili kuwaondolea watu hofu na taharuki kwa kuwajengea matumaini. Ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI ulihudhuria pia kwa kutambua kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ndiye mfadhili mkuu wa miradi hii ambayo imepitishwa na Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Watu wa Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kuanzia mwaka 2018 limeanza pia kuchangia gharama ya miradi inayosimamiwa na kutekelezwa na Mfuko huu.

Wadau wengine ni Hispania kupitia Shirika la Misaada la “Manos Unidas”. Miradi yote iliyopitishwa inalenga kuwa ni ushuhuda wa huruma na upendo wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.Mama Kanisa anawaalika na kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, ili kuhakikisha kwamba, katika mapambano na hatimaye ushindi dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 hakuna mtu awaye yote atakayebakia nyuma kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Itakumbukwa kwamba, Mfuko wa Maendeleo ya Watu wa Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watu mahalia huko Amerika ya Kusini na kwenye Visiwa vya Caribbean kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi ili kupambana na hali pamoja na mazingira yao, ili hatimaye, yaweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko huu, alikazia umuhimu wa mshikamano kati ya watu mbali mbali huko Amerika ya Kusini, ili kupambana kikamilifu na ongezeko la deni la nje linalokwamisha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu na hivyo kusababisha umaskini wa hali na kipato kuongezeka kwa kasi sanjari na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu yanapaswa kupewa msukumo wa pekee na wala si fedha kama kipimo cha ustawi na maendeleo ya kiuchumi. Watu wote wanayo haki ya kushiriki katika ustawi na maendeleo yao na kufaidika na rasilimali za dunia, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Walengwa wakubwa ni maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuinua na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu, ili hatimaye, waweze kujisikia kuwa ni wadau katika mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mfuko wa Maendeleo ya Watu utachangia kiasi kikubwa katika sera na mikakati ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya watu huko Amerika ya Kusini na katika Visiwa vya Visiwa vya Caribbean.

Mfuko wa Maendeleo
13 August 2020, 13:50