Tafuta

Bwana Maximino Caballero Ledo, ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Uchumi Vatican, SPE. Bwana Maximino Caballero Ledo, ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Uchumi Vatican, SPE. 

Maximino Callero Ledo: Katibu Mkuu Sekretarieti ya Uchumi Vatican

Baba Mtakatifu amemteua Bwana Maximino Caballero Ledo, mwamini mlei kuwa Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican. Bwana Maximino Ledo, alizaliwa huko Hispania kunako mwaka 1959, Ni mtaalam mbobezi katika masuala ya fedha na uchumi. Alijipatia shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu Madrid katika masuala ya uongozi wa biashara. Ameoa na ana watoto wawili.

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican, SPC, inaratibiwa na Baraza la Uchumi la Vatican lililoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 24 Februari 2014 kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Vigezo muhimu vinavyozingatiwa ni: huduma makini, ukweli, uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali fedha za Kanisa ambazo kimsingi ni kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa kuandaa bejeti ya Vatican na taasisi zake. Udhibiti wa matumizi ya fedha za Kanisa utaendelea kufanyika ili kuhakikisha kwamba, kiwango cha bajeti kilichotengwa kinaheshimiwa kama sehemu ya maboresho ya huduma kwa watu wa Mungu kwa kuzingatia nidhamu, tija, weledi na ufanisi bora.

Ni katika muktadha huu wa mageuzi makubwa katika sekta ya uchumi mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 4 Agosti 2020, amemteuwa Bwana Maximino Caballero Ledo, mwamini mlei kuwa Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican. Kabla ya uteuzi huu, Bwana Maximino Caballero Ledo, alikuwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Baxter Healthcare Inc., yenye Makao yake makuu nchini Marekani. Itakumbukwa kwamba Bwana Maximino Caballero Ledo, alizaliwa huko Mèrida, Badajoz, Hispania kunako mwaka 1959, ameoa na kubahatika kupata watoto wawili. Ni mtaalam mbobezi katika masuala ya fedha na uchumi. Alijipatia shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu Madrid katika masuala ya uongozi wa biashara. Kwa takribani miaka 20 ametekeleza shughuli zake nchini Hispania, Mashariki ya Mbali, Afrika na nchi kadhaa za Bara la Ulaya.

Kunako mwaka 2007, akahamishia makazi yake nchini Marekani, hadi kuteuliwa kwake. Bwana Maximino Caballero Ledo, katika mahojiano maalum na Vatican News anasema kwamba, kati ya kazi nyingi ambazo angeweza “kuchangamkia” hii haikuwemo hata kidoto katika ndoto zake. Kazi yake imekuwa ni fursa ya kuweza kukutana na watu wa kila aina, akakuza na kujenga ndani mwao, umoja unaofumbatwa katika utofauti, kama sehemu ya utajiri wa watu wa Mungu. Alifurahishwa sana na jinsi ambavyo Kanisa Katoliki nchini Marekani linavyowahusisha waamini wake katika maisha na utume wa Kanisa kwa hali na mali. Waamini wamekuwa wakarimu kiasi kwamba, wanaweza kulitegemeza Kanisa lao pamoja na kuendelea kutekeleza miradi inayohusiana na huduma za kijamii kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaosimikwa katika huduma kwa ajili ya waja wake.

Bwana Maximino Caballero Ledo anasema, baada ya Baba Mtakatifu Francisko “kutia nia” ya kutaka kumteua kuwa Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Uchumi, mawazo mengi yamemjia kichwani mwake hususan: familia na nyumba yake huko Marekani, lakini ameamua kupiga moyo konde na kukubali mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko, kwa kutambua heshima kubwa aliyomkirimia, lakini pia wajibu na dhamana tete iliyoko mbele yake. Ni matumaini yake kwamba, kwa kutumia karama, ujuzi, welezi na uzoefu wake katika masuala ya uchumi na fedha, ataweza kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Daima, sheria, kanuni na taratibu; ukweli na uwazi vikipewa kipaumbele cha kwanza, ili Sekretarieti ya Uchumi iweze kutekeleza vyema majukumu yake. Tangu sasa, anapenda kujiaminisha mikononi mwa Baba Mtakatifu katika utekelezaji wa majukumu yake kwa uaminifu na uadilifu mkubwa!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Novembe 2019, alimteuwa Padre Juan Antonio Guerrero Alves, S.I, kuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Uchumi Vatican. Akaanza rasmi kazi yake Mwezi Januari 2020. Kabla ya uteuzi huu, Padre Juan Antonio Guerrero Alves, kuanzia mwaka 2017 alikuwa ni Mshauri wa Mkuu wa Shirika la Wayesuit Ulimwenguni, Mratibu na mwakilishi wa Mkuu wa Shirika katika shughuli mbali mbali za Kanda ndani ya Shirika la Wayesuit, (DIR).

Papa: Uteuzi: Uchumi

 

 

05 August 2020, 07:09