Vatican News
Mchango wa upendo na mshikamano wa kidugu na kiimani na Nchi Takatifu utafanyika tarehe 13 Septemba 2020 ili kusaidia shughuli mbali mbali za kichungaji na kijamii eneo la Nchi Takatifu. Mchango wa upendo na mshikamano wa kidugu na kiimani na Nchi Takatifu utafanyika tarehe 13 Septemba 2020 ili kusaidia shughuli mbali mbali za kichungaji na kijamii eneo la Nchi Takatifu.  (AFP or licensors)

Mchango wa Mshikamano na Nchi Takatifu: 13 Septemba 2020

Papa kwa kusoma alama za nyakati, akaridhia ombi lililowasilishwa kwake na Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki na kuamua kwamba, mchango wa mshikamano na upendo wa kidugu ufanyike Jumapili, tarehe 13 Septemba 2020 katika makesha ya kuadhimisha Sherehe ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa miaka mingi, watu wa Mungu katika Nchi Takatifu wamekuwa wakifurahia ukarimu kutoka kwa waamini wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa njia ya upendo wa mshikamano, waliweza kuendelea na maisha yao ya kila siku kama kielelezzo cha uwepo wao wa Kiinjili katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, ili kujenga mazingira ya amani na utulivu. Lakini mambo yamekwenda mrama sana kwa maadhimisho ya Juma Kuu kwa Mwaka 2020 kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati, akaridhia ombi lililowasilishwa kwake na Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki na kuamua kwamba, mchango wa mshikamano na upendo wa kidugu ufanyike Jumapili, tarehe 13 Septemba 2020 katika makesha ya kuadhimisha Sherehe ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba.

Hii ni Siku ambayo Masalia ya Msalaba Mtakatifu yaligunduliwa huko Yerusalemu na huo ukawa mwanzo wa ujenzi wa Kanisa kuu la Kaburi Takatifu na Ibada ya hadhara. Padre Francesco Patton, OFM, Mlinzi mkuu wa maeneo matakatifu anasema, kwa namna ya pekee kabisa, Wakristo wanaadhimisha Sherehe ya Kutukuka kwa Msalaba, kama chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, kwa kumtoa Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu ili aje kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kumbe, Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha wokovu wanadamu na upatanisho ulioletwa na Kristo Yesu, kati ya binadamu na Muumba wake na kati ya binadamu wenyewe. Msingi wa ubinadamu mpya unasimikwa katika mshikamano wa udugu na upendo wa dhati, kielelezo makini cha imani tendaji!

Ni matumaini ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kwamba, huu utakuwa ni mwanzo wa matumaini mapya na wokovu baada ya mateso makubwa yanayowakabili watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Hiki ni kipindi cha upendo na mshikamano kwa wale wote wanaoendelea kuishi katika Nchi Takatifu, mahali ambapo ni mwanzo wa Habari Njema ya Wokovu. Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu: Ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda wakiwa pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, mwaliko mahususi kwa Wakristo ni: kumtafakari Kristo mfufuka mbaye ni kiini na chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa waja wake. Mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu ni huduma inayotolewa kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa kuonesha mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu, kwa kuchangia kwa hali na mali.

Mchango huu unaliwezesha Kanisa kuendelea kulinda na kutunza maeneo matakatifu ya dini ya Kikristo! Mchango huu ni muhimu sana katika kugharimia shughuli mbali mbali za kitume na kichungaji zinazotolewa na Mama Kanisa katika maeneo haya. Mchango huu utaliwezesha Kanisa kuendelea kutoa huduma bora ya elimu kwa wanafunzi zaidi ya 10, 000 wanaopata elimu kutoka katika shule, taasisi, vyuo vya elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu. Ni msaada unaoliwezesha Kanisa kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, bila kuwasahau wale ambao wameathirika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Siria. Huu ni mshikamano wa imani, matumaini na mapendo kwa kutambua kwamba, imani ya Kikristo inapata chimbuko lake kutoka katika Nchi Takatifu. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Paulo VI, kwa mara ya kwanza alitembelea Nchi Takatifu mwezi  Januari 1964 na kuguswa na mahitaji ya Wakristo.

Katika Wosia wake wa kitume “Nobis in animo” yaani “Umuhimu wa Kanisa katika Nchi Takatifu”  uliochapishwa tarehe 25 Machi 1974, alikazia umoja na mshikamano wa waamini na huo ukawa ni chanzo cha Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu "Pro Terra Sancta". Mtakatifu Paulo VI alihimiza sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu, kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo unaoonesha jiografia ya ukombozi. Tangu wakati huo, Kanisa linaendelea kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoteseka kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, ni alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uekumene wa damu, huduma na sala pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika misingi ya: haki, amani na maridhiano.

Ni kwa njia ya ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano Kanisa linataka kuwajengea waamini na watu wote wenye mapenzi huko Mashariki ya kati Injili ya amani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi ili kuondokana na: vita, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kiimani, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika ujumbe wake kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa mwaka 2020 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Katika mateso, Kristo alionesha kwa namna ya pekee mshikamano na watu wanaoteseka; watu wanaoendelea kuadhimisha Ijumaa kuu katika maisha yao kutokana na upweke hasi, vita, baa la njaa, kwa kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna watu wenye njaa ya chakula na upendo; kuna watu wanaoelemewa na Msalaba wa upweke na hali ya kutengwa na hata na watoto pamoja na ndugu zao wenyewe.

Kuna watu wanaoelemewa na Msalaba wa kiu ya haki na amani; Msalaba wa uzee; wakimbizi na wahamiaji ambao wanafungiwa mipaka kutokana na woga usiokuwa na mashiko; kuna watu wanaoelemewa na Msalaba wa masuala ya kisiasa; watoto wasiokuwa na hatia walionyanyaswa na kudhulumiwa utu na heshima yao; watu wanaoteseka kutokana na usasa! Kristo Yesu anaendelea kupyaisha matumaini kwa waja wake kwa njia ya Fumbo la Ufufuko na ushindi wake dhidi ya dhambi na mauti! Nchi Takatifu ni mahali ambapo pameshuhudia Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka; kielelezo cha upendo wa Kristo Yesu unaookoa. Nchi Takatifu ni mahali ambapo Yesu alitoka jasho la damu. Ni mahali alipoweka Sakramenti ya Ekarisri Takatifu, akashuhudia huduma inayomwilishwa katika upendo kwa kuwaosha wanafunzi wake miguu kielelezo makini cha udugu wa upendo. Akiwa katika Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari baada ya kuhukumiwa kuteswa na kufa Msalabani, Simoni wa Kirene alimsaidia kubeba Msalaba, hadi alipofikia kileleni. Kabla ya kukata roho, akawakabidhi wanafunzi wake kwa Bikira Maria. Akakata roho na kuzikwa kwenye kaburi jipya, ambako alifufuka siku ya tatu kadiri ya Maandiko Matakatifu.

Kardinali Leonardo Sandri katika barua yake kwa ajili ya Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu "Pro Terra Sancta kwa mwaka 2020" anaendelea kufafanua kwamba, Nchi Takatifu na kwa namna ya pekee, Jumuiya ya Wakristo imekuwa na nafasi na mchango wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa, unaooneshwa kwa njia ya mshikamano na msaada wa kiuchumi tangu nyakati ya Mtakatifu Paulo, Mtume. Kanisa la Kiulimwengu limepata zawadi ya Furaha ya Injili na Wokovu kwa njia ya Kristo Yesu “jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake” 2 Kor. 8:9. Furaha ya Injili inawasukuma na kuwahamasisha Wakristo kuwashirikisha jirani zao furaha na ukarimu kwa kuendeleza ombi la uaminifu wa watoto wa Kanisa. Nchi Takatifu na hasa Ukanda wa Mashariki ya Kati ni eneo ambalo limekumbwa na majaribu makubwa kwa miaka mingi, kiasi kwamba, kwa siku za hivi karibuni idadi ya Wakristo huko katika Nchi Takatifu inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka na Mapokeo ya Kikristo kutoweka kama “ndoto ya mchana”. Matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Athari zake zitaendelea kusikika kwa vizazi vyote. Hawa ni watoto waliopokwa haki yao ya utoto, kwa kukosa fursa ya elimu ufunguo wa maisha kwa siku za usoni. Elimu ingewawezesha kugundua wito pamoja na kupata fursa za ajira, ili kuwa na maisha bora zaidi na hatimaye, kumalizia maisha ya uzee wao kwa amani.

Mama Kanisa anajitahidi kuhakikisha kwamba,  analinda na kudumisha uwepo wa Wakristo katika Nchi Takatifu kama sauti ya watu wasiokuwa na sauti. Anatekeleza dhamana hii kwa njia ya shughuli za kichungaji na Kiliturujia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo huko Nchi Takatifu. Kanisa linatoa elimu kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kama unavyofafanuliwa kwenye “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Maisha ya Pamoja”. Yote haya yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukarimu unaoshuhudiwa na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa linaendelea kuwajengea uwezo wanandoa watarajiwa na wale wote wanaotafuta fursa za ajira. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya umaskini kwa kuwajengea watu uwezo wa kiuchumi pamoja na kuwapatia huduma bora za afya, bila kusahau msaada mkubwa kwa wakimbizi na wahamiaji huko Mashariki ya Kati. Utunzaji wa Madhabahu na nyumba za Ibada ni kielelezo cha ukarimnu kutoka kwa waamini.

Lengo ni kuendelea kutunza maeneo matakatifu ya Fumbo la Umwilisho na Pasaka, mahali ambapo Wakristo wanapata msingi wa utambulisho wao pamoja na maisha bora zaidi. Kwa njia hii, Wakristo katika Nchi Takatifu wameendelea kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotembelea Nchi Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko tangu wakati, anapenda kuwashukuru wale wote watakaochangia kwa ari na moyo wa upendo na ukarimu kwa ajili ya Nchi Takatifu

Mchango Nchi Takatifu

 

 

13 August 2020, 14:17