Tafuta

Vatican News
Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani linalipongeza Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa Kuadhimisha Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake na Miaka 25 ya "Ut Unum Sint" Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani linalipongeza Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa Kuadhimisha Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake na Miaka 25 ya "Ut Unum Sint"  (Vatican Media)

Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani na Uekumene

Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani amemtumia salam, pongezi na matashi mema Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika maadhimisho ya matukio makuu mawili mintarafu mchakato wa majadiliano ya kiekumene: Miaka 60 ya Baraza na Miaka 25 ya Waraka wa JPII: "Ut Unum Sint" Wamoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa mwaka 2020 linaadhimisha Matukio makuu mawili. Mosi, ni Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Ut unum sint” yaani “Ili wawe wamoja: Dhamana ya Kiekumene”. Ujumbe huu ulichapishwa hapo tarehe 25 Mei 1995. Huu ni mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na ni njia ya Kanisa inayojikita katika upyaisho wa maisha na wongofu wa ndani. Ni Waraka wa Kitume uliochapishwa kama kumbukumbu ya miaka 30 baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mtakatifu Yohane Paulo II akakazia tena umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Pili, ni kumbukumbu ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXIII alipoanzisha Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kama lilivyokuja kufahamika tangu mwaka 1988.

Lengo ni kuendeleza majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali, ili kujenga fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa ambalo limejeruhiwa kutokana na utengano miongoni mwa Wakristo. Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, “The Lutheran World Federation”, (LWF) amemtumia salam, pongezi na matashi mema Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika maadhimisho ya matukio makuu mawili mintarafu mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Katika kipindi cha miaka 60, baada ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kuna viongozi waliojipambanua katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hawa ni pamoja na Kardinali Augustin Bea alijizatiti kutekeleza mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano ya kiekumene. Kumekuwepo na mafanikio makubwa kati ya Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani na Kanisa Katoliki.

Tume za pamoja zimeweza kuchapisha Tamko la Mwaka 1980: Wote Chini ya Kristo Mmoja; “All Under One Christ” na Tamko la Mwaka 1999: “Joint Declaration on the Doctrine of Justification” Kuhusu Kuhesabiwa haki. Tamko hili linapembua kwa kina: Kuhusu Ujumbe wa Biblia juu ya kuhesabiwa haki; mafundisho ya kuhesabiwa haki kama suala la kiekumene. Tamko linatoa ufafanuzi kuhusu ufahamu wa pamoja wa kuhesabiwa haki, maelezo ya ufahamu wa pamoja wa kuhesabiwa haki, udhaifu wa binadamu na dhambi, kuhusiana na kuhesabiwa haki: Tamko linaangalia kuhesabiwa haki kama msamaha wa dhambi na kuwafanya watu wenye haki; kuhesabiwa haki kwa imani na kwa njia ya neema; aliyehesabiwa haki kama mtu mkosefu. Mambo mengine yaliyopembuliwa kwenye Tamko hili ni pamoja na: Sheria na Injili; uhakikisho wa wokovu; matendo mema ya mtu aliyehesabiwa haki na hatimaye ni umuhimu na lengo la maafikiano yaliyofikiwa. Matamko haya mawili ni dira na mwongozo wa majadiliano ya kiekumene na Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani.

Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani anasema, tarehe 31 Oktoba 2016 lilizindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, tukio ambalo lilimshirikisha Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wengine wakuu wa Makanisa. Tukio hili, lilikuwa ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani katika kipindi cha miaka 50 iliyopita na matunda yake yanaanza kuonekana. Kilele cha Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri kilikuwa ni Mwaka 2017 kwa kukazia: shukrani, toba na matumaini. Wakristo wana kiu ya kutaka kuona kwamba, wanaungana na kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu. Miaka yote hii ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kutoka katika kinzani, kuelekea katika ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Hiki ni kipindi cha kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mchakato huu wa majadiliano ya kiekumene!

Itakumbukwa kwamba, Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., wakati ule alisema kwamba, Jukwaa hili limekuwa ni sehemu muhimu sana ya kufunga Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, kwa kukazia uekumene wa huduma makini kwa watu wa Mungu. Huu ni uekumene unaosimikwa katika ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko, kuelekea katika umoja kamili miongoni mwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Ni Jukwaa ambalo limekazia misingi ya haki na amani kama sehemu muhimu sana ya mabadiliko ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Makanisa yanapaswa kusoma alama za nyakati kwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa na ushuhuda wa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha.

Ni wakati wa kujibu kilio cha Mama Dunia na kilio cha Maskini kwa njia ya sera na mikakati makini ya kiuchumi, inayofumbatwa katika mwanga wa Injili ya matumaini. Imekuwa ni fursa ya utekelezaji wa “Waraka wa Uekumene wa Huduma” “Ecumenical Diakonia” uliochapishwa hivi karibuni. Haya ni matunda ya kazi ya pamoja iliyofanywa na Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani na Umoja wa Makanisa unaojulikana kama “Act Alliance”. Hapa, kipaumbele cha kwanza ni uchambuzi wa uekumene wa huduma unaopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa Makanisa ya Kikristo sehemu mbali mbali za dunia. Wakristo wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, maisha yao yanajikita katika ushuhuda wa huduma inayomwilishwa katika maisha na utume wa Makanisa ndani na nje ya mipaka ya Makanisa mahalia.

Waluteri
30 August 2020, 11:15